Donald Trump na Vladimir Putin wamekutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza kabisa, na wakasalimiana kwa mikono huku mkutano wa G20 mjini Hamburg ukuanza.
Viongozi hao wa Marekani na Urusi wamesema wanataka kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambao uliathiriwa na tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa Marekani.
Masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na biashara yanatarajiwa kutawala mazungumzo katika mkutano huo mkuu wa siku mbili.
Kumeshuhudiwa maandamano katika barabara nje ya eneo ambapo mkutano huo unafanyika.
Mke wa rais wa Marekani Melania Trump ameshindwa kuondoka katika hoteli ambapo amekuwa akikaa katika jiji hilo la Ujerumani kutokana na maandamano.
Alikuwa amepangiwa kufanya matembezi mafupi pamoja na wake wengine wa marais wanaohudhuria mkutano huo.
Lakini msemaji wake Stephanie Grisham amesema: "Polisi wa Hamburg walikataa kuturuhusu tuondoke."
Polisi 76 wamejeruhiwa katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Mkutano wa G20 (Kundi la mataifa Ishirini) huwa ni mkutano wa nchi 19, zilizostawi na zinazostawi, pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).
Katika hotuba yake ya kufungua mkutano huo, Kansela Angela Merkel alisema : "Sote tunafahamu changamoto zinazoikumba dunia kwa sasa.
"Tunafahamu kwamba muda unayoyoma na kwa hivyo suluhu lazima itafutwe. Na suluhu inaweza tu kupatikana iwapo baadhi yetu tutalegeza baadhi ya misimamo yetu na kufanya kazi kwa pamoja ingawa si lazima tulegeze misimamo sana, bila shaka, kwa sababu tunaweza kuwa na misimamo tofauti kuhusu baadhi ya masuala."
Kutarajiwe nini kutoka kwa mkutano wa Trump na Putin?
Video fupi ambayo imepakiwa kwenye ukurasa wa Facebook wa serikali ya Ujerumani imeonesha wawili hao wakisalimiana kwa mikono.
Bw Trump anaonekana baadaye akiupigapiga mkono wa Putin kama anaupapasa hivi huku wawili hao wakitabasamu wakiwa na viongozi wengine.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana tena baadaye Ijumaa alasiri.
Haijabainika iwapo wawili hao watahutubia wanahabari baadaye au ni kwa kiasi gani wanahabari wataruhusiwa kufuatilia mkutano wa wawili hao.
No comments:
Post a Comment