Saturday, July 8

Abiria waomba kuruhusiwa kusafiri usiku


Morogoro. Abiria wa mabasi yanayotoka mikoa ya bara yanayopita mkoani Morogoro kuelekea jijini Dar es Salaam wameiomba serikali iruhusu mabasi ya abiria kusafiri baada ya saa sita usiku hasa katika maeneo ambayo sio hatarishi kwa usafiri wa wakati huo.
Abiria hao walitoa ombi hilo jana Ijumaa wakati wakizungumza na Mwananchi katika kituo cha mabasi Msamvu.
Wamelalamikia kitendo cha kuzuiwa kuendelea na safari hata kabla ya saa sita usiku na kubainisha kuwa kinasababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wengi.
Kwa muda mrefu sasa serikali imepiga marufuku mabasi ya abiria kuendelea na safari baada ya saa sita usiku hivyo baadhi ya mabasi yanayotoka mkoani Mwanza na Mbeya kuelekea Dar es Salaam yanalazimika kulala mkoani Morogoro.
Abiria Shiraji Nyanda alisema kulala njiani kunawaongezea wasafiri gharama na wale wenye watoto wanapata usumbufu zaidi.
"Nia ya serikali ni njema ya kuhakikisha usalama wa watu wake lakini kwa barabara ya Dar-Moro ni salama sana… wangeruhusu tu mabasi yaendelee na safari. Lakini kibaya zaidi tunazuiliwa hapa kabla hata ya hiyo saa sita," alisema Nyanda.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni zilizopo, mabasi ya abiria hayaruhusiwi kusafiri baada ya saa nne usiku.
Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jane Arnold, ambaye alikua anasafiri na watoto, alisema kulala kwenye basi na watoto kumemsababishia usumbufu na kumuongezea gharama za safari.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani wilaya ya Morogoro, Victor Ayo, alisema mabasi hayo yanazuiliwa Morogoro sit u kwa kuogopa kutenkwa, bali pia kwa usalama wa abiria na vyombo hivyo vya usafiri.
Akifafanua, alibainisha kuwa mabasi yanazuiliwa kusafiri usiku ili pia kupunguza ajali zinazoweza kutokea kutokana na uchovu wa dereva.
Alisema kwa wakati huo dereva anakuwa amechoka baada ya kuendesha gari kwa muda mrefu na barabara hiyo inakuwa na msongamano wa malori.
"Niwashauri tu abiria wawe wavumilivu katika hili kwani linafanyika kulinda usalama wao," alisema.
Ofisa huyo pia aliwataka madereva kutii sheria za usalama barabarani ili kulinda usalama wao na usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

No comments:

Post a Comment