Monday, June 12

Magufuli aitaka Acacia itubu na kuanza upya


Rais John Magufuli amesema iwapo kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia ikitubu na kukubali makosa yake, serikali ipo tayari kwa majadiliano lakini kwa sasa hakuna mchanga  wa madini utakaotoka nje ya nchi.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo (Jumatatu) Ikulu baada ya kukabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini.
Amewataka Acacia kuomba leseni upya lakini kwa makosa yaliyoonekana hawana budi kuilipa Serikali.
Pia amewataka wanasheria wa nchi hii wasimame pamoja kwani suala hili ni kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa hili.
Amemtaka Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, aunde timu ya wanasheria waaminifu, wasiokubali kuhongwa na kisha sheria hizo zipelekwe bungeni na zijadiliwe  
“Hata kama kipindi cha bunge kitaongezwa, lakini wanasheria wapitie sheria hizo kifungu kwa kifungu ili mradi lipatikane suluhisho,” amesema.
Ameongeza: “Tukiendelea kukaa kimya tutaliangamiza taifa, tutakuja kujibu mbele za Mungu ‘its so painful, really painful.”
Amesema ukienda maeneo mengi hapa Dar es Salaam, mikoani utaona jinsi Watanzania wanavyoishi katika mateso na hata wakati alipokuwa akipita mikoani kuomba kura za urais aliona mateso ya Watanzania. “Nilifikia wakati nikajiuliza naomba hii kazi ya nini.”

No comments:

Post a Comment