Sunday, November 20

Urefu wazuia matibabu yake MOI

KIJANA Baraka Elias (35), mwenye urefu wa futi 7.4 ambaye ameshindwa kufanyiwa matibabu ya kubadilishwa nyonga katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), amevunja ukimya na kueleza changamoto zilizosababisha ashindwe kupatiwa matibabu kutokana na urefu wake usiokuwa wa kawaida.
Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwa wazazi wake Mtaa wa Bwela, Pugu Majohe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana, Elias alisema madaktari wameshindwa kumtibu kwa sababu mashine za MOI hazilingani na urefu wake.
Alisema anatarajia kupewa rufaa ili akatibiwe nje ya nchi.
“Madaktari wamenieleza bado wanafanya mazungumzo na wenzao wanaoshirikiana nao kutoka nje ya nchi ili wajue ni nchi gani itakuwa tayari kunichukua kufanikisha matibabu yangu.
“Sielewi matibabu yatagharimu kiasi gani cha fedha, nitatumia muda gani na vifaa gani hadi kukamilika,” alisema.
Elias alisema alifikishwa katika taasisi hiyo, Aprili mwaka huu baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma.
Akizungumzia chanzo cha tatizo lake, Elias alisema alipata hitilafu ya nyonga baada ya kuanguka kwenye ngazi za nyumbani kwake mkoani Ruvuma na tangu wakati huo hakuweza kuendelea kufanya shughuli zake za kiuchumi.
Alisema baada ya muda kidogo alipelekwa Hospitali ya Peramiho ambako alifanyiwa kipimo cha X-ray na kuonekana nyonga yake ilikuwa imevunjika.

ALIVYOPOKEA RIPOTI YA MOI
Elias ambaye muda wote anaonekana kuwa mchangamfu, alisema taarifa aliyopatiwa na madaktari wa MOI kwamba anapaswa kupewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi aliipokea kwa mtazamo chanya.
“Niliona ni hali ya kawaida kwa sababu kupewa rufaa ni mfumo wa kawaida wa kimatibabu, madaktari wana utendaji wao… wanapoona wameshindwa wanakupeleka kwingine ambako unaweza kupata msaada zaidi na ndiyo maana nilitolewa Peramiho kuja MOI.

HAWEZI KUPANDA DALADALA
Alisema kwa sasa hawezi kupanda daladala kutokana na urefu wake kwani kukaa kwenye kiti huwa ni changamoto kubwa kwake kwa sababu siti zake zimetengenezwa kwa kujibana.
“Zamani nilipokuwa mzima nilikuwa napanda daladala, nilikuwa napata shida kukaa, jinsi zilivyotengenezwa hazina nafasi ya kutosha tofauti na gari za wenzetu (wazungu) zimetengenezwa kwa kuachanishwa nafasi mtu yeyote anaweza kukaa bila usumbufu,” alisema.

UREFU KWENYE DNA
Elias alisema wazazi wake wamemweleza kuwa urefu alionao ni wa kurithi kutoka kwenye kizazi chao, kwani hata mababu zake wapo ambao walikuwa warefu.
“Wazee hao wanatoka katika pande zote mbili, yaani kwa baba na kwa mama, sijui watu wananichukuliaje jinsi nilivyo, binafsi najiona kawaida na wengine kwa sababu hata hapa nyumbani hakuna aliye mrefu zaidi yangu,” alisema.

CHANGAMOTO
Alisema changamoto kubwa anayokabiliana nayo hivi sasa ni usafiri wa kumtoa nyumbani hadi Muhimbili kupata matibabu.
“Huwa tunalazimika ama kukodi gari kutoka nyumbani hadi hospitalini au tunaazima la mtu tunaweka mafuta,” alisema.

KUPANDA NDEGE
Elias alisema iwapo rufaa itapatikana hahofii kama atashindwa kuingia ndani ya ndege kwa safari ya matibabu nje ya nchi.
“Kama nilivyoeleza awali, wazungu huwa wanafikiri mbali, wanafanya vitu vikubwa. Huko kwenye nchi zao wapo warefu zaidi yangu na wanapanda ndege kama watu wengine.
“Hata gari zao wanazotengeneza siku hizi ni za tofauti, hivi karibuni tu Japan ilitoa hizi gari ndogo ambazo zina uwezo wa kusogeza kiti nyuma na ukakaa vizuri, najua nitaweza kuingia ndani ya ndege,” alisema.

AOMBA MSAADA
Elias alisema ingawa kanisa analoabudu linashirikiana naye bega kwa bega, msaada mkubwa kwake umebaki kwa familia yake.
Kutokana na hali hiyo, anaomba msaada kutoka kwa mtu, mashirika au taasisi yoyote itakayoguswa na mkasa wake.
“Siwezi kufanya kazi, kila siku nahitaji fedha za matumizi, nahitaji msaada, naamini wapo watakaoguswa, nipo tayari kwa msaada wowote kwa sababu nina changamoto nyingi, naumwa sijui lini nitapata matibabu, nategemea majibu ya madaktari,” alisema.

No comments:

Post a Comment