Sunday, November 20

Mabilioni ya fedha Kagera yaiibua Serikali


*Ni baada ya watu kuhoji ujenzi wa miundombinu
* Ofisi ya Waziri Mkuu yasisitiza msimamo uko palepale
Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya kuenea taarifa za kuyeyuka mabilioni ya fedha yaliyochangwa na wasamaria wema kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Serikali imeibuka na kutoa taarifa juu ya sakata hilo.
Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi sasa Serikali imetumia Sh bilioni 1.13 kukarabati miundombinu na si kuwajengea au kukarabati nyumba wananchi ambao wanaishi kwenye mahema.
Aidha, Meja Jenerali Kijuu aliendelea kushikilia msimamo wa Serikali kuwa kila mwananchi aliyeathirika na tukio hilo, ajihudumie na kukarabati nyumba yake mwenyewe.
mkuu-wa-mkoa-mhe-kijuu-akiongoza-zoezi-la-kugawa-mahitaji-kwa-wahanga-laeo-jioniAlisema Serikali tayari imekusanya Sh bilioni 5.428 kutoka kwa watu, taasisi na mashirika mbalimbali, waliotikia wito wa kusaidia waathiria wa tetemeko hilo lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
Kijuu alisema fedha hizo zilivunwa kupitia akaunti maalumu ya maafa iitwayo ‘Kamati Maafa Kagera’ na michango mingine kupitia mihamala ya fedha ya simu za mkononi.
Baada ya taarifa ya Kijuu kutoka, iliibua maswali na mjadala mkali, hasa katika mitandao ya kijamii, ambako wachangiaji wengi walihoji kwanini fedha hizo hazijawafikia walengwa hadi sasa, huku wakibaki kutaabika.
Kutokana na mjadala huo kushika kasi kila kukicha, jana Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na  Bunge), Uledi Mussa, alilazimika kutoa ufafanuzi wa Serikali namna ambavyo imeshirikina na wadau kuchukua hatua kubwa za kuwasaidia waathirika na kwamba bado inaendelea kufanya hivyo.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, Serikali ilikuwa imepokea misaada ya vifaa, vyakula, fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya Sh bilioni 15.19.
Mussa alisema pamoja na misaada hiyo, tayari Serikali imetoa matibabu bure kwa majeruhi wote 560, imeandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki dunia katika tetemeko hilo, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alihudhuria.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau ilitoa mkono wa pole wa Sh milioni 1.8 kwa kila familia iliyopatwa na msiba. Imeendelea kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwamo chakula, dawa, nguo, makazi ya muda, huduma za tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa waathirika katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera zilizopata athari,” alisema.
Alisema Serikali imeendelea kufanya tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka ya athari za tetemeko hilo ili kubaini maeneo zaidi ya kuwasaidia wananchi kwa kushirikiana na ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali, wakiwamo Msalaba Mwekundu, Plan International (T), BRAC(T), World Vision, CARITAS, Save the Children, JH Piego na Benki ya Dunia.
“Tathmini za wataalamu, makadirio ya awali yanaainisha Sh bilioni 104 zinahitajika kukabiliana na kurejesha hali katika Mkoa wa Kagera. Gharama hizo zinajumuisha ujenzi wa makazi ya muda kwa waathirika wa nyumba zipatazo 16,667 zilizoharibika katika viwango tofauti, ambapo kiasi cha Sh bilioni 41.7 zinahitajika.
“Sh bilioni 1.92 kwa ajili ya kodi ya miezi sita kwa wapangaji waliokuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoharibika, ukarabati wa shule za msingi 163 kwa gharama ya sh bilioni 12.7, sekondari 57 kwa gharama ya Sh bilioni 45.65, vituo vya afya na zahanati 32 kwa gharama ya Sh milioni 772 na majengo ya taasisi nyingine 20 kwa Sh bilioni 1.3,” alisema.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, Serikali imepokea misaada ya vifaa, vyakula, fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya Sh bilioni 15.19 kutoka kwa wadau mbalimbali, washirika wa maendeleo, balozi na nchi marafiki. Tayari misaada hiyo imeshagawiwa na inaendelea kusambazwa kwa walengwa.
“Mchanganuo wa misaada hiyo iliyopelekwa ipo kama ifuatavyo: Fedha taslimu kiasi cha Sh 5,412,984,934.82 kimeshapokelewa kupitia benki. Kiasi cha Sh 17,579,427.00 kupitia mitandao ya simu, ahadi za Sh 6,703,000,000. Hivyo jumla ya ahadi na fedha taslimu hadi sasa ni Sh 12,133,564,361.82,” alisema.
Alisema Serikali pia imepokea misaada mingine yenye thamani ya Sh bilioni 2.25, ikiwamo unga tani 58.12, sukari mifuko 1,150, mchele tani 133.96, maharage tani 19,666, mahindi tani 70.1, majani ya chai tani 3, maji katoni 1,570, mafuta lita 6,022, sabuni katoni 443, shuka 495, blanketi 6,125, magodoro 1,146, mahema 367 na turubai 6,237.
Aliongeza: “Serikali imepokea pia vifaa vya ujenzi vikiwamo saruji mifuko 24,233, bati 20,933, misumari kilo 145, nondo vipande 725, kofia za bati 150 na mbao 250.
“Ifahamike baadhi ya waliotoa ahadi kama Serikali ya Uingereza, wameahidi kutekeleza ahadi zao kwa kujikita moja kwa moja katika ujenzi wa shule, baada ya Wakala wa Majengo kuainisha viwango na gharama. Aidha Serikali inaendelea kupokea michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa lengo la kusaidia waathirika hawa.”

HATUA ZA KUREJESHA HALI
Mussa alisema tangu kutokea kwa maafa hayo, Serikali imeendelea kufanyia kazi masuala muhimu yaliyoainishwa katika tathmini ya tetemeko.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, licha ya kuendelea kuwapatia wananchi mahitaji muhimu kama chakula, dawa na misaada ya kujikimu katika makazi ya muda, kiasi cha Sh 969,238,326.35, mifuko ya saruji 17,423, bati 5,348 na misumari kilo 1,107 vilitumika kwa kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa shule za msingi na sekondari.
“Juhudi hizi ziliwezesha wanafunzi wa shule hizo waliokuwa katika hatari ya kukosa masomo kuendelea na masomo yao. Gharama hizo pia zimejumuisha ukarabati wa zahanati katika halmashauri za Mkoa wa Kagera, na kuanza kwa ujenzi wa kituo kipya cha afya (Ishozi/Kabyaile) kitakachojumuisha chumba cha upasuaji na wodi ya kinamama na watoto kwa faida ya wananchi wote wa maeneo hayo.
“Pia Serikali imegharamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara, maji, na umeme katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa na tetemeko,” alisema.
Alisema Shirika la Word Vision kwa kushirikiana na Serikali tayari limetoa mifuko ya saruji 2,300 yenye thamani ya Sh 39,000,000 kwa kaya 460 zilizobomokewa nyumba na zilizoonekana kuwa na uhitaji zaidi. Katika awamu ya kwanza kila kaya ilipata mifuko mitano ya saruji.
“Na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili umeanza, inatarajiwa kugawiwa mifuko ya saruji 10,645 yenye thamani ya Sh milioni 164.9 kwa kaya 2,129. Tumeainisha pia kaya nyingine zilizoathirika zaidi zipatazo 370 za watu waliomo kwenye makundi maalumu (wazee, wajane na walemavu), ambao watapatiwa vifaa vya ujenzi (mabati 20 na mifuko mitano ya saruji kwa kila kaya) kukarabati nyumba zao,” alisema.
Aliongeza: “Serikali inapenda kusisitiza tena kwa wananchi, maafa ya tetemeko hayakupangwa wala kutokea kwa nguvu za mwanadamu bali majanga ya asili, hivyo wakati juhudi zikiendelea kusaidia zaidi pale panapowezekana, wananchi wanaendelea kuombwa kufanya jitihada zao binafsi za kurejesha makazi yao katika hali yake ya awali.
“Serikali inawapongeza wananchi wengi ambao tayari wameitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli aliyewaasa kuanza ujenzi wa nyumba zao kwa kuwa Serikali isingeweza kumjengea nyumba kila mwathirika.
“Kwa sababu ingawa michango na misaada hii japo haijafikia lengo la Sh bilioni 104.9 zinazohitajika kurejesha hali nzima ya Kagera, itaendelea kutumika kwa uadilifu na uwazi kwa faida ya waathiria wenyewe,” alisema.
Tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17, watu 252 walijeruhiwa, nyumba 840 zilianguka na nyingine 1,264 zilipata nyufa.

No comments:

Post a Comment