RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete, jana amezuiwa na maofisa wa Serikali kusafiri nje ya nchi kutokana na miongoni mwa wajumbe wanne aliokuwa ameongozana nao kutokuwa na viza.
Taarifa zilizofika chumba cha habari jana jioni, zilidai kuwa Kikwete ambaye pia alikuwa ameongozana na mke wake, Salma alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo lilitokea saa 10:00 jioni na hivyo Kikwete pamoja na ujumbe wake huo kukwama kusafiri.
Chanzo kimoja kilichopo uwanjani hapo, kililidokeza gazeti hili kuwa Kikwete pamoja na ujumbe wake huo, walikuwa wakielekea nchini Dubai na ilikuwa wasafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.
“Kikwete kama Kikwete yeye hakuwa na shida kwa sababu ana Diplomatic Passport, watu wengine ndio hawakuwa na viza.
“Kwa kawaida International flight (ndege za kimataifa) kaunta zinafungwa saa moja kabla ya ndege kuruka, na ndege waliyokuwa waondoke nayo ilikuwa inaondoka saa 10:30 jioni, viza za hao watu zilikuja saa 10:00 wakati kaunta zikiwa zimefungwa,” kilisema chanzo hicho.
Kilisema kwa kiongozi kama Kikwete, linapotokea tatizo kama hilo, wakati mwingine unaweza kupiga simu kwa watu wa Uhamiaji huko anakoelekea, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu tayari ndege ilikuwa imeondoka.
Haijajulikana mara moja kilichosababisha kutotumiwa utaratibu wa kupiga simu kama inavyoelezwa, ikitokea kiongozi mkubwa kama Kikwete au wasaidizi wamekwama kukamilisha taratibu fulani fulani za kusafiri nje ya nchi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, huenda Kikwete na ujumbe wake wakasafiri leo baada ya kuwa wamekamilisha taratibu zote.
Taarifa kutoka kwa wasaidizi wa Kikwete, zilidai kuwa wakati tukio hilo linatokea uwanjani hapo, rais huyo mstaafu hakuwa amefika bali wasaidizi wake ingawa tayari mizigo ilikuwa imekwishapandishwa ndani ya ndege.
Inaelezwa kuwa baada ya safari hiyo kukwama mizigo hiyo ilishushwa.
Taarifa nyingine zilidai kuwa wakati tukio hilo likitokea, Kikwete alikuwa uwanjani hapo na kwamba kwa kawaida mizigo isingepandishwa kama muhusika hayupo.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wasaidizi wa Kikwete, alisema wajumbe ambao hati zao ama zilikuwa na kasoro au hazijakamilika ni wasaidizi wake.
Alisema Kikwete, mke wake pamoja na wasaidizi wake, walikuwa wanaelekea Abudhabi na walikuwa wapande ndege hiyo ya Emirates Dubai na kisha kuendelea na usafiri mwingine.
Msaidizi wake huyo alisema taratibu zote zilikamilika ingawa walikiri kuwa walikuwa wamechelewa.
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta ndugu wa karibu na Kikwete ambaye alithibitisha kuwa alikuwa anasafiri, lakini hakuwa na habari za kukwama kwake.
Zipo taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazodai kuwa imekuwa ni kawaida kwa wasaidizi wa Kikwete kusafiri nje ya nchi bila viza, na kwamba tukio la safari ya jana kukwama lisingetokea kama utaratibu huo haungekuwapo.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Msemaji wa JNIA, Nuru Nyoni azungumzie sababu za Kikwete na ujumbe wake kukwama, alisema suala hilo lipo chini ya Uhamiaji.
“Siwezi kuzungumzia mimi, hili suala lipo chini ya Uhamiaji, labda uwapigie Uhamiaji, pia hata uthibitisho siwezi kutoa maana leo ni weekend sijafika ofisini,” alisema Nuru.
Alipotafutwa Ofisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji, Abasi Ilovia, kupitia simu yake ya kiganjani, aliomba apigiwe baada ya dakika kumi ili aweze kuwasiliana na watu waliopo JNIA kwa taarifa zaidi.
Ilovia alipopigiwa tena baada ya muda huo, alisema anasubiri majibu kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Ndege.
No comments:
Post a Comment