Friday, October 28

Maajabu matokeo ya darasa la saba


Dar/Shinyanga. Matokeo ya darasa la saba mwaka huu yameacha kicheko kwa Shule ya Msingi Kwema Modern iliyopo Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kitaifa.
Shule hiyo imefanya maajabu kwa kutoa wanafunzi saba katika orodha ya watahiniwa 10 bora kitaifa.
Hata hivyo, wanafunzi 238 wamefutiwa matokeo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya baadhi ya wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule na walimu wakuu kuwapatia majibu na kubainika kuwa yanayofafana.
Pia, wanafunzi 21 watarudia mitihani yao kutokana na sababu mbalimbali kama maradhi.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema watahiniwa 555,291 (sawa na asilimia 70.36) wamefaulu kati ya 789, 479 waliofanya mtihani huo Septemba mwaka huu.
Matokeo hayo yanaonyesha kiwango cha ufaulu mwaka huu kimepanda kwa asilimia 2.52 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2015 ambao ulikuwa asilimia 67.84.
Mbali ya Kwema kuwa shule ya kwanza kwa matokeo ya jumla, imetoa mtahiniwa bora wa kwanza kitaifa.
Mtahiniwa huyo, Japhet Elia (12) ambaye anatoka familia ya wakulima mkoani Kigoma, amefuatiwa na wenzake wawili, Jamal Ally na Enock Daud pia wa shule hiyo walioshika nafasi ya pili na tatu.
Dar, Shinyanga zachuana
Tofauti na matokeo ya mwaka 2015 ambayo shule za Kanda ya Ziwa zilitamba, mwaka huu mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga imechuana vikali.
Kwa mujibu wa Dk Msonde, Dar es Salaam imeibuka kinara kwa kutoa shule nyingi katika orodha ya shule 10 bora, huku Shinyanga ikiongoza kwa kutoa wanafunzi wengi bora kitaifa.
Alisema Dar es Salaam imetoa shule nne kati ya 10 bora, ikifuatiwa na Shinyanga yenye shule mbili.
Katika orodha ya wanafunzi bora kitaifa ambayo mwaka huu imetawaliwa na wahitimu tisa wa kiume na mmoja wa kike, Shinyanga imeongoza kwa kutoa wanafunzi saba kati ya 10. Dar es Salaam imefuatia kwa kutoa wahitimu wawili na Kagera mhitimu mmoja.
Mikoa hiyo pia imechuana vikali katika orodha ya wanafunzi bora kitaifa kwa jinsia. Wakati Dar es Salaam ikitoa wanafunzi watano kati ya kumi kwa upande wa wasichana, Shinyanga imeongoza kwa wavulana kwa kutoa wanafunzi wanane.
Shule 10 bora
Dk Msonde alizitaja shule 10 bora kwa kigezo cha kuwa na wanafunzi 40 na zaidi kuwa ni Kwema (Shinyanga), Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy (Dar es Salaam), Tusiime (Dar es Salaam), Mudio Islamic (Kilimanjaro), Atlas (Dar es Salaam), St Achileus (Kagera), Gift Skillfull (Dar es Salaam) na Carmel (Morogoro).
Shule zilizofanya vibaya ni Mgata (Morogoro), Kitengu (Morogoro), Lumba Chini (Morogoro), Zege (Tanga), Kilole (Tanga), Magunga (Morogoro), Nchinila (Manyara), Mwabalebi (Simiyu), Ilorienito (Arusha) na Chohero (Morogoro).
Ushirikiano siri ya ushindi
Mkurugenzi wa Shule ya Kwema Modern, Pauline Mathayo alisema mafanikio waliyopata yanatokana na ushirikiano wa karibu uliopo shuleni hapo kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
Pia, alitaja siri nyingine kuwa ni kufuata miongozo ya elimu wanayopewa na Serikali.
Baba, mwana washangaa
Katika kile kinachoonekana ni kutoamini kilichotokea, Elia Stephano, mzazi wa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, alisema hakutegemea kama mwanawe angeweza kupata mafanikio hayo makubwa, licha ya kuwa amekuwa na nidhamu kubwa tangu akiwa mdogo.
“Ukweli baada ya kuelezwa hivyo kwamba mtoto wangu amekuwa wa kwanza kitaifa, nilianza kutetemeka kwa furaha,” alisema Stephano anayejishughulisha na kilimo na ujasiriamali mkoani Kigoma.
“Hayakuwa mategemeo yangu ingawa nilikuwa namwamini mtoto wangu. Lakini si kwa kiasi cha kuwa mshindi wa kwanza kitaifa.”
Alisema mtoto wake anapenda kusoma na kufundisha wenzake huku mara nyingi akipenda kumuomba Mwenyezi Mungu.
Mtoto aliyeongoza kitaifa, Japhet alisema pamoja na kufanya vizuri kwenye mitihani alipokuwa akisoma, hakuwa na matarajio ya kushika nafasi ya kwanza.
“Namshukuru Mungu kwa matokeo hayo. Pia, nawaomba watoto wenzangu katika mambo yao yote wamtangulize Mungu kwa kila jambo hata kama wana uwezo binafsi,” alisema Japhet huku akieleza kuwa ndoto yake ni kuwa mhandisi wa ndege.
Tusiime wazungumza
Akizungumzia matokeo ya mwanafunzi wa kike aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa wasichana Justina Gerald, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Tusiime, Philibert Simon alisema siri ya mwanafunzi huyo kufanya vizuri ni usikivu, nidhamu na uchu wa kujifunza.
Simon alisema msichana huyo ambaye pia ameshika nafasi ya nne kitaifa, alikuwa akifanya vizuri katika mitihani yake shuleni hapo.
Alisema wakati akiwa darasa la saba aliongoza mara 19 katika mitihani 32 waliyofanya wanafunzi hao. Akishuka sana amekuwa wa pili,” alisema Simon.
Udanganyifu
Licha ya ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.5 katika mitihani ya darasa la saba, matokeo yametiwa dosari na udanganyifu uliojitokeza wakati wa uendeshaji wake.
Msonde alisema wakati wa mitihani hiyo, matukio machache ya udanganyifu yalifanywa na baadhi ya wasimamizi, wamiliki wa shule na walimu wakuu.
Udanganyifu uliofanyika unahusisha wamiliki na walimu wa shule kuiba mtihani na kuandaa majibu kwa ajili ya wanafunzi, walimu kuwasaidia wanafunzi kufanya mtihani, walimu kuwapa majibu wanafunzi na kufanana kwa majibu kusiko kwa kawaida.
Kwa mfano, katika shule ya Tumaini, Sengerema mkoani Mwanza, mmiliki wa shule aliandaa majibu ambayo watahiniwa waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mitihani.
Katika shule ya Mihamakumi wilayani Sikonge, mwalimu mkuu na walimu wengine waliwafanyia watahiniwa mitihani lakini baadaye maafisa wa Takukuru waliwakamata.
Msonde alisema tukio jingine la udanganyifu lilifanywa Shule ya Msingi Qash wilayani Babati, Manyara ambapo mwalimu alijificha chooni, kupokea maswali kutoka kwa watahiniwa na kuandaa majibu ili kuwapa wanafunzi.
Katika shule ya St Getrude mkoani Ruvuma, mwalimu mkuu na walimu wengine walijificha mabwenini na watahiniwa walijifanya wanaomba ruhusa ya kwenda chooni, kisha walienda mabwenini kuchukua majibu na kuyasambaza ndani ya chumba cha mtihani.
Shule nyingine zilizohusika katika udanganyifu huo ni Tumaini iliyopo Halmashauri ya Sengerema (kuiba mtihani na kuandaa majibu), Little Flower Halmashauri ya Serengeti (kuiba mitihani na kuandaa majibu).
“Necta imewafuta matokeo yote watahiniwa 238 kutoka shule sita za mikoa tofauti tofauti waliobainika kufanya udanganyifu na tumezishauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wote waliohusika kulingana na kanuni za utumishi na sheria za nchi,” alisema Msonde.
Aliongeza kuwa Necta haitamvumilia mtumishi yeyote anayevunja kanuni na sheria za nchi kwa kuvuruga usimamizi wa mitihani ya Taifa.
Imeandikwa na Shija Felician, Suzan Mwillo na Ephrahimu Bahemu.

Sumaye apewa notisi ya siku 90 kuendeleza mashamba


Dar es Salaam. Serikali imemtaka Frederick Sumaye kuendeleza mashamba yake mawili ndani ya siku 90, la sivyo itafuta hati ya umiliki wake, lakini waziri mkuu huyo mstaafu amesema notisi hiyo ni matokeo ya chuki ya Serikali dhidi yake baada ya kuhama CCM na kujiunga Chadema.
Sumaye, ambaye alikuwa mmoja wa wasemaji tegemeo kwenye mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anamiliki shamba lililoko mkoani Morogoro na jingine lililoko Mabwepande jijini Dar es Salaam, ambalo limevamiwa na wananchi.
Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alisema hati ya shamba la Sumaye iko katika hatua ya kufutwa na kwamba Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni, Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi.

Sita wafutiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa



Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imewafutia adhabu ya kunyongwa hadi kufa na kuamuru kuachiwa huru watu sita waliohukumiwa kwa mauaji  ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na mfanyakazi wa Benki ya NMB, tawi la Wami Morogoro.

Uamuzi huo ulisomwa jana na Jaji Projest Rugazia wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam baada ya kutolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande. Wengine ni Jaji Ibrahimu Juma na Jaji Augustine Mwarija.

Jopo hilo lilikubali hoja za warufani waliowakilishwa na mawakili Richard Rweyongeza, Majura Magafu, Barnabas Luguwa, Samson Mbamba na Gabinus Galikano kuwa Mahakama Kuu ilikosea kuwatia hatiani kwa kuwa haikuwa na ushahidi wa kutosha.



NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2016 EXAMINATION RESULTS

http://necta.go.tz/matokeo/2016/psle/psle.htm

MATOKEO YA MTIHANI WA DARASA LA SABA 2016 – PSLE-2016 EXAMINATION RESULTS

Wednesday, October 26

Wachina Wawili Wadakwa kwa Kumteka Mwenzao

DAR ES SALAAM: JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata Wachina wawili, Wang Young Jing (37) Chen Chung Bao (35) kwa makosa ya utekaji nyara jijini Dar katika eneo la Palm Beach Hotel.


Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, CP Simon Sirro, akilionyesha gari hilo lililokuwa limeibwa kwa wanahabari (hawapo pichani).
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, CP Simon Sirro, amesema watu hao walimteka raia wa China mwanamke aitwaye  Liu Hong (48) ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa  Le Grande Cassino waliyemteka Oktoba 23 mwaka huu ambapo  polisi walimkuta akiwa ndani ya chumba cha Hotel ya Palm Beach iliyoko Upanga jijini Dar es Salaam na walimkamata pia mtu aliyekuwa amekodi chumba hicho.

…Akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).
Alifafanua kuwa Oktoba 24 majira ya saa kumi na moja jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha polisi kilifanikiwa kumtia nguvuni raia mmoja  wa China akiwa ndani ya chumba cha hoteli hiyo baada ya kuvunja mlango.


Madawa ya kulevya aina ya mirungi yaliyokamatwa na jeshi la polisi kwenye operesheni hiyo.
Sirro alisema baada ya kufungua chumba hicho walimkuta raia aliyetekwa akiwa hajitambui na akiwa na majereha usoni, pia palikutwa vipande vya taulo vyenye damu vilivyotumika kumfungia mikono ambapo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Ameeleza kuwa sababu kubwa ya utekaji nyara huo ilikuwa kumtaka majeruhi huyo atoe YEN 100,000 ambazo ni  sawa na dola za Marekani 19,000.
…Sirro akionyesha mitambo ya kutengenezea pombe aina ya gongo iliyokamatwa wakati wa operesheni.
Katika hatua nyingine Sirro amesema kuwa wamefanikiwa kukamata wezi wa magari na kupatikana kwa gari la ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mkoa wa Morogoro, Capt. Innocent  Philipo Dallu ambaye alikuwa ameegesha gari lake maeneo ya Mbezi Juu akitokea kanisani  kwa ajili ya kuingia kwenye duka la vifaa vya ofisini na mashuleni ambapo gari hilo liliporwa.
…Akionyesha baadhi ya funguo bandia zilizokamatwa katika oparesheni hiyo.
Amesema jeshi lake  limefanikiwa kulikamata gari hilo aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 400 DEH huko Kiwangwa, Bagamoyo mkoani Pwani likiwa na watu wawili ambao ni  Ezekiel David (25) na Geofrey Nkwabi (52) na upelelezi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.


Mwijage Kuzindua Maonyesho ya Magari Dar


Mratibu wa maonyesho hayo, Ally Nchahaga (wa kwanza kulia) akizungumza na wanahabari.
WAZIRI  wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, atakuwa mgeni maalum katika kuzindua tamasha la  maonyesho magari nchini lijulikanalo kama Automotive Festival (Autofest) linalotarajiwa kuonyesha magari mapya na ya kisasa katika viwanja vya Biafra, Kinondoni,  jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 28 hadi 30 mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mratibu wa Maonyesho hayo, Ally Nchahaga, amesema tamasha hilo litakuwa na matoleo mapya ya kila aina ya magari kama vile magari ya abiria, ya biashara, bodi za magari, mashine zinazohusiana na magari sambamba na pikipiki za kisasa na burudani mbalimbali za kusisimua zitakazofanywa katika kuyaendesha magari na kurukisha pikipiki juu kwa mbwembwe na kadhalika.
“Tukio hili linahusisha moja ya maonyesho muhimu na yenye mvuto katika ulimwengu wa vyombo vya moto na lengo letu ni kuendelea kuleta aina mbalimbali ya bidhaa za vyombo vya moto na huduma kwenye ‘Autofest’ ili wadau wapate kujifunza na  kufurahia na kukidhi tamaa yao kwani magari yatakayokuwepo yanatumia teknolojia mpya na si ya zamani,” alisema Nchahaga.
Aidha alitaja viingilio katika tamasha hilo kuwa ni 10,000/= kwa sehemu ya kawaida, 5,000/= kwa watoto,  40,000/= ni kwa tiketi za  VIP na 100,000/= kwa tiketi za musimu.
Kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Kuendesha tunaelekea wiki ya usalama barabarani, ni muhimu madereva kutoa fursa kwa madereva wenzao hata kama una haki”.

MFALME MOHAMMED VI WA MOROCCO AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA MSIKITI


Mfalme Mohammed VI wa Morocco akibusu Masahaf kabla ya kumkabidhi Waziri Mkuu Kasim Majaliwa katika hafla fupi ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti kwenye eneo la BAKWATA Kinondoni jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016.  Kulia ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Abukary Zubeir. Jumla ya Masahaf 10000 zilikabidhiwa na Mfalme huyo.(Picha n Ofisi ya Waziri Mkuu)


Mfalme Mhammed  VI wa Morocco na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakishuhudia wakati Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zubeir (kulia)  akitia saini Makubaliano ya ujenzi wa Msikiti kwenye eneo la BAKWATA, Kinondoni jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Mfalme   Mohammed VI wa wa Morocco,  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Rais Mstaafu Alhaj  Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohammed Bilal wakiwa katika hafla fupi ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa msiki uliofnywa na Mfalme Mohammed wa Morocco kwenye  eneo la BAKWATA, Kinondoni jijini Dar es salam Oktoba 25, 2016. (icha na Ofisi ya Waziri Mkuu)