Watu wakiwa wamekusanyika katika makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi
wakati msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,
Edward Lowassa ulipokuwa ukielekea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kuchukuwa fomu za urais, Dar es Salaam
Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsindikiza wakati akienda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ni salamu kwa CCM na ‘wameisoma namba’ kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.
Akiwahutubia mamia ya wafuasi wa vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Lowassa aliyeonekana kuwa na furaha muda wote, alisema maandamano waliyoyafanya hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Haijatokea katika historia ya nchi yetu maandamano makubwa ya aina ile, nimefurahishwa na vijana wametembea kutoka Buguruni hadi Kinondoni na hamjachoka nawapongeza sana, asante sana,” alisema Lowassa.
Alisema ana mambo mawili ya kusema; kwanza kuwashukuru wafuasi na wapenzi wa Ukawa kwamba kwa kujitokeza kwa wingi wamepeleka meseji moja kwa wasiowatakia mema, wanaosema CUF na Chadema ni watu wenye fujo, wamethibitisha kwamba si kweli.
“Tumewahakikishia kuwa sisi ni watu wenye nidhamu na uwezo, Mwenyezi Mungu akipenda Oktoba tunachukua nchi asubuhi peupeee, kwa hiyo watu wasitafute visingizio, watafute vingine, watoto wa mjini wanasema wameisoma namba,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akizungumzia jambo la pili, mbunge huyo wa Monduli aliyejiondoa CCM siku 15 zilizopita, alisema anauchukia umaskini kiasi kwamba anauona kama ukoma.
Lowassa ambaye mara nyingi husema hajakutana barabarani na Rais Jakaya Kikwete, alisema rafiki yake huyo ndiye aliyeharibu uchumi wa nchi, lakini akasema asingetaka kutoa mashtaki bali kutoa takwimu za hali ilivyobadilika.
“Wakati Rais Benjamini Mkapa anaondoka madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo ni Sh2,300, kutoka 650 hadi 2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?” aliuliza na kujibiwa, “ameharibuuu.”
“Bei ya mchele ilikuwa Sh550 leo Sh2,200, ameharibu uchumi, hakuharibu? Sembe kilo ilikuwa Sh250 leo ni Sh1,200, ameharibu hakuharibu?” alihoji Lowassa na watu wakamjibu ‘ameharibuuu” na kisha akaongeza kuwa kwa sababu hizo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Lowassa alitumia fursa hiyo kuwaalika wanachama wa CCM wasioridhika na hali ilivyo kujiunga na Ukawa kwa kuwa inawezekana kutafuta mabadiliko nje ya chama hicho na kwamba wasione haya bali waangalie idadi kubwa ya vijana waliojitokeza jana.
Mgombea huyo, alisema Tanzania imeshuhudia uporaji mkubwa wa mali za Taifa, ambapo tembo wameuawa kuliko wakati mwingine wowote, hivyo kutokana na vitendo hivyo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Kuhusu kutunza shahada za kupigia kura, Lowassa alisema Wanaukawa hawapaswi kufanya mchezo kwa kuwa CCM imekuwapo madarakani muda mrefu watatumia kila kitu ndani ya uwezo wao kubaki madarakani.
“Na sisi tutumie kila kitu kilicho ndani ya uwezo wetu kuingia madarakani. Kitakachotuingiza madarakani ni kura, hifadhi shahada yako, shawishi na wengine, tarehe 25 Oktoba tunawatoa madarakani,” alisema.
Alisema amesikia maneno kuwa kuna mchezo wa watu wanapita mitaani wanachukua shahada za kupigia kura za wanajeshi, askari magereza wanachukua namba.
Alimuhoji mmoja wa wanasheria wa Chadema, Mabere Marando iwapo kama amesikia taarifa hizo, naye akajibu: “Kwa niaba ya wanasheria wote wa Chadema tunaahidi kitu kimoja, njama zote walizonazo kujaribu kuhujumu kura za Lowassa tutazidhibiti, njama zote walizonazo kuhujumu ushindi wa wabunge wetu tutazidhibiti, njama zote walizonazo kujaribu kudhibiti ushindi wa madiwani tutazidhibiti.”
Marando alisema mawakala wote wa vyama hivyo wanapaswa kupeleka matokeo ya vituo vyote baada ya kubandikwa saa 12 jioni na kwamba yeye hatasubiri atatangaza badala ya kusubiri saa saba usiku.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema maandamano yaliyofanyika jana ni historia mpya ambayo ni elimu kwa Watanzania. Ari iliyoonyeshwa tangu asubuhi inasadifu hamu ya Watanzania.
Pia, alisema Rais Kikwete ametangaza kuwa wapinzani ni maadui na kumtaka kuangalia lugha anayoitumia, kwa kuwa Ukawa watajibu kwa hoja na si matusi.
“Ninamhusia sana Rais Jakaya Kikwete amebaki na siku 75 tu za kuwa Amiri Jeshi Mkuu, ni ushauri wangu wa bure kabisa yeye na wenzake wachunge sana ndimi zao, maslahi ya taifa kwanza vyama baadaye, tunampa nishani iwapo atamaliza siku 75 kwa amani na kumkabidhi Amri Jeshi Mkuu, Edward Lowassa,” alisema Mbatia. “Rafiki yangu (Ibrahimu)Lipumba amekimbia akidhani Ukawa utaparaganyika lakini sasa umeimarika zaidi,” alisema Mbatia huku akishangaliwa na umati wa watu na kumaliza kuwa “Hakuna mwanadamu ambaye yupo juu kuliko wengine au taasisi yoyote.”
Makaidi
Mwenyekiti wa NLD Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alisema kuwa katika umri wake mkubwa alionao hajawahi kuona maandamano ya watu wengi kama waliojitokeza kumsindikiza Lowassa jana.
“Nina miaka 74 lakini sijaona kitu kama cha leo nakaanza kujiuliza hii maana yake nini? Nikachukua mfano kama mimi ni chama tawala na wapinzani ni wengi namna hii ningeanza kufanya nini, ningejiuzulu mara moja,” alisema Makaidi.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Tasilima alisema kuwa walioleta siasa mbaya nchini wanatakiwa kuwajibika kwa kuwa wamesababisha kuwapo kwa uchumi mbaya pia.
“Lowassa akiingia Ikulu ataenda kuondoa uchumi na siasa mbaya,” alisema Tasilima.
Maalimu Seif
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alisema umati mkubwa wa vijana waliojitokeza kumsindikiza Lowassa umedhihirisha kuwa watu walikuwa wamekata tamaa sasa wanataka matumaini mapya.
Hata hivyo, alisema haitoshi kumsindikiza Lowassa kwa idadi kubwa namna hiyo kama hawataenda kupiga kura kwa kuwa maandamano hayawezi kuiondoa CCM madarakani.
“Hatutaishinda CCM kwa maandamano bali kwa kupiga kura, tunza kadi yako zimebaki siku chache,” alisema Hamad.
Onesmo Ole Nangolo
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, alipokewa rasmi na kusema alijiunga CCM mwaka 1977, lakini alichokishuhudia Dodoma kwenye uchaguzi wa mgombea wa Rais kwa tiketi ya chama hicho kimemlazimisha kuhamia Chadema.
“Ile CCM niliyokuwa naifahamu si tuliyokwenda juzi Dodoma, misingi na haki imegeuka, kimekuwa chama cha viongozi wachache kwa maslahi yao binafsi, unyanyasaji umetawala ndani ya CCM, sina moyo wa chuma, sikuridhika na mchakato wa Dodoma,” alisema Nangolo.
Ilivyokuwa
Jiji la Dar es Salaam lilisimama kwa wastani wa saa nane kutokana na msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu.
Makundi ya watu wa kada mbalimbali wakiwamo madereva wa bodaboda, bajaji, magari na watembea kwa miguu walionekana kufunga barabara ya Uhuru kuanzia Buguruni eneo la Rozana zilipo ofisi za CUF na Posta zilipo ofisi za NEC.
Maandamano hayo yalisababisha msongamano wa magari na kusababisha magari ya abiria maarufu kama daladala na magari binafsi kutafuta njia mbadala kufanikisha safari zao.
Idadi ya watu waliojitokeza katika msafara inaweza kufananishwa na ile iliyojitokeza wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama Julai 2013.
Watu wengi walionekana wakitumia simu kupiga picha na kurekodi video za matukio mbalimbali pembeni mwa barabara huku wengine wakiwa juu ya maghorofa wakitazama.
Wapo waliokuwa wakitoka maofisini na kukaa pembezoni mwa barabara kushuhudia tukio hilo huku maelfu wakitembea umbali wa kilometa sita kuufuata msafara huo.
Msafara huo ulitumia saa mbili na nusu kutoka Buguruni hadi ofisi za NEC.
Kabla ya msafara
Wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD walianza kukusanyika tangu saa moja asubuhi katika makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni na viongozi mbalimbali walianza kuingia saa 3:56 asubuhi na kumkuta mwenyeji wao Maalimu Seif.
Wengine
Makundi ya mashabiki waliokuwa wakizunguka wakiimba nyimbo mbalimbali, ukiwamo; ‘kama siyo juhudi zako Kikwete, Lowassa tungempata wapi? Na wengine wakikejeli, “Magufuli toroka uje, Tanzania mpya bila CCM inawezekana, tumechoka kuokota makopo na funguo za Magufuli zipo Ukawa.
Safari ya Biafra
Baada ya kukabidhiwa fomu na Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Deogratius Nsanzugwanko, Lowassa, mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi waandamizi wa Ukawa waliendeleza msafara wa kwenda Makao Makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Licha ya umati uliomsindikiza kutembea kilomita nane ukitoka Buguruni, idadi ya watu ilizidi kuongezeka na kuendeleza maandamano yaliyoanzia makutano ya mtaa wa Ghana na Ohio ilipo NEC kupitia Barabara ya Barack Obama na kuunga hadi Ali Hassan Mwinyi.
Kama ilivyokuwa awali, wafuasi hao waliendelea kuimba bila kuchoka nyimbo mbalimbali za hamasa ili wasichoke na kila eneo walilokuwa wakipita umati mkubwa wa watu waliojipanga katika barabara hizo ulishangilia na hata kuwafanya baadhi ya waliokuwamo kwenye magari kuonyesha alama ya “V” inayoyotumika na Chadema.
Msafara ulizidi kuongezeka urefu baada ya wale waliochelewa kuungana nao na baadaye uliiacha barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kuingia barabara ya Kinondoni ambayo kutokana na wembamba wake iliwalazimu wenye magari waliokuwa safarini kuegesha pembeni kupisha watu waliokuwa wakiandamana.
Katika safari yote hiyo, polisi walikuwa wameegesha magari yao katika kila umbali wa kilomita moja na nusu au zaidi na kufanya umati huo uwashangilie kila unapowapita.
Licha ya kuwa taarifa za awali zilibainisha kuwa maandamano hayo yangeishia Makao Makuu ya Chadema, ilibidi uongozi wa chama hicho ubadilishe utaratibu na kuwapeleka watu wote katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni kwa kuwa eneo la mtaa wa Ufipa lisingetosha.
Walipofika Biafra baada ya kumaliza takribani kilomita saba kutoka NEC, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu aliwasalimia wafuasi hao na kumkaribisha Lowassa awashukuru ambaye alizungumza kwa ufupi akitamka maneno, “hii haijawahi kutokea.”
Lowassa aliwapongeza polisi kwa kufanya kazi kwa weledi na kueleza kuwa busara na amani vilivyotumika katika maandamano hayo vinadhihirisha kuwa Chadema na Ukawa ni vyama vya kushika dola.
Baada ya watu kutawanyika, msafara wa viongozi ulirudi mtaa wa Ufipa kuendeleza hotuba ambako baadhi ya wafuasi walioshtukia kuwa walidanganywa walirudi kwenda kuwasilikiliza viongozi.
No comments:
Post a Comment