Monday, September 2

Msigwa amkalia kooni Waziri Kagasheki



Dodoma. Msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amesema kuna ugawaji holela wa maeneo katika Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Ngorongoro (NCAA) kwa kampuni za kitalii na kudai kwamba Waziri wake, Balozi Khamis Kagasheki anahusika.

Msigwa aliwaambia waandishi wa habari katika ofisi za kambi hiyo mjini Dodoma jana kuwa Balozi Kagasheki amerudia makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake, Ezekiel Maige.

Hata hivyo, Waziri Kagasheki amejibu tuhuma hizo akisema hana mamlaka kisheria ya kugawa vitalu kama inavyodaiwa na kwamba kilichotolewa ni vibali kwa ajili ya kambi za watalii (tented camps).

“Katika Kamati ya Vitalu tulisema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa ugawaji na Maige alipata wakati mgumu lakini huyu aliyemrithi hajabadili kitu,” alisema Msigwa, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema). Mchungaji Msigwa alisema kampuni mbili za Leopard Tours na Masai Sanctuaries zilipewa vitalu vya utalii ndani ya eneo la NCAA kinyume na mpango wa miaka mitano wa ugawaji wa mamlaka.

Kwa kawaida wataalamu wa uhifadhi na uongozi NCAA hukutana kila baada ya miaka mitano ili kugawa vitalu katika eneo la Ngorongoro. Msigwa alisema Waziri Kagasheki alitakiwa kupata ushauri kutoka uongozi wa Ngorongoro kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa vitalu hivyo.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo nyaraka zinazoonyesha kuwa kampuni hizo zilipewa vitalu vya utalii vya Ndutu na Oloololo ambavyo havikuwa katika mpango wa ugawaji kama inavyotakiwa kisheria.”

Alidai kuwa katika moja ya barua ambazo kambi hiyo inazo, Waziri Kagasheki aliiandikia Kampuni ya Leopard Tours akiitaarifu kuwa tayari ameiagiza NCAA ipewe kitalu chenye ukubwa wa hekari tano.

“Alielekeza mamlaka kuipa kampuni hiyo ekari tano kwa Dola za Marekani 30,000 (Sh48 milioni) ambacho ni nusu ya kiwango cha kawaida cha Dola 60,000 (Sh95 milioni) kwa ekari 10,” alisema Msigwa.

Barua hiyo ya Julai 17, 2013 yenye kumbukumbu namba CAB.315/319/01B iliyosainiwa na Balozi Kagasheki inauelekeza uongozi wa NCAA kumpa viwango hivyo.

Waziri Kagasheki alisema alitoa punguzo hilo kwa kampuni hiyo ya Leopard si kwa ajili ya kitalu, bali tozo kwa ajili ya kambi yake ya watalii na kueleza kushangazwa na tuhuma zilizoelekezwa kwake akisema sheria haimruhusu kugawa vitalu hadi awasiliane na kamati husika. Alisema aliwapunguzia ada hiyo Leopard kwa kuwa walipewa mita za mraba 29.7 na kudaiwa Dola 60,000. Alisema wangetakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kama wangepewa mita za mraba 60.

“Niliona hawa jamaa hawajatendewa haki kwani walitozwa ada kubwa kwa ajili ya nusu eneo,” alisema na kumtaka Msigwa kutoa ushahidi wa barua kama amegawa vitalu. Balozi Kagasheki alisema ugawaji wa vitalu utafanyika keshokutwa atakapokutana na kamati husika.

Haya hivyo, Mchungaji Msigwa alisema waziri alifanya uamuzi huo bila kuzingatia sheria na kanuni za ugawaji wa vitalu, pia akivunja sheria kwa kufanya uamuzi moja kwa moja na kampuni hiyo na kushusha viwango vilivyowekwa kisheria bila kutoa tangazo la Serikali.

Mke wa Kagasheki atuhumiwa

Mbali na tuhuma hizo, Mchungaji Msigwa pia amemtuhumu Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige akidai kwamba ametumia ushawishi wa mumewe, Balozi Kagasheki kupewa msaada wa Sh10 milioni na NCCA kupitia taasisi yake ya Catherine Foundation Development Ltd kinyume cha kanuni inayotaka isizidi Sh2 milioni.

“Mradi huu ulipewa fedha hizo huku dokezo la maombi ya msaada huo ukionyesha kuwa watendaji wa NCAA walitoa mapendekezo mara mbili kuwa hakuna bajeti ya kusaidia msaada huo,” alisema.

Msigwa alisema Kaimu Mhifadhi wa NCAA alinukuliwa akisema fungu la msaada halina fedha ya kutosha na kwamba Magige ashauriwe kusubiri mpaka mwaka wa fedha ujao 2013/2014... “Dokezo hili lilisainiwa tarehe 14.12.2012 lakini jambo la kushangaza na la kutia walakini... Mhasibu aliagizwa ilipwe kiasi hicho.”

Alisema pamoja na baadhi ya watendaji kueleza kwamba NCAA haikuwa na fedha, Kaimu Mhifadhi Mkuu alitoa agizo Juni 18,2013 la kutoa kiasi cha Sh10 milioni kwa taasisi hiyo.“Katika hili kuna mgongano mkubwa wa masilahi kwa sababu huwezi kumtenganisha Mheshimiwa Kagasheki na kazi zake za uwaziri na hii ya Catherine Foundation ambaye ni mke wake,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Balozi Kagasheki alikanusha vikali tuhuma hizo na kusema hakuwa na mamlaka ya kuishinikiza NCAA... “Nisingependa kuzungumzia masuala ya mke wangu maana kuna mambo mazito ya nchi ya kuzungumzia. Ila siwezi kushinikiza taasisi iliyo chini yangu itoe Sh10 milioni pengine labda ingekuwa Sh1 milioni.”

Kagasheki alisema hamshangai Mchungaji Msigwa kwani amekuwa na tabia ya kumzushia mambo na kukumbusha alivyoshinikiza ajiuzulu katika kikao kilichopita cha bajeti.

Naye Magige alipoulizwa kuhusu fedha hizo, alikiri taasisi yake kupewa lakini akasema walifuata taratibu zote katika kuomba kama wanavyofanya katika taasisi nyingine.

“Sisi tunaomba misaada katika taasisi mbalimbali na katika hili tulifuata taratibu zote na wakaamua watupe Sh10 milioni. Tungekataa wakati wanafunzi hawana madawati?” alihoji Magige.

Alisema kutolewa kwa fedha hizo kulikuwa hakuna shinikizo lolote kutoka kwa Waziri Kagasheki na kwamba kama ingekuwa hivyo, taasisi hiyo ingepewa fedha nyingi zaidi.

Alieleza kushangazwa na kauli za Msigwa dhidi yake na taasisi yake ambayo alisema imekuwa msaada mkubwa kwa shule za msingi Arusha ambazo zimekuwa na upungufu wa madawati.

No comments:

Post a Comment