Monday, September 2

KINGUNGE AMSHANGAA KAGAME



MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, amejitosa katika mgogoro wa kidiplomasia uliopo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Kingunge alimshangaa Rais Kagame kwa jinsi alivyouchukulia vibaya ushauri wa Rais Jakaya Kikwete, aliompa juu ya waasi wa nchini humo.

Alisema kwamba, kilichotolewa na Rais Kikwete juu ya waasi hao, ulikuwa ni ushauri ambao ulilenga kurejesha amani nchini Rwanda na wala si vinginevyo.

“Kutoelewana baina ya nchi jirani si jambo dogo na jema, hivyo si vizuri hali hiyo ikaachwa iendelee kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhu.

“Nashauri jitihada zote zifanyike ili sintofahamu hii baina yetu na Rwanda ipate suluhu haraka iwezekanavyo, kwa sababu sisi ni majirani.

“Ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rwanda ulikuwa sahihi na nauunga mkono, lakini maadam wenzetu Rwanda hawakuupokea vizuri, jawabu ni kufanya juhudi za kidiplomasia ili mtafaruku huo uishe.

“Hata hivyo, pamoja na mambo mengine, mgogoro huo hauna sababu ya kututoa au kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa sababu nchi zote tano zinahitajiana na tuna wajibu kwa wananchi wetu kushirikiana kwa faida ya nchi zote husika,” alisema Kingunge kwa kifupi.

Akizungumzia vyama vya upinzani nchini, Kingunge alisema safari yao katika kuchukua dola bado ni ndefu kutokana na kutokuwa na mtandao unaofikika nchi nzima.

Alisema vyama vikubwa vya upinzani vikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF), bado viongozi wake wana tabia ya kuhutubia na kuondoka badala ya kujenga chama chenye mtandao.

“Tatizo la vyama vyetu vya upinzani nchini, lilianza tangu mwaka 1992 vilipoanzishwa na tangu wakati huo, havijaweza kujirekebisha, viongozi wake wanafikiria kwenda Ikulu tu na hivyo wanajielekeza kwenye kushinda urais na kusahau nafasi nyingine.

“Lakini, ili kufika Ikulu, lazima uwe na watu wa kukufikisha huko na watu hao ni wanachama kutoka kwenye vijiji, kata, wilaya na taifani. Kama kule kwenye watu hao hawajaweza kujizatiti, suala la kwenda Ikulu litawachukua muda mrefu.

“Ili kuwa na nafasi ya kushinda uchaguzi, chama lazima kiwe kimejikita kwa umma wa wananchi na siyo kuzungukazunguka,” alisema Kingunge.

Alisema mikutano ya hadhara kwa vyama ni sahihi kufanyika na kwamba ndiyo kazi ya vyama vya siasa, kwani chama kinapata nafasi ya kueneza sera na kujipima kisiasa kupitia mikutano hiyo.

Pamoja na hayo, alisema mvuto huo wa kisiasa huwa si wa wakati wote kwani inawezekana chama kina tabia ya kuzungumza juu ya masuala ambayo wananchi wanapenda kuyasikia hata kama hawakubaliani nacho.

“Kupata watu wengi kwenye mkutano haimaanishi kwamba vyama vingine havipendwi au havikubaliki, inawezekana vyama vingine vikawa vinapendwa na kukubalika, lakini havina tabia ya kufanya mikutano.

“Lakini, kwa ujumla wake, ni kwamba vyama vyote hivyo vinaweza kushinda urais kama tu vinashinda kwenye majimbo ya ubunge, ila kwa hali jinsi ilivyo hivi sasa, safari yao bado ni ndefu hawawezi kuchukua nchi,” alisema mwanasiasa huyo.

Sakata la Mansour
Akizungumzia kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Kisiwani Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid, Kingunge alisema mwanasiasa huyo alistahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alistahili adhabu hiyo.

“Chama kina sera ambazo tunazitekeleza na tunaziheshimu, tuna katiba inayotuongoza na kwa mujibu wa katiba yetu, tuna vikao vinavyofuatilia uadilifu wa wanachama wetu.

“Uadilifu huo ni pamoja na kuheshimu Katiba na sera za msingi wa chama na vikao vya mara kwa mara, kwa hiyo, mwanachama anayeonekana kwa kauli na vitendo vyake yuko kinyume na matakwa ya Katiba, Halmashauri Kuu ina madaraka ya kumvua uanachama, uongozi au kumpa adhabu nyingine.

“Kwa hiyo, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ilikuwa sahihi, hivi ni nani asiyemfahamu Mansour kwamba ni CUF? Hili suala liko wazi familia yao nzima ni wanachama wa CUF, kwa hiyo si ajabu kwake.

“Mimi nastaajabu kwa sababu, kwanza baba yake alikuwa miongoni mwa watu 14 waliotekeleza Mapinduzi ya Zanzibar na hakuwa mkorofi, sijui imekuwaje Mansour naye akabadilika maana ninavyomfahamu hakuwa hivi,” alisema Kingunge.

Agosti 26, mwaka huu, kikao cha NEC, kilimvua uanachama Mansour kwa kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.

No comments:

Post a Comment