Saturday, April 7

Ujerumani inahitaji mashujaa kama Martin Luther King Jr.

Mbali na mashujaa kwenye ulingo wa michezo, Ujerumani ina mashujaa wachache sana nje ya ulingo huo.

USA Martin Luther King, Jr. National Memorial in Washington (picture-alliance/newscom/L. Vogel)
Huu ni wakati mwafaka wa kutafakari kuhusu dhana ya kukataa tamaduni zinazopendwa, taasisi ama misingi iliyowekwa, anaandika mhariri mkuu wa shirika la utangazaji  Deutche Welle, Ines Pohl.
"Sina furaha katika nchi inayohitaji mashujaa," mwandishi wa Ujerumani wa tamthilia, Bertolt Brecht anaandika kwenye mchezo wake "Maisha ya Galileo," mwisho wa Vita Vikuu vya Pili. Kwa nukuu hiyo, Brecht, mwenyewe alilengwa na Wanazi, alikataa na kupinga tabia ya kuabudu mashujaa katika jamii iliyotawaliwa  kiimla.
Aliamini kwa moyo wake wote kuwa jamii zinazoendeshwa na mfumo wa demokrasia hazihitaji mashujaa kuyatafutia ufumbuzi  matatizo yao. Kinyume chake, wajibu wa watu binafsi hushabikiwa na kukwezwa, na matokeo ya tabia ya kuabudu mashujaa ni utiifu wa kijinga ambao huchangia mmoja kuwa mnyonge.
King anakumbukwa 
Bg 50. Todestag von Dr. Martin Luther King Jr. (Flip Schulke. Photo courtesy of UT Austin's Briscoe Center for American History)
Mkewe King Coretta Scott na familia wakimuomboleza, 1968
Martin Luther King Jr. aliuawa miaka 50 iliyopita siku ya Jumatano. Mhubiri huyo hakukata matumani kwenye vita dhidi ya ukosefu wa haki, vita vya Vietnam na kudhulumiwa kwa Waamerika weusi. Yeye na wafuasi wake walijitolea bila ya kutumia nguvu wala ghasia, licha ya kukabiliwa na machafuko  dhidi yao. Hata leo, angali anawatia ujasiri watu ambao wanahisi kutoridhika na uongozi uliopo na wanaoamini kuwa  maisha tofauti yanawezekana.
Hivi karibuni  mji wa Washington, DC, Marekani, maelfu ya watu waliandamana wakipinga ushawishi wa makundi yanayojihusisha na matumizi ya bunduki kwa siasa za Marekani.  Maandamano makuu, yalipangwa na kuongozwa na wanafunzi wa shule ya Parkland, Florida, baada ya wanafunzi wenzao 14 na wafanyikazi watatu wa shule ya upili ya Stoneman Douglas, kuuawa mwezi Februari. Kwenye mhadhara wa kitaifa ulioandaliwa katika mji mkuu, Yolanda Renee King, mwenye umri wa miaka tisa, aliongeza uzito hotuba ya babu yake, "Nina Ndoto" na urithi wa vuguvugu la makundi ya kupigania haki za binadamu ni bayana katika maneno na vitendo vya Emma Gonzalez, mwenye umri wa miaka 18, mmoja wa waandalizi wa mkusanyiko uliopewa jina, " Msafara kwa ajili ya  maisha yetu."
Sio suala la utiifu kuwa na mashujaa kama vile King na watu kama yeye. Watu kama hao wanatupa nguvu na ujasiri. Wanasaidia makundi ya vuguvugu kukua na makundi hayo yana nguvu zaidi kuliko watu binafsi.
Chimbuko la matumaini
Ines Pohl Kommentarbild App (DW/P. Böll)
Ines Pohl Mhariri mkuu wa Deutche Welle
Mashajaa kama vile King wanatupa matumaini. Wanatuonyesha kuwa kuna thamani ya kusimama na kuyaacha mazingira tunayopenda, kubainisha ujasiri na kuonyesha umoja; kujenga mitandao na kutovunjika mioyo; na kutikisa watu kutoka kwenye nafasi na hadhi zao kuu na kuwaita kushiriki.
Ni nguvu hizi ambazo Ujerumani na mataifa mengine yanahitaji kuukabili ulimwengu ambao hueleweki na kutovunjika moyo ndani ya mizozo ambayo yaelekea haina ufumbuzi. Hatimaye, ni muhimu kudumisha imani na uwezekano wa taifa linaloendeshwa kwa misingi ya demokrasia ambalo linaruhusu uhuru wa wananchi.  Ulimwengu unamkumbuka Martin Luther King leo — sio tu kwasababu ya yale aliyoyafanikisha wakati wa uhai wake , lakini pia kwasababu ya jinsi anavyozidi kuhitajika.

Mzozo wa Sahara Magharibi wafukuta

Morocco ameonya kuchukua hatua ikiwemo ya kijeshi kama Umoja Mataifa hautachukua hatua dhidi ya ujenzi na mpango wa chama cha Polisario kuanzisha vituo vya kijeshi katika ukanda usio wa kijeshi katika Sahara Magharibi.

Westsahara Konflikt Flüchtlinge im Smara Flüchtlingscamp (Getty Images/AFP/D. Faget)
Wimbi la kumbukumbu ya wakimbizi la mzozo wa muda mrefu wa Sahara Magharibi
Waziri wa mambo ya nje wa Morocco Nasser Bourita ameonya kwamba nchi yake inazingatia kuchukua hatua zote ikiwemo ya kijeshi kama Umoja Mataifa hautachukua hatua dhidi ya ujenzi na mpango wa chama cha Polisario kuanzisha vituo vya kijeshi katika ukanda usio wa vita unaosimamiwa na Umoja wa mataifa katika eneo la Sahara Magharibi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Waziri Bourita amesema kwamba makubaliano ya kusitisha vita ya mwaka 1991 yanatishiwa na vitendo vya hivi karibuni vya chama cha Polisario ambacho kinatafuta uhuru wa eneo la Sahara Magharibi lenye utajiri mkubwa wa madini. Nikimnukuu hapa anasema" Morocco inasema wazi kabisa hatua zote zinazingatiwa, Morocco haiwezi kuruhusu mabadiliko kwa makubaliano yaliyopo. Kama Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Kimataifa haziwajibiki, Morocco itachukua majukumu yake."
Kukanisha kwa tuhuma za Morocco
Westsahara Konflikt UNO (Getty Images/AFP/F. Batiche)
Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Sahara ya Magharibi
Mapema wiki hii mwakilishi wa Chama cha Polisario katika Umoja wa Mataifa, Ahmed Boukhari alizikanusha tuhuma Morocco kwa kuzieleza kuwa zisizo na msingi na za uongo. Baadae Jumatatu aliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika barua yake kwa kusema jeshi la ulinzi wa amani la Umoja wa Mataifa  katika eneo la Sahara Magharibi halijaripoti taarifa yoyote ya kisa cha kukiukwa kwa makubaliano ya kuweka chini silaha, kilichofanywa na kundi hilo lenye kufanya harakati za kutaka kujitenga.
Boukhari ameituhumu Morocco kwa kutaka kubadili hali ya sasa ilivyo kwa kujenga barabara katika eneo la ukanda salama wa eneo la Guergert. Vilevile amesema tuhuma hizi za sasa za Morocco zina lengo la kuliondosha baraza la usalama katika zingatio la masuala yake yanayosababisha mkwamo kwa kipindi hiki katika eneo la Sahara Magharibi. Jana Jumatano Shirika la habari la Algeria APS lilichapisha taarifa ya Kundi la Polisario ikisema Boukhari amefariki dunia Jumanne nchini Uhispania akiwa na umri wa miaka 64 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Morocco ilichukua udhibiti wa jimbo hilo la Sahara Magharibi mwaka 1975 baada ya mtawala wa kikoloni Kihispania kujiondoa , na kusababisha mapigano ya chini kwa chini kwa ajili ya uhuru wa jimbo hilo ambayo yalimalizika mwaka 1991 wakati umoja wa mataifa ulipoweza kupatanisha na kupeleka jeshi la kulinda amani katika jimbo hilo. Hatua hiyo pia ilikwenda sambamba na kufanyika kwa kura ya maoni kwa ajili ya kuamua hatma ya baadae ya eneo hilo. Hata hivyo kura hiyo haijapigwa mpaka wakati huu.
Morocco inalichukulia eneo la Sahara Magharibi lenye utajiri mkubwa wa madini kama "jimbo lake la kusini" na imependekeza kulipa eneo hilo nguvu kubwa ya kujitawala. Lakini Chama cha Polisario kimeendelea kushinikiza kujitegemea kwa kutumia kura ya maoni kwa watu wa eneo hilo ambao wanakadiriwa kuwa kati ya 350,000 na 500,000. Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Morocco Nasser Bourita anasema amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hapo jana na amemkabidhi barua kutoka kwa Mfalme Mohammed wa Sita ambae pia alizungumza na mkuu huyo wa umoja wa mataifa. Anasema mfalme nae amesitizita kutatuliwa haraka mzozo uliopo tofauti na hapo Morocco itachukua hatua.

Ni miaka 50 tangu kifo cha Martin Luther King Jr

Je, ndoto ya kiongozi huyo wa harakati za haki za kiraia Martin Luther King Jr, ya kuwepo usawa Marekani imetimika au imegeuka kuwa jinamizi?

USA Martin Luther King Jr. - Rede I have a dream, 1963 (picture-alliance/AP Photo)
Mnamo tarehe 4, mwezi Aprili mwaka 1968, vuguvugu la kupigania haki za kiraia nchini Marekani lilimpoteza kiongozi wao mkuu. Martin Luther King Jr aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa amesimama katika kibaraza cha hoteli moja mjini Memphis. 
Martin Luther King Jr, kiongozi wa vuguvugu la amani la kupigania haki hasa za Wamarekani weusi aliuawa akiwa na umri wa miaka 39, hakuishi kuona kama ndoto yake ya kuwepo usawa Marekani ingefikiwa au la.
Licha ya kuongezeka kwa uhuru wa watu weusi nchini Marekani katika kipindi cha miaka 50 tangu kifo cha King Jr, watu wengi weusi nchini humo bado wanakabiliwa na changamoto chungu nzima katika karibu kila nyanja.
Je, ndoto ya usawa imetimia?
Kutokuwa na usawa wa kiuchumi, kubaguliwa,kukamatwa na kufungwa jela kwa Wamarekani weusi  na polisi kuwaua kiholela watu weusi yanajitokeza kama mambo matatu makuu ya mifano ya changamoto nyingi zinazoonesha bado watu weusi hawajapata hadhi ya kujihisi sawa na wazungu,kuthaminiwa na kufanikiwa maishani.
USA Memphis Martin Luther King 1968 (picture-alliance/AP Photo/J. Thornell)
Martin Luther King Jr(katikati) wakati wa maandamano mjini Memphis
Katika jela za Marekani, kuna takriban wafungwa milioni 2.3 ambao ni watu weusi, hiyo ni asilimia 34 ya wafungwa wote nchini humo. Rekodi za kihalifu zinawafanya vijana kupata ugumu wa kupata kazi, kuwa na matatizo ya kisaikolojia na kuziathiri familia nyingi kwa kila nyanja. Uwezekano wa wanaume weusi kuuawa na polisi ni mara tatu kuliko wanaume wazungu.
Na hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa Marekani inaoongozwa na Rais ambaye anaonekana kuwa na ubaguzi wa rangi, wengi wanahofu kuwa juhudi zilizopigwa na Martin Luther King Jr na wanaharakati wengine wa kutetea usawa na haki za kiraia huenda zikahujumiwa.
Mkurugenzi wa kituo cha Ronald W. Walters kinachotoa mafunzo ya uongozi na sera za umma katika chuo kikuu cha Howard mjini Washington DC Elsie Scott anasema anatiwa wasiwasi na hali ilivyo hivi sasa Marekani.
Scott anasema hakuna matumaini makubwa nchini humo wakati taifa linapokumbuka miaka 50 tangu kuuawa kwa King Jr akiongeza kuwa anadhani watu wengi weusi wanatiwa wasiwasi na msimamo wa utawala wa Rais Donald Trump.
Licha ya kuwa kiwango cha elimu na kupenya kwa watu weusi katika tabaka la wastani na la juu kimeongezeka tangu miaka ya sitini lakini idadi ya wanaosalia katika umasikini na kutopata elimu ya kutosha inasalia kuwa juu mno.
Wamarekani weusi bado wanahisi kubaguliwa
Margaret Simms, mtafiti katika taasisi ya Urban mjini Washington D.C anasema asilimia ya watu weusi wanaopata kipato cha wastani inasalia kuwa kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita. Simms anasema viwnago vya umasikini hivi sasa vinawaathiri Wamarekani weusi mara tatu kuliko inavyowaathiri wazungu.
USA Protest der Black lives matter - Bewegung in Memphis, Tennessee (picture-alliance/dpa/M. Brown)
Nembo ya vuguvugu la kutetea haki za watu weusi Marekani
Kunasalia kuwa na pengo kubwa la upatikanaji wa ajira kati ya watu weusi na wazungu nchini Marekani.
Ibrahim Kendi mkurugenzi wa kituo cha kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi katika chuo  kikuu cha Washington anasema  wakati King alipokuwa hai, wamarekani weusi walikuwa na uwetzekano wa mara mbili kutopata ajira ikilinganishwa na wazungu na sasa miaka 50 baada ya kifo chake bado hali ni hiyo hivyo kuashiria bado kubaguliwa kwa misingi ya rangi ya ngozi upo.
Wanaharakati wa kutetea usawa Marekani wanasema bila ya kuwepo fursa sawa za kiuchumi, Wamarekani weusi wamshindwa kujitengeza mali na hivyo kuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa maishani na kuwaachia vizazi vyao mali.
Mbali na hayo, katika mitaa wanayoishi Watu weusi, shule ni za viwango vya chini na hivyo watoto wa Wamarekani weusi wanashindwa kuvunja mkondo wa kutokuwepo elimu ya kiwango bora. Wachambuzi wanasema hadi pale hatua madhubuti zitakapochukuliwa kuvunja mkondo huo wa umasikini na ubaguzi wa Wamarekani weusi, hali hiyo itaendelea kwa miaka mingine 50 ijayo.

Puigdemont aitaka serikali Uhispania kuheshimu demokrasia

Kiongozi wa zamani wa jimbo la Katalonia Carles Puigdemont ametoa wito mpya kwa serikali kuu ya Uhispani kuanzisha majadiliano juu ya madai ya Catalonia kutaka kujitenga, baada ya kuachiliwa kutoka jela Ujerumani.

Deutschland Puigdemont - Berlin (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)
Rais wa zamani wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont akizongwa na mashabiki wake mjini Berlin kabla ya kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari, Aprili 7, 2018.
Puigdemont amewaambia waandishi habari wa Ujerumani kwamba anatarajia uamuzi wa mahakama ya Ujerumani wa kutomrejesha Uhispania kwa madai ya uasi unaonyesha kwamba majadiliano yanahitajika kuuzima mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini mwake.
Kiongozi huyo wa zamani wa Catalonia aliwekwa kizuizini kwa waranti wa Umoja wa Ulaya uliotolewa na serikali ya Uhispania baada ya kuingia nchini Ujerumani Machi 25. Mahakama ya jimbo la Schleswig-Holstein imeamua mashtaka ya uasi hayaruhusu kutolewa uamuzi wa mshtakiwa kurejeshwa nyumbani alipotokea.
Puigdemont alisema Uhispania inapaswa kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa kwa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, akimaanisha wanasiasa kadhaa wa Catalonia wanaotaka kujitenga, waliofungwa baada ya tangazo la upande mmoja la uhuru wa Catalonia kutoka Uhispania mwaka uliopita.
Deutschland Puigdemont - Berlin (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)
Wafuasi wa Puigedemont walimpokea kwa shangwe na vifijo kutoka jela alikokuwa anazuwia nchini Ujerumani baada ya kukamatwa.
Alisema anatumaini kurejea kuishi nchini Ubelgiji baada ya mchakato wa Ujerumani kumalizika lakini alidhamiria kubakia mjini Berlin wakati mchakato huo ukiendelea. Aliongeza kuwa atakapowasili Ubelgiji, ataendelea na shughuli zake za anazozifanya uhamishoni.
Utata wa kurejeshwa Uhispania
Maafisa nchini Ujerumani bado wanazingatia iwapo kumrejesha Puigdemont nchini Uhispania baada ya kukamatwa Machi 25 kwa waranti uliotolewa na Madrid, wakati akisafiri kupitia Ujerumani.
Serikali ya Uhispania inamtuhumu kwa "uasi" na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuandaa kura haramu ya maoni kuhusu uhuru wa Catalonia mwezi Oktoba.
Siku ya Alhamisi, mahakama nchini Ujerumani iliamua kuwa hangeweza kurejeshwa kwa misingi ya uasi, kwa sababu kosa na hilo chini ya sheria ya Ujerumani, la uhaini, linahitaji mshtakiwa awe amefanya vurugu.
Puigdemont hata hivyo anaweza kurejeshwa Uhispania kukipatikana ushahidi wa madai ya kutumia vibaya fedha za umma kwa kufanya uchaguzi wa maoni wa mwaka jana uliopigwa marufuku na mahakama ya katiba ya Uhispania.
Deutschland PK Puigdemont will in Deutschland Justiz-Entscheid abwarten (picture-alliance/AA/C. Karadag)
Puigdemont akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Jumamosi Aprili 7, 2018 baada ya kuachiwa kutoka jela siku ya Ijumaa.
Uhispania yakataa rufaa
Waziri wa sheria wa Ujerumani Katarina Barley amesifu uamuzi huo wa mahakama, akiliambia gazeti la kila siku la Sueddeutsche Zeitung siku ya Jumamosi, kwamba uamuzi wa majaji ulikuwa "sahihi kabisa." Matamshi yake yalikosolewa mara moja kama ya "kusikitisha" na waziri wa mambo ya nje wa Uhispania, Alfonso Dastis.
"Tunahisi matamshi kuhusu uamuzi wa majaji kwa wakati huu siyo sahihi," aliwaambia waandishi wa habari katika mji wa kusini mwa Uhispania wa Seville.
Mahakama ya juu kabisa ya Uhispania inazingatia kukataa rufaa katika mahakama ya sheria ya Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg kuhusu taratibu za kukabidhiana watuhumiwa miongoni mwa mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Maandamano yalikuwa yamepangwa katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Neumuenster, ambako Puigdemont alishikiliwa tangu kukamatwa kwake, kupinga uwezekano unaondelea kuzingatiwa wa kumkabidhi kwa Uhispania.

Ujerumani yamuachia huru Puigdemont

Mahakama moja ya Ujerumani imekubali kumuachia huru aliyekuwa kiongozi wa jimbo la Catolonia Carles Puigdemont kwa makosa ya uasi ya kufanya kampeni za kutaka uhuru wa jimbo hilo.

Deutschland Neumünster Freilassung Carles Puigdemont (Reuters/F. Bimmer)
 Mahakama hiyo imesema kuwa Puigdemont anaweza kurejeshwa Uhispania na kushtakiwa kwa makosa madogo ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kiongozi huyo wa zamani wa jimbo la Catolonia alikamatwa mwezi uliopita baada ya Uhispania kutoa waranti wa kukamatwa kwake alipoingia Ujerumani.
Puigdemont apatiwa dhamana na mahakama
Deutschland Neumünster Freilassung Carles Puigdemont (picture-alliance/dpa/A. Heimken)
Carles Puigdemont akizungumza na wanahabari
Uamuzi huo unamaanisha kuwa Puigdemont, aliyetoroka Uhispania miezi miwili iliyopita na kuelekea Ubelgiji baada ya waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy kupuuzilia mbali utawala wake wa jimbo, hawezi kuhukumiwa kwa uasi nchini Uhispania atakaporejeshwa kwa mujibu wa msemaji wa mahakama ya Ujerumani. Puidgemont amezungumza na wanahabari baada ya kupatiwa dhamana.
"Nataka wenzangu watatu ambao wamefungwa katika gereza la Uhispania wachiwe huru. Ni aibu kwa Ulaya kuwa na wafungwa wa kisiasa. Demokrasia ya aina hiyo ni hatari sana nchini Uhispania."
Msemaji huyo, Frauke Holmer amesema kuwa mahakama sasa lazima iamue kama atarejeshwa uhispania na kushtakiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Shirika la habari la Reuters lilipouliza mahakama ya Juu na Serikali ya Uhispania iwapo ni sawa kusema kuwa Puigdemont sasa atashtakiwa kwa makosa ya uasi, halikupata jibu.
Uhispania inaheshimu uamuzi wa Ujerumani
Spanien | Regierungssprecher Inigo Mendez de Vigo (picture-alliance/dpa/epa/Ballesteros)
Inigo Mendez de Vigo, msemaji wa serikali ya Uhispania
Mahakama ya Ujerumani ilisema kuwa makosa ya uasi ambayo Puigdemont anakabiliwa nayo sio makosa ya uhalifu nchini Ujerumani, lakini hakuna ushahidi wa kutosha kuhusu suala la machafuko ambalo limehusishwa naye.
Makosa ya uasi yana kifungo cha hadi miaka 25 nchini Uhispania. Mahakama ya Ujerumani imemtoza dhamana ya euro elfu 75 sawa na dola elfu 92
Wakili Wolfang Schomburg ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa Puidgemont anajiandaa kuhamisha fedha hizo za dhamana.
Huku hayo yakiarifiwa jaji mmoja nchini Ubelgiji amewapa dhamana waliokuwa mawaziri watatu wa jimbo la Catolonia ambao Uhispania inawataka kurejeshwa nchini humo kuhusu suala tata la uhuru wa jimbo hilo kwa mujibu wa mwendesha mashtaka.
Msemaji wa serikali ya Uhispania Inigo Mendez De Vigo amesema, "Serikali inaheshimu na kuzingatia maamuzi ya mahakama, haijawahi kukiuka athari za maamuzi yake. Puidegemont yuko chini ya mamlaka ya Ujerumani ambayo imebainisha kuwa hajadhulumiwa  kwasababu ya imani yake kisiasa lakini kwasababu ya kutoroka makosa ya uhalifu yanayomkabili."
Watatu hao waliokuwa mawaziri chini ya kiongozi aliyeondolewa madarakani Carles Puigdemont, walijisalimisha katika kituo cha polisi cha Ubelgiji kujibu waranti wa kukamatwa kwao iliyotolewa mwezi uliopita na Uhispania.
Puidgedemont na mawaziri wake wanne walitorokea Ubelgiji mmezi Oktoba mwaka uliopita kuepuka kushtakiwa kwa makosa ya uasi walipokuwa wakitaka jimbo la Catolonia kujitenga na Uhispania.

Zuma awa ngangari mbele ya mashtaka ya rushwa

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma alifikishwa kizimbani katika mahakama iliyofurika Ijumaa kukabili mashtaka ya rushwa na aliibuka mkaidi, akiyataja mashtaka hayo kuwa yaliochochewa kisiasa.

Jacob Zuma Durban Südafrika (picture-alliance/AP/T Hadebe)
Zuma mwenye umri wa miaka 75, alionekana mtulivu wakati wa usikilizaji wa kwanza wa kesi hiyo uliodumu kwa dakika 15 tu, ambapo kesi hiyo iliahirishwa hafi Juni 8.
Jaji Themba Sishi ameahirisha kesi hiyo, baada ya kuwasilikiza mawakili wa pande zote waliothibitisha kuwa Zuma atakata rufaa kupinga uamuzi wa kumshitaki. Polisi iliimarisha usalama nje ya jengo la mahakama, lakini tukio hilo limepita kwa amani.
Wakati mapambano ya muda mrefu yanatarajiwa, tukio la Zuma kusimama mbele ya majaji chini ya miezi mwili baada ya kujiuzulu wadhifa wake, lilikuwa ushindi kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati waliopigana kwa miaka kadhaa kumuwajibisha.
Mashtaka yanayomkabili Zuma
Mashitaka 16 ya hongo, udanganyifu na utakatishaji fedha yalirejeshwa hivi karibuni baada ya kutupiliwa mbali karibu muongo mmoja uliopita. Yanahusiana na mkataba wa silaha katika miaka ya 1990, wakati Zuma alipokuwa naibu rais.
Südafrika | Präsident Zuma tritt zurück ARCHIV (Reuters/R. Ward)
Wafuasi wa Zuma wanaamini kiongozi wao anaandamwa tu na hana hatia.
Zuma anashtumiwa kwa kuchukuwa hongo kutoka kampuni ya Ufaransa inayotengeneza silaha ya Thales, katika mkataba wa mamilioni ya dola, wakati alipokuwa waziri wa uchumi na wakati huo makamu wa rais wa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC.
Kampuni ya Thales, ambayo iliiuzia Afrika Kusini meli za kivita kama sehemu ya mkataba huo, pia inakabiliwa na mashtaka ya rushwa na mwakilishi wa kampuni hiyo alihudhuria mahakamani pamoja na Zuma.
Zuma anadaiwa kuchukuwa kinyume na sheria jumla ya Randi milioni 4.7, sawa na Euro 280,000 kwa kiwango cha sasa cha ubadilishaji fedha -- kutoka malipo 783 yaliyoshughulikiwa na Schabir Shaik, mfanyabiashara aliyekuwa mshauri wake wa kibiashara. Shaik alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani mwaka 2005 kwa tuhuma sawa na hizo, lakini uchunguzi uliookolewa sana mwaka 2016, ulimuondolea lawama Zuma.
Zuma ambaye aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya kuondolewa mashtaka, anakanusha kutenda kosa lolote, na anadai kuwa tume ya uchunguzi ilithibitisha kuwa hakuna ushahidi wowote kwamba fedha zilizopokelewa na yeyote miongoni mwa washauri zililipwa kwa afisa yeyote.
Adai kuandamwa kisiasa
Nje ya jengo la mahakama, Zuma aliimba na kucheza jukwani mbele ya kundi kubwa la wafuasi wake, wengi wao wakiwa wamevalia nguo za rangi za chama cha ANC. Aliwambia wafuasi kuwa yeye ni mhanga wa visasi vya kisiasa.
Aliongeza kuwa amekuwa akipigania haki za za kiuchumi za raia weusi wa Afrika Kusini walio wengi tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi wa weupe wachache mwaka 1994.
Ujumbe huo unavuma miongoni mwa watu wengi wanaochukia ukweli kwambasehemu kubwa ya uchumi inaendelea kuwa mikononi mwa wazungu wachache licha ya kuja kwa demokrasia.
Südafrika - neuer Präsident Cyril Ramaphosa (picture-alliance/AP Photo)
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameapa kupambana na rushwa aliokiri kuwa tatizo kubwa kwa taifa hilo.
"Mtu anapotuhumiwa kwa uhalifu, hilo halimaanishi kwamba wamekutwa na hatia. Mtu huyo bado ana haki kama mtu mwingine yeyote," alismea Zuma.
ANC yamtupa mkono
Mwezi uliopita mwendesha mashtaka mkuu wa Afrika Kusini Shaum Abrahams -- aliyepachikwa jina la utani la "Shaun Kondo" -- kutokana na utiifu wake kwa Zuma wakati wa urais wake -- aliagiza Zuma ashitakiwe kwa udanganyifu, rushwa na utakatishaji fedha.
Chama cha ANC kilimlaazimisha Zuma kuachia madaraka mwezi Februari, kutokana kwa sehemu kubwa na changamoto za kisheria zilizokuwa zikiongezeka dhidi yake pamoja na kashfa kadhaa za rushwa, na chama hicho kimejitenga na kiongozi wake huyo wa zamani.
Mrithi wa Zuma Cyril Ramaphosa ameapa kupambana dhidi ya rushwa serikalini, ambayo alikiri kuwa ni tatizo kubwa.

Gari lagonga watu Ujerumani, watatu wauawa, 20 wajeruhiwa

Watu wasiopungua wanne wameuawa baada ya basi dogo kuparamia kundi la watu katikakati mwa mji wa Muenster nchini Ujerumani Jumamosi mchana. Habari zinasema dereva wa gari hilo ni Mjerumani mwenye matatizo ya akili.

Deutschland Kleintransporter fährt in Münster in Menschenmenge - Tote und Verletzte (Reuters/NonstopNews)
Polisi wakifanya ukaguzi katika eneo ambako gari limegonga watu na kusababisha vifo vya wanne na 20 kujerihiwa.
Waliokufa wanahusisha dereva mshukiwa, aliejiuwa kwa kujipiga risasi akiwa ndani ya gari hilo kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la polisi.
Lakini gazeti maarufu la Sueddeutsche Zeitung limeripoti kuwa maafisa wanaamini hakukuwa na lengo la ugaidi katika tukio hilo, na kwamba dereva huyo anaaminika kuwa Mjerumani mwenye umri wa kati aliekuwa na matatizo ya kisaikolojia.
Gazeti la Sueddeutsche pia limeripoti kuwa nyumba ya mshukiwa ilikuwa ikakaguliwa kutafuta uwezekano wa kuwepo na viripuzi. maafisa wa serikali ya Ujerumani walikuwa bado hawajasema ni nini wanadhani lilikuwa lengo la tukio hilo.
Na wakati huo huo, polisi walisema walikuwa wanahakiki ripoti za mashuhuda kwamba wahalifu wengine huenda wamekimbia kutoka kwenye gari hilo.
Msemaji wa Polisi Andreas Bode anasema mashuhuda waliwambia kuwa watu wengine waliondoka kwenye gari baada ya kugonga. Shirika la habari la Ujeurmani DPA, liliripoti kwamba mashuhuda walizungumzia juu ya watu wawili waliokuwemo ndani ya basi hilo mbali na dereva.
Deutschland Kleintransporter fährt in Münster in Menschenmenge - Tote und Verletzte (Reuters/NonstopNews)
Polisi wakizuwia mtaa ulio karibu na eneo la tukio.
Bode alisema polisi ilikuwa imegundua kifaa cha kutia mashaka ndani ya gari hilo na walikuwa wanakichunguza. Meya wa Muenster alisema maafisa walikuwa bado hawajabaini lengo la tukio hilo. Meya huyo Markus Lewe aliwaambia waandishi habari kwamba Muenster nzima ilikuwa inawomboleza tukio hilo baya.
Maandamano ya Wakurdi
Tayari askari polisi wengi walikuwa katika eneo hilo waklifanya doria wakati wa maandamano ya Wakurdi, na tukio hilo lilitukia muda sawa wa maandamano hayo wa saa tisa na nusu za alasiri.
Wafanyakazi wa mgahawa ulio karibu na baa ambako shambulio hilo lilitokea walielezea kusikia sauti kubwa kabla ya mambo kuanza kwenda haraka na walilaazimika kuondoka mgahawani hapo. Hawakuona tukio halisi litikokea.
Serikali ya Ujerumani imetoa salamu za rambirambi kwa wahanga. "Habari mbaya za Muenster," aliandika msemaji Ulrike Demmer kwenye ukurasa wa twitter.
Waziri wa sheria Katarina Barley alizishuru taasisi za huduma za dharura na kusema kwamba kila kitu kinapaswa kufanyw aili kubaini kilichopelekea tukio hilo. Muenster ni mmoja ya miji muhimu ya vyuo vikuu nchini Ujerumani, ukijivunia zaidi ya wanafunzi 50,000.

Baba Mzazi: 'Abdul Nondo babu yake ni muasisi wa TANU'

Julius Nyerere Rais wa zamani wa Tanzania na muasisi wa chama cha TANU ambacho hivi leo ni CCM akichangaya mchanga wa Zanzibar na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Abdul Nondo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye anakabiliwa na kesi ya kujiteka mwenyewe, mzazi wake Omar amethibitisha kuwa baba yake alizaliwa mwaka 1919 huko Ujiji, Kigoma na kuwa ni miongoni mwa waasisi wa chama cha Tanu.
Mzee Omar, alisema baba yake huyo aliyemtaja kwa jina la Omar Kagobe alipata watoto 30, mmoja akiwa yeye.
“Nashangaa hao wanaomkamata na kumhoji mtoto wangu kuwa sio raia, wananichekesha sana kwa kuwa najua mwisho wa siku watajua ukweli wake. Ukweli ni kwamba wazazi wangu ndio waasisi wa Tanu na walishiriki kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi hii, hivyo suala hilo halinipi wasiwasi wala hofu na hivyo vyeti wanavyovitaka mbona vipo tu, ila waelewe kuwa sisi ni Wamanyema halisi na ni raia halali wa nchi hii,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Mkoa wa Kigoma, Sendwe Mbaruku, alitoa taarifa Alhamisi kuhusu suala la Nondo kuhojiwa na uhamiaji na kusema; “Kijana Abdul ni mtoto wetu hapa Kigoma, wazazi wake ni wakazi na wapiga kura wa hapa Ujiji, zaidi ni Watanzania wenzetu.”
Maelezo haya yametolewa na mzazi huyo Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uraia wake, vimesema vyanzo vya habari nchini Tanzania.
Mzazi huyo amesema babu yake Nondo, alishawahi kuwa Polisi kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1940 hadi 1958 na alishafanya kazi huko Mabatini mkoani Mwanza na sehemu nyingine za nchi.
Alisema babu yake wakati akiwa polisi, ndipo zilipoanzishwa Kota za Msimbazi, Dar es Salaam na jina lake lilikuwa maarufu, akijulikana kama Mzee Kagobe.
Kama haitoshi alisema bibi yake Nondo alikwenda kuhiji, mnamo 1970 na alipewa hati ya kusafiria ya Tanzania, huku akihoji, “Kama angekuwa sio raia wa Tanzania angepewaje hati hiyo?”
Baada ya Nondo kuripoti polisi mjini Mafinga alishikiliwa na jeshi hilo Mkoa wa Iringa na baadaye kukabidhiwa kwa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema kupitia uchunguzi wa kisayansi, wamebaini kuwa hakuwa ametekwa, bali alijiteka na tayari suala lake lipo mahakamani, Iringa.

White House yatangaza vikwazo dhidi ya Warusi 38, makampuni ya Russia

Wafanyabiashara mashuhuri nchini Rashia na maafisa wa nchi hiyo waliowekewa vikwazo na Serikali ya Marekani kama walivyo orodheshwa na Wizara ya Fedha ya Marekani, Washington Aprili 6, 2018. (Juu kushoto, kutoka kushoto) Oleg Deripaska, Vladimir Bogdanov, Suleiman Kerimov, Kirill Shamalov, Viktor Vekselberg, (Kati Kutoka kushoto) Mikhail Fradkov, Sergei Fursenko, Alexei Dyumin, Vladimir Kolokoltsev, Konstantin Kosachev, (Chini, Kutoka Kushoto) Andrei Kostin, Alexei Miller, Nikolai Patrushev, Vladimir Ustinov, Viktor Zolotov.
White House imetangaza vikwazo dhidi ya Warusi 38 na makampuni, ikisema Marekani inakabiliana na kile kinachoendelea ikiwa ni mbinu za Serikali ya Russia za “vitendo vya kuvuruga” demokrasia nchi za Magharibi na ulimwenguni kote.
Katika muhtasari alioutoa msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders Ijumaa amesema Marekani bado inataka kushirikiana na Russia.
“Pia, kile tunachotaka kukiona ni serikali ya Russia ibadilishe mwenendo wake kikamilifu. Tunataka kuendelea kuwa na mazungumzo na kufanya kazi siku za usoni kwa kujenga mahusiano mazuri,” Sanders amesema.
Vikwazo hivyo vitawekwa dhidi ya makampuni saba ya Russia – ikiwemo Oleg Deripaska, kampuni ya aluminium ambayo ni mshirika wa karibu na Rais Vladimir Putin- na makampuni mengine 12 ambayo wanayamiliki au kuyahodhi.
Pia maafisa 17 wa serikali ya Russia, na kampuni ya kutengeneza silaha inayomilikiwa na serikali ya Russia na kampuni zake tanzu, benki ya Russia, pia zitalengwa na vikwazo hivyo.

Unesco, Rwanda zajadili vituo vipya vya Urithi wa Dunia

Watu wakijitolea kuzika mabaki ya wahanga wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, Rwanda
Rwanda imeanza kuadhimisha Ijumaa kumbukumbu ya miaka 24 tangu kutokea mauaji ya halaiki yaliowauwa watu takriban millioni moja wengi wao wakiwa wa kabila la Watutsi.
Baraza la Seneti nchini Rwanda lilijadili Alhamisi suala la kutenga vituo vitatu vya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki na kuvigeuza sehemu ya Urithi wa Dunia. Sherehe hizo zitaendelea kwa wiki nzima ambapo taifa zima linakuwa katika maombolezi na nyumba za starehe husitisha huduma zote ila zile za dharura.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, baraza la seneti limepokea ripoti ya mashauri ya kitaifa ya kupambana na mauaji ya halaiki inayoelezea hatua zilizofikiwa katika mazungumzo yaliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.
Mwenyekiti wa mashauri hayo ya kupiga vita mauaji ya halaiki, Damascene Bizimana aliliambia bazara la seneti kwamba kuna timu ya wajumbe wa UNESCO watakaoshiriki kwenye sherehe za maadhimisho ya wiki moja ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki, na wajumbe hao watazuru vituo hivyo vitatu ili kuvitathmini iwapo vinatimiza masharti yatakayo wezesha kugeuzwa kuwa sehemu ya urithi wa dunia.

Sita wakiwemo watoto 4 wapoteza maisha Kenya

Ramani ikionyesha njia ya Nairobi-Mombasa
Watu sita wamepoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumamosi njia kuu ya Nairobi-Mombasa nchini Kenya karibu na kituo cha biashara cha Mariakani.
Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa polisi Kaloleni, Kennedy Onsando amesema kuwa ajali hiyo ilitokea katika majira ya saa kumi na mbili asubuhi.
Ajali hiyo ilihusisha gari ya abiria aina ya Nissan (Matatu) ambayo ilikuwa ikisafiri kuelekea Wundanyi kutoka Mombasa iliyogongana na gari la uchimbaji visima linalomilikwa na kampuni ya Deep Water Drilling.
Kamanda huyo amesema kuwa watu wanne akiwemo mwanamke mmoja na watoto watatu walikufa hapo hapo wakati mwanamke mwengine na mtoto walikufa wakiwa njiani kwenda hospitali kupatiwa matibabu katika kaunti ndogo ya Mariakani.
Kati ya wale waliouwawa katika ajali hiyo, walikuwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili na minne. Polisi wanamtafuta dereva wa gari ya uchimbaji ambaye alitoweka kutoka sehemu ya ajali.
Kuna kesi iliyowazi kwa upande wa dereva wa gari la uchimbaji kwa kubahatisha kuingia katika upande wa pili wa barabara na kusababisha gari ya abiria ya Matatu kupata ajali,” Onsando amesema.

UNHCR yalaani mauaji ya kinyama ya mtoto kambini Uganda

Mmoja ya kambi za wakimbizi inayoendeshwa na UNHCR iliyoko eneo la Kyangwali, Uganda, iliyopigwa picha Machi 20, 2018.
Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limelaani mauaji ya kinyama yaliyofanyika kwa mkimbizi mwenye umri wa miaka miwili kutoka Sudan Kusini, katika kambi ya wakimbizi ya Palabek, Wilaya ya Lamwo, Kaskazini mwa Uganda.
“Haya ni mauaji ya kutisha na kuwa hayawezi kuhalalishwa kwani ni kitendo cha kinyama cha uwendawazimu,” amesema, Joel Boutroue, Mwakilishi Mkazi wa UNHCR nchini Uganda.
“Kwa niaba ya UNHCR, ninapenda kufikisha rambirambi zetu zenye huzuni kubwa kwa familia ya mtoto aliyeuwawa.”
Kwa mujibu wa gazeti la The Monitor nchini Uganda pia amehimiza vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapewa ulinzi wa kutosha katika kambi hizo.
UNHCR kupitia mshirika wake Lutheran World Federation (LWF) ilisaidia gharama za maziko ya mtoto huyo aliyeuwawa Jumamosi.
Polisi nchini Uganda inaripotiwa kuwa imeanza uchunguzi kufuatia mauaji hayo. Hata hivyo mazingira na sababu zinazohusisha mauaji hayo hazijafahamika.
UNHCR imetoa wito kwa serikali ya Uganda kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo na kuhakikisha haki inatendeka.

Kakobe asema ameitwa uhamiaji kuhojiwa


Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema ameitwa kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji siku ya Jumatatu, Aprili 9, 2018.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumamosi Aprili 7, 2018 Askofu Kakobe amesema ataitikia wito huo.
“Wamenieleza kuwa wananiita kwa sababu ya mahojiano hivyo nitakwenda tu hakuna shida. Wameniita Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam,”amesema.

Magufuli aukumbuka wimbo wa ‘Wapo’ wa Ney


Rais John Magufuli ameukumbuka wimbo wa Ney wa Mitego wa ‘Wapo’ ambao ulifungiwa na baadaye kuagiza ufunguliwe.
Tukio hilo limetokea leo Aprili 7, alipokuwa akimaliza kuhutubia katika uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia mjini Arusha kitakachosaidia kutoa huduma kwa watalii na maofisa wa kibalozi.
Hafla hiyo imekwenda sambamba na uzinduzi wa nyumba 31 za polisi, ambapo wageni mbalimbali walihudhuria wakiwemo wakuu wa polisi wastaafu.
Hata hivyo, katika kutaka kuwataja mmoja mmoja waliohudhuria, Rais Magufuli alijikuta akitaja baadhi ya majina na kuongeza neno yupo na baadaye kusema kuwa angekuwa msanii angeimba ule wimbo wa ‘Wapo’, maneno yaliyosababisha umati uliohudhuria shughuli hiyo kushangalia.
Machi 26, mwaka jana wimbo huo wa Ney ulifungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), uliodaiwa kuwa ulimkashifu Rais.
Hata hivyo siku inayofuata, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kuufungulia, agizo ambalo alidai limetoka kwa Rais.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Rais alifurahishwa na ‘Wapo’ huku akimshauri mwanamuziki huo kutaja majina ya watu wengine kwenye wimbo huo kama vile wakwepa kodi, wauza unga, wabwia unga na watu wengine wasiokuwa na maadili.
Mbali ya kufungiwa wimbo, pia Ney alijikuta akikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa mjini Morogoro ambapo nao waliamuriwa kumwachia huru.

Magufuli: Kamateni kijiji kizima chenye mashamba ya bangi


Arusha. Rais John Magufuli ameagiza askari kuwakamata wazee, wanawake, vijana na watoto wa maeneo yanapobainika mashamba ya bangi akieleza kuwa wakikamatwa watasema ukweli na watazifyeka wenyewe.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Aprili 7 wakati akizungumza na wakazi wa Arusha Uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya kuzindua kituo cha polisi na nyumba 31 za polisi.
“Sitaki Jeshi la Polisi litumike kufyeka bangi, kwa nini mkafyeke bangi? Tumieni intelijensia yenu mkakae pale kijijini na mtajua nani anakwenda kukagua mashamba hayo. Nyie shikeni wote katika hicho kijiji, kamateni wote, wazee, wanawake hata watoto shika, ndipo watasema ukweli,” amesema.
Rais amesema wanaolima bangi wakikamatwa ndio wanaotakiwa kuzifyeka.

Diwani Chadema alia na Tarura


Dar es Salaam. Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Assenga amesema uamuzi wa Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara  za Mijini na Vijijini (Tarura)  umewaondolea madiwani nguvu na imani kwa wananchi.
Assenga ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Aprili 7, 2018 wakati akikabidhi msaada wa rangi za nyumba na mabati katika shule ya msingi Tabata Kisiwani, jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inatambua wazi kuwa barabara ni msingi mkubwa kwa madiwani hivyo kuwanyang'anya kunalenga kutaka kuwaonyesha wananchi kuwa hawafanyi kazi.
Amedai tangu barabara ziwe chini ya Tarura hakuna linalofanyika na matokeo yake wananchi wanawatupia lawama viongozi.
"Mvua zimenyesha, barabara zimeharibika na hakuna dalili ya kufanyiwa ukarabati hii yote lawama inakuja kwetu, niwaambie wananchi wasitunyooshee vidole madiwani hayo ni mambo ya Serikali,"amesema.
 "Serikali inatambua wazi jukumu la kujenga barabara likiwa chini ya diwani itaonekana anafanya kazi sana hasa katika kipindi hiki ambacho kata nyingi zinaongozwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), ndio sababu wakatunyang'anya,"
Kuhusu rangi hizo, amesema amechukua uamuzi huo kwa kuwa majengo ya shule hiyo hayakuwa katika muonekano mzuri.
"Kuna uwezekano tangu shule imejengwa haijawahi kukarabatiwa nimeona ipo haja ya kuanza kufanya ukarabati ili kuipa mwonekano mzuri," amesema.
"Nataka hata watoto wetu wanaosoma shule za ‘Kayumba’ nao wajisikie wapo sehemu nzuri, ndio sababu nilihakikisha wanaachana na kubeba ndoo za maji na nikawavutia maji ndani ya vyoo vyao vya shule."
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Evodius Katabazi amesema umekuja wakati muafaka.
"Kuta zimechoka na si kuta tu hata majengo na mapaa muonekano wake si mzuri. Ofisi ya walimu paa lake halifai kabisa, linavuja hali inayowapa wakati mgumu kuhifadhi nyaraka zao," amesema Katabazi.
"Kwahiyo naweza kusema msaada huu umekuja wakati muafaka na tunaomba wadau wengine watakaoguswa watusaidie kuiweka vizuri shule yetu," amesema Katabazi.

Tucta yataka watumishi darasa la saba kurejeshwa kazini

Morogoro. Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) leo Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya darasa la saba.
Akisoma tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini Nyamhokya amesema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka watumishi hao kurejeshwa kazini.
Amesema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.
Nyamhokya amesema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.
“Kwa hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi chote,” amesema.
Mambo mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni; ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.