Saturday, April 7

Diwani Chadema alia na Tarura


Dar es Salaam. Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Assenga amesema uamuzi wa Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara  za Mijini na Vijijini (Tarura)  umewaondolea madiwani nguvu na imani kwa wananchi.
Assenga ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Aprili 7, 2018 wakati akikabidhi msaada wa rangi za nyumba na mabati katika shule ya msingi Tabata Kisiwani, jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inatambua wazi kuwa barabara ni msingi mkubwa kwa madiwani hivyo kuwanyang'anya kunalenga kutaka kuwaonyesha wananchi kuwa hawafanyi kazi.
Amedai tangu barabara ziwe chini ya Tarura hakuna linalofanyika na matokeo yake wananchi wanawatupia lawama viongozi.
"Mvua zimenyesha, barabara zimeharibika na hakuna dalili ya kufanyiwa ukarabati hii yote lawama inakuja kwetu, niwaambie wananchi wasitunyooshee vidole madiwani hayo ni mambo ya Serikali,"amesema.
 "Serikali inatambua wazi jukumu la kujenga barabara likiwa chini ya diwani itaonekana anafanya kazi sana hasa katika kipindi hiki ambacho kata nyingi zinaongozwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), ndio sababu wakatunyang'anya,"
Kuhusu rangi hizo, amesema amechukua uamuzi huo kwa kuwa majengo ya shule hiyo hayakuwa katika muonekano mzuri.
"Kuna uwezekano tangu shule imejengwa haijawahi kukarabatiwa nimeona ipo haja ya kuanza kufanya ukarabati ili kuipa mwonekano mzuri," amesema.
"Nataka hata watoto wetu wanaosoma shule za ‘Kayumba’ nao wajisikie wapo sehemu nzuri, ndio sababu nilihakikisha wanaachana na kubeba ndoo za maji na nikawavutia maji ndani ya vyoo vyao vya shule."
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Evodius Katabazi amesema umekuja wakati muafaka.
"Kuta zimechoka na si kuta tu hata majengo na mapaa muonekano wake si mzuri. Ofisi ya walimu paa lake halifai kabisa, linavuja hali inayowapa wakati mgumu kuhifadhi nyaraka zao," amesema Katabazi.
"Kwahiyo naweza kusema msaada huu umekuja wakati muafaka na tunaomba wadau wengine watakaoguswa watusaidie kuiweka vizuri shule yetu," amesema Katabazi.

No comments:

Post a Comment