Rwanda, inaadhimisha miaka 24 tangu yafanyike mauaji ya kimbari.Mauaji hayo yalifanyika kote nchini humo isipokuwa wilaya moja tu.
Hiyo ni wilaya ya Giti kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Sababu ya wilaya hiyo kutoshuhudia mauaji ya kimbari ni mshikamano baina ya wananchi na uongozi uliosimama na kupinga kila aina ya uonevu.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana alipatembelea na kuzungumza na wenyeji wa eneo hilo
Mmoja wapo ni Fidele Ntabana anaelezea kuwa aliwekwa kizuizini kwa tuhuma za kuwa jasusi wa RPF lakini wananchi wa eneo hilo walilindana.
"Wahutu wa eneo hili walikuwa watu wazuri japo naweza kusema kwamba si wote kwa asilimia 100 lakini wengi hawakuwa na mpango wowote mbaya wa kuuwa watutsi.Familia yangu yote hakuna hata mmoja aliyeguswa.'' anasema
Watutsi kwa wahutu wanamsifu aliyekuwa kiongozi wao nyakati hizo, kunyima fursa propaganda za chuki na mauaji.
Mwenyeji mwingine, Andre Bisamaza anaelezea kuwa watu wabaya walikosa fursa ya kueneza propaganda ya mauaji.
Anasema kuwa "mara kadhaa wanamgambo Interahamwe walitumwa kutekeleza mauaji katika eneo hili lakini yeye na askari jeshi na polisi aliokuwa nao walilazimika kuingilia kati na kuwafukuza wanamgambo hao''
Aliyekuwa kiongozi wa wilaya hii ya zamani ya Giti Sebushumba Edouard sasa ni mzee aliyestaafu.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana alimkuta akisimamia shughuli za ukataji miti katika shamba lake.
Je ni siri gani aliyoitumia kuwaunganisha watu na kuhakikisha hakukuwa na mauaji katika eneo alililokuwa akiliongoza?
Bwana Edouard anasema kuwa ''kilichonisaidia ni desturi yangu kama kiongozi wakati huo ya kupinga uonevu ambayo pia niliijenga miongoni mwa wananchi wangu."
"Pia nilikuwa mtu asiyevumilia machafuko ya aina yoyote na kuadhibu wenye makosa.Kadhalika mimi na wasaidizi wangu tulikuwa tunaelewana kwa kauli moja.Ningelipata shida kubwa tusingekuwa na kauli moja.Ni wazi kwamba wananchi hawangeamua wenyewe kuuwa watutsi bila viongozi kuunga mkono vitendo hivyo'' anasema Edouard
Mwaka 1996 kiongozi huyo mstaafu alikuwa miongoni mwa wengine wengi waliotunukiwa medali za heshima kutokana na juhudi zao za kulinda raia wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.
No comments:
Post a Comment