Nairobi, Kenya. Mfanyabiashara anayeshika nafasi ya kwanza kwa utajiri barani Afrika, Aliko Dangote amekosoa utawala wa Kenya kwa ubinafsi wao na kuendelea kushindwa kuweka mbele masuala yenye maslahi kwa taifa linapokuja suala la maendeleo.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi mashuhuri wa Kenya Jeff Koinange, Dangote alisema alifuta mipango ya kujenga kiwanda kikubwa cha saruji baada ya kukatishwa tamaa na watoa maamuzi ambao aliwaita ni “mafisadi kuliko Wanigeria.”
Akizungumza katika kipindi cha alfajiri cha studio za redio FM, Jeff alielezea mazungumzo binafsi aliyofanya na Dangote alipohudhuria hafla iliyoandaliwa na bilionea huyo kwa ajili ya kumuaga binti yake mwezi uliopita nchini Nigeria.
“Nilimuuliza, ‘Al Hajj lini utakuja tena Kenya?’ na yeye alisema ‘Jeff, kuna watu wako kule (Kenya) ambao wametanguliza ubinafsi wao na maslahi binafsi kuliko ya taifa. Sikuwahi kufikiria Kenya ingekuwa imekubuhu kwa rushwa kuliko Nigeria,’” alielezea Koinange.
Dangote, anayekadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Shilingi za Kenya 1.5 trilioni kwa utafiti wa jarida la Forbes, alitembelea Kenya Septemba 2013 katika msafara wa wafanyabiashara matajiri 50 kutoka Nigeria walioongozana na rais wa wakati huo Goodluck Jonathan.
Tajiri huyo wa Nigeria hivi karibuni alisogeza hadi mwaka 2021 kuleta kiwanda chake nchini baadala ya mwaka ujao.
Dangote anafahamika kwa kupanga bei ya chini ili kudhibiti soko jipya na hatua ya kusogeza mbele itawapa nafuu wafanyabiashara wengine katika soko hilo ambalo linashuhudia ushindani mkali.
No comments:
Post a Comment