Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu imewapatia dhamana viongozi sita wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, lakini hata hivyo watasalia rumande hadi kesi wiki ijayo tarehe 3 Aprili ambapo wataletwa mahakamani kukamilisha masharti ya dhamana.
Wanasiasa hao hawakuletwa mahakamani katika uamuzi wa dhamana yao huku afisa wa magereza akiiambia mahakama ni kutokana na gari lililotakiwa kuwasafirisha kuja mahakamani hapo kuwa bovu
Baadhi ya masharti ya dhamana ni kila mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili pamoja na ya shilingi milioni 20, sawa na takribani dola 9000 za kimarekani.
- Tanzania: Viongozi sita wa upinzani waachiliwa kwa dhamana
- Miguna asafirishwa tena kutoka Kenya
- Kesi zinazowaandama Wanasiasa wa Upinzani Tanzania
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ni miongoni mwa wanachama na viongozi wa juu wa Chadema waliofika kufuatilia mwenendo wa kesi inayowakabili Mbowe na viongozi wengine wa chama.
Wafuasi wa chama hicho pia walijitokeza wakiwa nje ya mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakisubiri uamuzi wa mahakama juu ya rufaa .
Viongozi hao walikamatwa Jumanne wiki hii na kufikishwa mahakamani ambapo wanakabiliwa na makosa manane ikiwa pamoa na uchochezi na kukusanyika katika mkutano wa hadhara pasipo na kibali.
Awali wakili wa serikali Faraja Nchimbi alisema kosa lao la kwanza ni kuandaa mikusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.
Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa ni pamoja na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha NIT Akwilina Akwiline.
Wanashtakiwa pia kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali wilayani Kinondoni shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yote dhidi yao ambapo Wakili Nchimbi alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.
Awali kupitia afisa habari wa Tumaini Makene, Chama hicho kililaani vikali kukamatwa kwa viongozi wao na kusema ''Zimekua ni sarakasi dhidi ya upinzani...njama hizi dhidi viongozi wetu hatutaweza kuzinyamazia, tutaendelea kuzilaani na tunaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria''.
Kesi gani zinazowaandama wanasiasa wa upinzani hasa Chadema?
Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, kuna wabunge 13 wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali.Chama kikuu cha upinzani Chadema ndicho kinachoonekana kuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wake wanaozongwa na kesi mbali mbali.
Mbunge wa Singida, kupitia chama cha chadema Tundu Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu,anakabiliwa na kesi sita. Kesi zote zinahusiana na uchochezi.
Lissu anasemekana kuwa ndiye mwanasiasa aliyekamatwa mara nyingi zaidi ya wengine. Miongoni mwa kesi zake zilizoibua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi ni ile aliyoshutumiwa kutoa matamko ya uchochezi na kumuita Rais John Magufuli 'dikteta uchwara'.
Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la kazi zake za usanii Sugu, ambaye ni mbunge wa Mbeya mjini, sasa yuko gerezani kwa kipindi cha miezi mitano baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kutumia lugha za matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Kwa upande wake Halima Mdee, mbunge wa jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, yeye anazo kesi nne zote zikiwa za uchochezi ikiwemo ile aliyotuhumiwa kutumia lugha mbaya kumpinga Rais Magufuli baada ya kutangazwa kwa marufuku ya kuwaruhusu wanafunzi wa kike kurudi shuleni mara wapatapo ujauzito.
Mbunge wa Arusha Godbless Lema yeye anakabiliwa na kesi nne pia huku zote zikiwa za uchochezi. Siku za nyuma Lema aliwahi kukaa mahabusu kwa muda wa miezi minne kwa kosa la uchochezi. Hivi sasa Lema amekuwa akihudhuria mahakamani mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Chadema taifa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe yeye ana kesi 3 ikiwemo kesi ya wiki hii. Kwa sasa anahitajika kuhudhuria polisi kila siku.
John Mnyika mbunge wa jimbo la ubungo jijini Dar es salaam kwa upande wake anahitajika kuhudhuria polisi kila wiki tangu jaribio la kufanyika kwa maandamano ya chama hicho mwezi uliopita. Huyu kesi yake yeye bado haijawekwa wazi
Mbunge wa Mara, Esther Bulaya, aliwahi kushikiliwa na polisi kwa kosa la kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake, jambo ambalo polisi walidai kuwa lilikuwa ni uvunjifu wa sheria.
No comments:
Post a Comment