Saturday, March 10

UWT yapitisha vipaumbele vya miaka miwili


Dar es Salaam. Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia  kamati yake ya  utekelezaji ya baraza kuu umepitisha vipaumbele vyake vinne kwa mwaka 2018/20.
Akizungumza leo Jumamosi Machi 10, 2018 mwenyekiti wa umoja huo, Gaudensia Kabaka amesema kikao hicho kimekubaliana kuanza na vipaumbele hivyo vinne.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020, kwa kuungana na Serikali kupitia idara ya maendeleo ya jamii kuanzia kata mpaka Taifa.
“Wajibu wetu utakuwa kuhoji na kufuatilia huduma za jamii kama maji, elimu, afya ya mama na mtoto, lengo ni kuhakikisha kila kilichomo ndani ya ilani kinafanyiwa kazi kama kilivyoainishwa, ” amesema Kabaka.
Amesema kipaumbele cha pili ni kujiimarisha kiuchumi kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuendeleza vyanzo vilivyopo kuanzia ngazi ya kata mpaka Taifa.
“Vipo vyanzo vingi vya mapato ambavyo UWT haijaviibua, tunajipanga upya kuanza kujipambanua ili kuwa na tija katika jamii,” amesema.
“UWT si masikini, tuna mashamba, majumba na viwanja. Tumefanya tathmini ya kuvitambua kwanza katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam, tunaendelea katika mikoa mingine, ili tujiendeshe kwa tija zaidi.”
Amesema  kipaumbele kingine ni kuongeza wanachama kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa, “UWT kama chombo cha kisiasa lengo lake pia ni kushika dola, hivyo wanachama hawa wapya ni mtaji wa uchaguzi hasa tunapoelekea chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020,” amesema  Kabaka.
Amesema jambo lingine watakaloliangazia kwa karibu ni kuwajengea uwezo viongozi, watendaji, wanachama, vikundi vya wanawake vya uchumi na kijamii wakiwamo watoto katika masuala mbalimbali.
“Tutatoa mafunzo ya mbinu za uongozi nchi nzima na tayari tumeshajipanga kwa hilo, uchumi na ujasiriamali, mapambano dhidi ya rushwa na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto,” amesema.
“Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni suala linaloninyima raha, hata nikiiona habari yake gazetini au kwingineko huwa nashindwa kumaliza kuisoma kwa sababu inauma sana.”   

No comments:

Post a Comment