Tuesday, March 6

Siku ambayo Vladimir Putin alitokwa na machozi hadharani

Vladimir Putin and Lyudmila Narusova at Anatoly Sobchak's funeralHaki miliki ya pichaREUTERS
Raia wa Urusi wanapojiandaa kumchagua Vladimir Putin kuwa kiongozi wao kwa muhula wa nne mnamo 18 Machi, mwandishi wa BBC Gabriel Gatehouse ameangazia tukio la kipekee lililotokea mwanzoni mwa uongozi wa Putin ikulu.
Wakati huo alikuwa kaimu rais na alikuwa anawania urais kwa mara ya kwanza.
Warusi huwa ni nadra sana kumuona rais wao akilia, ingawa kumetokea mikasa mingi sana wakati wa utawala wake wa miaka 18.
Lakini ilitokea wakati mmoja, mwanzoni mwa utawala wake - mnamo 24 Februari 2000, wakati wa mazishi ya Anatoly Sobchak.
Sobchak alikuwa mmoja wa watu ambao, kwa pamoja na Gorbachev na Yeltsin, walisaidia kusambaratika kwa Muungano wa Usovieti.
Ndiye mwanamageuzi ambaye pia alimuinua afisa wa KGB kwa jina la Vladimir Putin ambaye alikuwa afisa wa kiwango cha wastani kutoka kutofahamika hadi kumpa kazi yake ya kwanza katika siasa.
Hakuna ajuaye hasa ni nini kilimhamasisha kuchukua hatua hiyo.
Lakini leo hii, mirengo ya watu wenye msimamo mkali kutoka kwa idara za usalama wakati wa Muungano wa Usovieti imechukua na kudhibiti mamlaka nchini Urusi kwa kiasi ambacho kimetishia demokrasia.
Mayor Anatoly Sobchak opens Austria Square in St Petersburg in September 1992, with Vladimir Putin (left) in attendanceHaki miliki ya pichaALAMY
Image captionMeya Anatoly Sobchak akifungua rasmi Uwanja wa Austria mjini St Petersburg mnamo Septemba 1992, akiambatana na Vladimir Putin (kushoto)
Kuna wagombea wanane wa wanaowania urais uchaguzi wa sasa, lakini Putin anafahamika kuwa "mgombea mkuu" na hakuna aliye na shaka kuhusu matokeo.
Mmoja wa wagombea wanaoshindana naye ameeleza uchaguzi huo kuwa "uchaguzi bandia".
"Ni kama tu katika chumba cha kuchezea kamari," anasema, "ambapo mwenye chumba ndiye hushinda wakati wote, katika demokrasia ya Urusi, ushindi wakati wote huwa upande wa Putin."
Jina lake mgombea huyu, usishangae, ni Ksenia Sobchak, na ni bintiye Anatoly, rafiki na mlezi wa kisiasa wa zamani wa Putin.


Ksenia, kama anavyofahamika, ana miaka 36 na ni mtangazaji wa zamani wa kipindi cha uhalisia kwenye runinga ambaye amejiingiza kwenye siasa na kuwa mwanasiasa wa upinzani.
Wafuasi wa kiongozi mkuu wa upinzani Alexei Navalny ambaye amezuiwa kuwania wanasema yeye ni kikaragosi wa ikulu ya Kremlin na rafiki wa zamani wa familia ambaye ameingizwa na Putin kwenye kinyang'anyiro cha urais kuupa uchaguzi huo hisia za uhalisia.
Bila shaka, hangeweza kuwania bila idhini ya watawala. Hivyo ndivyo siasa na demokrasia Urusi hufanya kazi.
Ksenia Sobchak election posterHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionBango la kampeni: "Kura kwa Sobchak. Kura kwa ukweli. Kura kwa uhuru."
Lakini wanaume wenye kuvalia nadhifu suti za rangi ya kijivu ambao huendesha mambo ikulu Urusi huenda kufikia sasa wanajutia hatua yao.
Ksenia kwa sasa anatembelea studio za runinga mbalimbani na kuwafichua washirika wafisadi wa Bw Putin na pia kueleza hatua ya Urusi ya kutwaa eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine kama iliyo haramu.
Iwapo anawania, kama asemavyo, ndipo ashinde na si asikike tu, basi anavunja miiko fulani.
Nini kinatendeka kweli?
Tumwache binti kwa muda na tumuangazie babake.
Alikuwa meya wa St Petersburg, mji wa pili kwa umuhimu baada ya Moscow. Putin alikuwa naibu wake.
Wawili hao walikuwa na urafiki wa karibu sana kiasi kwamba Sobchak alipotuhumiwa kuhusika katika ulaji rushwa, Putin alimsaidia kuikimbia nchi hiyo akiwa ameabiri ndege maalum ya kukodishwa.
Hayo yalitokea miaka ya 1990.


Wazikumbuka siku hizo? Urusi ilikuwa kwenye vurugu.
Rais wake, Boris Yeltsin, alikuwa mlevu mara kwa mara na hakuimudu kazi.
Wanaume wenye suti za majivu Kremlin walifikia wamepata suluhu - mtu mwingine mwenye kuvalia suti za kijivu, asiye na doa, ambaye kutoka kwake wangeunda dawa ya kumkabili Yeltsin.
Walianza kumlea Putin kama mrithi wa Boris.
Kisha, ghafla, Putin alipokuwa anawania urais kwa mara ya kwanza, rafiki yake wa zamani Anatoly Sobchak, akafariki akiwa na umri wa miaka 62, akiwa chumba chake hotelini Kaliningrad.
Uchunguzi wa maiti yake ulisemakwamba alifariki kutokana na mshtuko wa moyo ingawa hakukuonekana dalili zozote za mshtuko wa moyo.
Mjane wa Sobchak alishuku kwamba mumewe alikuwa ameuawa na maafisa walikuwa wanaficha ukweli, na akaagiza uchunguzi huru wa maiti ufanyike.
Jina lake ni Lyudmila Narusova.
Nilikutana naye majuzi na kumwuliza iwapo alifikiri mumewe aliuawa.
Alitulia na kunyamaza kwa muda unaotosha kusema "Ndio" mara kumi, kisha akasema: "Sijui".
Ksenia Sobchak, Vladimir Putin and Lyudmila Narusova at a meeting to commemorate Anatoly Sobchak in February 2001Haki miliki ya pichaALAMY
Image captionKsenia Sobchak, Vladimir Putin na Lyudmila Narusova ibada ya kumkumbuka Anatoly Sobchak
Baadhi wamedokeza kwamba Putin huenda alihusika katika kifo cha Sobchak.
Sobchak alikuwa na siri kumhusu Putin? Narusova alipuuzilia mbali wazo hilo mara moja.
Nilirudi na kuangalia kwa makini video ya mazishi ya mwanasiasa huyo.
Putin anaonekana kuhuzunika sana. Macho yake mekundu, anaonekana kutatizika kumeza kitu kilichokwama kooni, huku akimkumbatia Lyudmila Narusova. Putin si mwigizaji.
Aidha, si mtu ambaye watu wamemzoea kuonesha hisia zake hadharani.
Hivyo, inaeleweka, kuamini kwamba anakabiliana na simanzi na majonzi halisi. Au ni kitu kingine? Dhamira yake inamhukumu?
"Kulikuwa na watu waliokuwa wanamsaidia Putin kuingia madarakani," Nasurova ananiambia.
Yuko sahihi.
Wakati huo, Putin alikuwa chombo cha kufikia madaraka kwa baadhi ya mirengo ya watu ndani ya Kremlin. Na kwa kiasi fulani bado yeye ni chombo.
Iwapo Sobchak aliuawa, aliuawa basi na moja ya mirengo hiyo iliyohofia kwamba mtu aliyemlea angechukua madaraka? Pengine. Na ikiwa ni hivyo, afisa huyo wa KGB aligundua kweli kwamba rafiki yake aliuawa akijaribu kuendeleza Mradi Putin. Ni jambo la kudhania tu, lakini naanza kufikiria hivyo.
Vladimir Putin and Lyudmila Narusova revisit Sobchak's grave in 2007Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionVladimir Putin and Lyudmila Narusova revisit Sobchak's grave in 2007
Nilimwuliza Narusova kuhusu uchunguzi wa maiti uliofanywa kwa amri yake.
Anasema hakutoa matokeo hayo hadharani, lakini bado ameweka stakabadhi hizo kwenye sefu katika eneo salama nje ya Urusi.
Nilipomwuliza ni kwa nini, hakusema.
Nilimshinikiza. Nilimwambia, "Inaonekana kana kwamba umejipatia kitu kama mpango wa bima."
"Unaweza kulitazama hivyo," alijibu.
"Una wasiwasi?" nilimwuliza, "kuhusu usalama wako au wa binti yako?"
Anakaa kimya kidogo kisha kusema: "Unajua, kuishi katika nchi hii ni jambo la kuogofya. Hasa kwa wale ambao wana msimamo pinzani na wa serikali. Hivyo ndio, nina wasiwasi, wasiwasi ninao..."

No comments:

Post a Comment