Wednesday, March 14

Profesa Maghembe atetea GMO

esa Maghembe atetea GMO

Profesa Jumanne Maghembe akiangalia miche mipya
Profesa Jumanne Maghembe akiangalia miche mipya ya kahawa inayohimili magonjwa alipotembelea taasisi ya utafiti ya Lyamungo (TaCRI) wilayani Hai, Kilimanjaro. 
Wakati kukiwa na wasiwasi kwa baadhi ya nchi za Afrika kuvamiwa na kinachotajwa kuwa ni ukoloni mpya wa chakula kupitia mbegu zinazozalishwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni yaani Genetic Modified Organism au GMO, baadhi ya wanasayansi wamepinga dhana hiyo wakitaja faida lukuki za teknolojia hiyo.
Wasiwasi wa wasomi hao umekuja wakati Serikali ikiwa imeruhusu utafiti wa uzalishaji wa mbegu kwa teknolojia ya uhandisi jeni au GMO mwaka 2016 baada ya kufanya tathmini ya kina kuhusu madhara yake kwa binadamu na mazingira.
Mpaka sasa wanasayansi wa Tanzania wanaendelea na utafiti wa mbegu za mahindi kupitia mradi wa Water Efficient Maize for Africa unaohusisha nchi tano ambazo ni Tanzania, Msumbiji, Kenya, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda.
Mpaka sasa mradi huo umeshazalisha mbegu za mahindi kwa njia ya kawaida (conventional method) yakiwa na sifa ya kukabiliana na ukame, huku utafiti mwingine wa mbegu za uhandisi jeni ukiendelea katika shamba kitalu lililoko Makutopora mkoani Dodoma.
Mbali na mahindi, Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Mikocheni Dar es Salaam (Mari) kinaendelea na utafiti wa mbegu za GMO katika zao la muhogo.
Miongoni mwa wataalamu wa sayansi ya mimea anayetetea GMO ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu, Profesa Maghembe ambaye pia ni waziri mstaafu kwa nyakati tofauti tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 akishika wizara za Elimu, Kilimo pamoja na Maliasili na Utalii, anasema Tanzania imechelewesha utafiti wa GMO na hivyo imejipotezea fursa za chakula na biashara.
Swali: Kwa nini unasema Tanzania imechelewa kuruhusu tafiti za GMO?
Jibu: Tumeweka sheria na kanuni ngumu ili kuzuia uzalishaji wa mazao yatokanayo na GMO huku wenyewe ni watumiaji wakubwa wa bidhaa na mazao. Zaidi ya asilimia 75 ya nguo zinazovaliwa na Watanzania zinatokana mbegu za GMO kutoka nchi za kigeni.
Swali: Umeanza kufafanua zao la pamba, hali ikoje kwa nchi za kigeni zinazotumia teknolojia hiyo?
Jibu: Nchi za Marekani, Urusi, China, India, Pakistan, Misri, Sudan, Mali, Burkina Faso na hata Kenya wameamua kuzalisha ‘BT Cotton’ (biotech cotton) na kuachana na nitakayoiita “Kienyeji Cotton’’ tunayoilima sisi.
Kwanza Bt Cotton haina madhara inapolimwa, kuvunwa, kutengenezwa kuwa bidhaa na katika kutumia bidhaa zake. Mpaka leo sijaona ushahidi wa kisayansi unaoonyesha madhara.
Isitoshe, pamba ya GMO ina thamani kubwa zaidi (kwa kila kilo au tani ikiwa sokoni kuliko ile ya kienyeji. Pamba hiyo ina nyuzi (lint) ndefu zaidi ya ile ya kienyeji na kwa hiyo inapata bei nzuri zaidi sokoni.
Halafu BT cotton ina tija zaidi katika kuzalisha pamba shambani. Pamba ya kienyeji yetu inazalisha kilo 300 kwa hekta moja, wakati uzalishaji wa Bt Cotton katika majaribio shambani ni kilo 2500 mpaka kilo 3000 kwa hekta moja.
Swali: Kumekuwa na madai kuwa uzalishaji wa GMO una gharama kubwa, unasemaje?
Jibu: Siyo kweli. Uzalishaji wa GMO humpunguzia mkulima gharama kwa kuwa pamba ya GMO ina uwezo wa Bt cotton kuhimili baadhi ya mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya pamba na hivyo kupunguza upuliziaji wa dawa (mpaka asilimia 50).
Kwa mfano BT cotton inahimili kuliwa na funza mwekundu (American Red Ball worm). Sababu hii ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa ni sababu mahususi itakayotuwezesha kuondoa karantini ya kupanda pamba iliyopo sasa kwa mikoa ya Kusini mwa nchi yetu.
Sifa nyingine muhimu ni uwezo mkubwa wa kuhimili ukame hasa kwa mikoa yetu inayolima pamba kwa wingi kama Simiyu, Shinyanga na hata Mwanza.
Swali: Kama kuna faida hizo, kwa nini kumekuwa na wasiwasi hivyo na nini madhara yake?
Jibu: Woga wetu hauna msingi wa kisayansi unatufanya tushikilie sheria na kanuni zilizopitwa na wakati na kuendelea kulima “Kienyeji cotton”. Kwa kufanya hivyo, tunawanyima fursa wakulima wa pamba kujiongezea mapato na kujiondoa kwenye lindi la umaskini.
Swali: Umezungumzia zaidi pamba ambayo ni zao la biashara, huna mfano wa zao la chakula?
Jibu: Mfano wa magonjwa yaliyoanza kudhibitiwa kwa kutumia teknolojia ni tatizo la mnyauko wa migomba mkoani Kagera ambalo ni la muda mrefu. Lakini ufumbuzi umepatikana baada ya kituo cha utafiti wa kilimo mkoani humo cha Maruku Agric Research Station kuzalisha miche ya migomba yenye jeni (genes) za zao la pilipili hoho zinazokinzana na virusi vya mnyauko.
Swali: Wasiwasi mwingine kwa wapinzani wa GMO ni kwamba wataalamu wetu wanachukua mbegu zilizofanyiwa teknolojia nje ya nchi na kuleta kwetu, hiyo ni kweli?
Jibu: Ni kweli, kuna watu wanadhani sisi tunanunua mbegu toka huko. Wanadhani hatuna uwezo, wenye uwezo ni Wazungu tu.
Utafiti wa GMO tunaousema na kuelezea tija yake tunaufanya wenyewe. Baadhi ya wanasayansi wetu wana ubingwa na sifa za hali yajuu sana unaotambuliwa na kupigiwa mfano duniani.
Kwa mfano, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa kilimo ya Mikocheni Dar es Salaam (Mari), Dk Joseph Ndunguru amebobea katika utafiti wa zao la muhogo.
Wakati Watanzania wakiogopa tafiti za GMO, baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zimeshaanza kutumia mbegu zilizozalishwa katika kituo cha utafiti wa kilimo cha Ukiriguru jijini Mwanza.
Swali: Wasiwasi mwingine ni wa kupoteza mbegu za asili, hilo unasemaje?
Jibu: Tunayo TPRI (Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu) Arusha, tunayo pia benki ya vinasaba au National Gene Bank. Katika benki yetu tunaweka aina zote za jamii na tabia za mazao yanayotumika katika kila kata, tarafa na wilaya za Tanzania.
Kama hakuna mbegu kama migomba tunahifadhi cuttings and cells za mazao na mimea hiyo. Kama ambavyo wanajeshi wanatumia Rifles, AK 48 na Sub Machine Guns mpaka leo ( pamoja na kugundua short na long range missile, ballistic missiles na hata nuclear powered ballistic missiles).
Mbegu zetu za asili ni muhimu sana leo na hata kesho, ndizo zinazobeba genes na mabadiliko kwenye eneo letu hili la Dunia.

No comments:

Post a Comment