Wednesday, March 14

Mfanyabiashara ahukumiwa kifungo miaka 81 jela


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha miaka 81 jela mfanyabiashara Timotheo Wandiba baada ya kutiwa hatiani katika mashtaka 27 ya kujipatia Sh2.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.
Mbali ya Wandiba, mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wenzake wawili; Dickson Okololo na Simon Efrem ambao upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao pasipo kuacha shaka.
Akisoma hukumu hiyo leo Machi 13, 2018 iliyoandikwa na Hakimu Joyce Minde, Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri amesema washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na makosa 82 ambapo upande wa mashtaka uliita mashahidi 14.
Katika makosa hayo 82, mashtaka 27 ni ya kughushi, 27 ya kutoa hati za uongo, 27 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na moja la utakatishaji fedha.
Hakimu Mashauri amesema mahakama hiyo imemtia hatiani Wandiba katika makosa 27 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu baada ya kuridhishwa na ushahidi  uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.
Katika makosa hayo, Mashauri amesema katika kila kosa Wandiba atatumikia kifungo cha  miaka 3 jela ambapo jumla itakuwa ni miaka 81, lakini kwa kuwa vifungo hivyo vitakwenda sambamba atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Pia, hakimu amesema mahakama hiyo imemuachia huru Wandiba na wenzake, Okololo na Efrem katika makosa mengine yote baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuyathibitisha pasipo kuacha shaka.
Katika kesi hiyo washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na makosa 82 ikiwemo kughushi, utakatishaji fedha na uwasilishaji wa nyaraka za uongo.
Wakati kesi hiyo ikiendeshwa washtakiwa walikuwa rumande kutokana na kukabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha ambapo kwa mujibu wa sheria halina dhamana.

No comments:

Post a Comment