Friday, December 1

‘WASICHANA HUJIUNGA KIDATO CHA TANO NA UJAUZITO’

MKUU wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru wilayani Ilemela, Meltilda Shija, amesema wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wamekuwa wakijiunga sekondari na ujauzito.
Amesema kwa sababu hiyo  wameanza kuwapima kila wanapojiunga na kidato cha tano.
Alikuwa akizungumza juzi wakati wa ufunguzi wa Kiwanda cha Bwiru Girls Initiative.
Shija alisema   alichokibaini ni kuwa wanafunzi wengi huwa huru baada ya kumaliza kidatu cha nne hivyo kujikuta wakishiriki ngono na hata wanapochaguliwa kujiunga kidato cha tano baadhi yao wamekuwa wakiwa na ujauzito.
“Mwaka jana tulipopokea wanafunzi wa kidato cha tano  Julai na kuwapima tulibaini baadhi yao wana mimba za miezi tisa, nane na sita jambo hili limejirudia kwa mwaka huu inasikitisha sana.
“Naomba  uwepo   msisitizo kwa viongozi mbalimbali wa kata, mitaa na vijiji kuwabaini wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne katika maeneo yao na kuwa nao karibu  kuwaokoa na janga la mimba,” alisema Shija.
Alisema wamekuwa wakipokea wanafunzi   lakini kumbe kipindi cha kusubiri matokeo wamekuwa wakiachwa na kujiingiza kwenye matatizo yanayowaharibia ndoto zao hivyo kujikuta wakiwa na ujauzito.
Shija alisema  mkakati wa shule yake ni kuwapima kila mara ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujisimamia na kuepuka vishawishi.
Alisema mkakati mingine  ni kujenga kiwanda hicho ambacho kitawashughulisha zaidi kupata stadi za maisha badala ya kutumia muda wao kwa mambo yasiyo na faida kwao.
Mkuu huyo wa shule  alisema ingawa kuanzishwa  kiwanda hicho pia kutasaidia kuwashughulisha hivyo kuwapunguzia muda wa kuwaza masuala ya ngono.
“Kiwanda hiki kimefanikiwa kushona sare zinazozingatia maadili ya shule na jamii kwa wanafunzi wa kidato cha tano ambazo ni sketi 700, magauni 700 na hijabu 200.
“Mauzo ya vituo hivyo yameokoa  Sh milioni 3.2 ambazo  zingetumika kama wangeshona sare hizo mtaani,” alisema na kuongeza kuwa mapato yameingizwa katika akaunti ya kujitegemea ya wanafunzi.
Akifungua kiwanda hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza , John Mongella, Mbunge wa   Ilemela, Angelina Mabula, aliwapongeza wanafunzi hao kwa kubuni wazo la kuanzisha kiwanda hicho.
Aliahidi kushirikiana nao kwa kuwashirikisha  wataalamu kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) na kuangalia namna ya kuboresha vifungashio vya bidhaa zao ili ziendane na soko.
Pia alishauri kuanzishwa   kitengo maalum kwa ajili ya kiwanda hicho   waweze kufikia malengo waliojiwekea na kufanikisha lengo la kuwa washonaji wa sare za shule zote za manispaa hiyo kusaidia kuwapunguzia wazazi gharama.
Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliahidi kukisaidia kiwanda hicho mtaji wa Sh milioni moja.
Alisema fedha hizo  zitatumika kununulia majora ya vitambaa   na kemikali za kutengenezea sabuni za maji na kiwi na matofali yote yatakayotumika kawa ajili ya ujenzi wa jengo la kiwanda hicho.
Aliitaka halmashauri hiyo kulimalizia litakapokamilika .
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la Kivulini, Yassin Ally, alisema azma yao ni kuwaona watoto wa kike  shuleni wanawezeshwa kuwa wanufaika na kushiriki katika Tanzania ya viwanda.

No comments:

Post a Comment