Wednesday, December 6

Rais Magufuli atuma rambirambi kifo cha Bendera


Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameomboleza kifo cha mkuu wa mkoa mstaafu, Joel Bendera kilichotokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). 
“Jioni hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa mstaafu Dk Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa na msiba huu, pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi,” amesema Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu leo Jumatano Desemba 6,2017.
Bendera amefariki dunia jioni ya leo katika Hospitali ya Muhimbili alikofikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.
Rais Magufuli amesema Bendera atakumbukwa kwa mchango alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo ukuu wa mkoa, naibu waziri na mbunge. Pia, katika maendeleo ya michezo.
“Alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka,” amesema Rais Magufuli.
Pia, amewapa pole wananchi wa mikoa ya Manyara alikokuwa mkuu wa mkoa Oktoba 26,2017 na mkoani Tanga alikokuwa mbunge.
Rais Magufuli ametoa pole kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanamichezo na wote walioguswa na msiba huo.

No comments:

Post a Comment