Wednesday, December 6

RAIS JPM KUZINDUA KAMPENI YA UZALENDO NA UTAIFA ‘NCHI YANGU KWANZA’

Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dk John Pombe Magufuli anataraji kuwa mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ utakaofanyika Ijumaa hii Disemba 8, 2017 kupitia ‘Usiku Wa Kitendawili’ mjini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa habari Msanii  wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto kupitia Kikundi cha Sanaa cha Mpoto Theatre Gallery na wadau wa sanaa za Ubunifu ndio wataouratibu usiku huo wa Kitendawili kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Sanaa utamaduni na Michezo.
Usiku wa Kitendawili ulianzishwa baada ya msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto kuachia wimbo ‘Kitendawili’ na baadaye kufikiria kuanzisha usiku wa wimbo huo na kuanzisha mjadala kuhusu uzalendo.
Akiongea na wadau wa sanaa katika Maandalizi ya Kampeni hiyo ya Kitaifa itayokuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julis Kambarage Nyerere, Mrisho Mpoto amesema kampeni hiyo ina lengo la kurejesha hali ya Uzalendo na Utaifa katika kutatua changamoto zilizojitokeza na zitakazojitokeza ndani ya Taifa letu.
Alisema mambo ambayo yatayozingatiwa katika kampeni hiyo ni pamoja na kudhubiti na hatimaye kukomesha kabisa mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa Umma, kuongezeka kwa tuhuma za rushwa, kuibuka ufisadi, ubadhilifu wa mali za Umma pamoja kuongeza hari ya kufanya kazi na Uzalendo.
“Usiku wa Kitendawili utatumika kama jukwaa la kuwaleta pamoja watanzania pamoja na viongozi wao ili kukumbushana kuhusu wajibu na kujadili mustakabali wa Taifa. Kutakuwa na vivutio mbalimbali pamoja na wimbo maalumu kutoka kwa wasanii maalumu Mwaka Huu,” alisema Mpoto.
Aliongeza,”Tumekuja kuunadi Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ kwasababu tunaamini Uzalendo na Utaifa lazima uwepo ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuunga mkono juhudi za Raisi Dkt. John Pombe Magufuli za kujenga Taifa lenye Uzalendo, Utu, Weledi na Uadilifu uliotukuka. Mimi ni mzalendo ndio maana hata kwenye hizi harakati nipo toka nimetoa wimbo wangu wa kwanza, ukiangalia nyimbo zangu zote ni za kuonganisha jamiii 120 za watanzani,”
“Naamini kwenye kufanya kazi ambayo itawafanya watanzania pamoja na kizazi kijacho kitambue kuna watu ambao walifanya kazi kubwa kwenye hili taifa, kuacha alama ambazo haziwezi kufutika katika maisha ya historia ya nchi hii, kwa sababu hivi vyote ambavyo vinaenda kufanywa ni kufufua upya na kuiweka pamoja mitazamo ya watanzania ili kujenga Taifa la Wazalendo na Wachapakazi kuiga nyayo zilizoachwa na hayati Baba wa Taifa,” alifafanua zaidi.
Mpoto amesema lengo kuu la maadhimisho hayo kuambatana na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa kuanzia mwaka 2018 ni kutumia jukwaa hilo kufikisha ujumbe wa umuhimu wa kujenga na kuendeleza Utaifa.
Alisema baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo wiki hii huko Dodoma, itafanyika kwenye mikoa yote nchini na itasimamiwa na Kamati za Utamaduni chini ya Uwenyekiti wa Mkuu wa Mkoa na  Wilaya.

No comments:

Post a Comment