WAZIRI wa Elimu, Sayansi , Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema ikiwa taifa litashindwa kusonga mbele kwa maendeleo litachangiwa na watu kukosa hofu ya Mungu.
Kauli hiyo aliiyoa Dar es Salaam jana katika ibada maalumu ya kuwaombea wanafunzi wa vyuo vikuu iliyoandaliwa na Kanisa la Tanzania Assemblies of God linalojulikana kama City Christian Centre lililopo Upanga.
Alisema ni jambo la busara na lenye kumpendeza Mungu kwa TAG kuandaa ibada hiyo kwa vile vijana wengi siku hizi wamekuwa wakijiingiza katika makundi yasiyofaa yakiwamo ya kutumia dawa za kulevya.
Waziri alisema vijana ndiyo taifa la leo na kama wengi wao wanahitaji kuingia katika siasa baadaye basi ni vema wakawa na hofu ya Mungu ili baada ya siasa kuwaneemesha waweze kuitumikia jamii.
“Nimeona Mchungaji alipouliza wangapi baada ya kumaliza vyuo vyao wanataka siasa wengi mlinyoosha mikono.
“Hapa ni vizuri mkajua kwenye siasa si kwa ajili ya kujitumikia ninyi wenyewe bali kuwatumikia Watanzania walio wengi na wenye mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Alisema kanisa lina wajibu wa kuwafundisha vijana uadilifu na endapo wakiwa na hofu ya Mungu basi mambo maovu yataepukika.
Alisema ni lazima kijana huyo atakuwa na uwezo wa kupambana na watu wenye utovu wa nidhamu, watumiaji wa dawa za kulevya kama ambavyo serikali inafanya kwa sasa sambamba na kupambana na ufisaidi.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Ranwell Mwenisongole, alisema ibada ya aina hiyo itakuwa inafanyika mwaka hadi mwaka lengo likiwa ni kuongeza maadili na mioyo ya upendo kwa wanafunzi na vijana.
Baadhi ya wanafunzi waliliohudhuria ibada hiyo wanatoka Chuo cha Afya Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), Chuo cha Usafirishaji (NIT) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
No comments:
Post a Comment