Monday, December 4

Namna idadi ya wanaosusa ving’amuzi ilivyoongezeka kwa kasi nchini


Asilimia 29.4 ya waliokuwa wamenunua ving’amuzi mwaka jana walikuwa
hawavitumii ikilinganishwa na asilimia sifuri mwaka 2014
Takribani theluthi moja ya watumiaji wa ving’amuzi nchini hawavitumii
tena vifaa hivyo kutazama luninga, kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka mitano iliyo-pita. Wachambuzi wa masuala ya habari na mawasiliano wanaeleza kuwa mwenendo huo uliopaa kwa kasi ndani ya miaka mita-tu iliyopita unahatarisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi kupitia luninga. Uchambuzi wa takwimu za robo ya pili
ya mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa idadi ya ving’amuzi
vinavyonunuliwa inaongezeka kila mwaka, lakini ukuaji huo unaathiriwa na kasi ya kupaa kwa ving’amuzi visivyotumika kwa muda mrefu. Takwimu hizo zinabainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka 2016 Tanzania ili-kuwa na ving’amuzi milioni 1.7 hata hivyo watumiaji 500,000 walikuwa hawavitumii
kwa wakati huo sawa na asilimia 29.4 ya ving’amuzi vyote vilivyokuwa vimenu-nuliwa. Idadi ya watu wenye ving’amuzi lakini hawavitumii ilianza kupanda miaka miwili iliyopita kutoka asilimia sifuri mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka jana huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa ukata umesababisha kutotumia vifaa hivyo vya dijitali. Ikumbukwe kuwa mwaka 2014
ving’amuzi vyote vilivyokuwepo nchini vilikuwa vinafanya kazi.
Baadhi ya wananchi walimweleza mwandishi wetu kuwa licha ya ukata baa-dhi ya kampuni za huduma za ving’amuzizinabadilibadili mifumo ya kulipia kila
mwisho wa mwezi kiasi cha kuleta ugumu kufanikisha malipo kwa wakati.
Pia uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya watu walikuwa wamenunua zaidi ya king’amuzi kimoja kutimiza mahitaji yao ya luninga, lakini kutokana na ukata wamelazimika kubakiza kimoja huku nacho wakilipia kwa msimu.
Mkazi wa Tabata, Athumani Bendera anasema malipo ya kila mwezi yanamtesa kutokana na ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa sasa ndiyo maana hatumii ving’amuzi mara kwa mara.
“Nina ving’amuzi vya Azam na StarTimes lakini hali ni ile ile kwani bila kufanya malipo ya mwezi sahau kupata chaneli za ndani ambazo nyingi hutuhabarisha habari za kitaifa na taarifa mbalimbali, sasa kwanini iwe hivi?” alihoji Bendera.
Ukosefu wa fedha za kulipia ving’amuzi kwa baadhi umefanya wategemee huduma za luninga kwenye vibanda ama sehemu za huduma kama baa na kwenye migahawa.
Zaharia Mohamed alisema kipindi anachoshindwa kulipia ankara ya king’amuzi hupata habari kupitia vijiwe tena zile ambazo zimekuwa gumzo mbali na hapo hushindwa kupata taarifa rasmi.
“Malipo ya mwezi si chini ya Sh10, 000 kwa kingamuzi kimoja na pia unaweza kulipia kifurushi cha wiki mbili kwa Sh6,000 jambo ambalo huwezi kukidhi mahitaji hivyo hushindwa kupata taarifa hasa ukilinganisha na hali ya maisha kwa sasa,”anasema Zaharia.
Wakala wa ving’amuzi na muuzaji wa vifaa vya luninga, Dotto Ally anasema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wateja hasa wa ving’amuzi vya StarTimes wakidai antena ndio kikwazo kikubwa.
“Wateja walio wengi wanalalamikia antena kuwa na gharama kubwa licha ya king’amuzi chenyewe hali inayowafanya kutumia njia mbadala na kukosa ubora wa picha wakati wa kuangalia taarifa kupitia luninga,” anasema Ally.
Mbali na kuuza ving’amuzi kulingana na msimu, Ally anabainisha kwa sasa bei za ving’amuzi na gharama za mwezi zimeshuka tofauti na zamani huku mfumo wa malipo kwa channeli za ndani ikiwa ni kilio kikubwa.
“Bei ya kifurushi cha Dstv Compact zamani ilikuwa Sh219,000 kwa sasa imeshuka hadi Sh 120,000. Mbali na kushuka kwa bei za ving’amuzi bado wateja wengi wanashindwa malipo kwa mwezi na kusababisha wasivitumie,” anasema Ally.
Omari Ahmed, fundi wa antena na madishi anayefanya kazi katika ofisi za StarTimes Buguruni anasema wateja wengi hawafuati ushauri wa kiufundi ndiyo maana hujikuta wakinunua ving’amuzi vingi ambavyo bado baadhi hupata picha dhaifu.
“Wengi wana zaidi ya king’amuzi kimoja na ukiuliza wanasema walinunua ili kupata picha bora na chaneli nyingi zaidi lakini matokeo yake hawajapata,” anasema.
Kauli za wachumi
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema uchumi pekee hauwezi kuwa sababu ya kuongezeka idadi ya watu wanaoshindwa kutumia ving’amuzi.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi anasema hali ya uchumi kwa sasa haisababishi watu kushindwa kununua ving’amuzi kwani wanaendana na mabadiliko ya teknolojia.
Profesa Moshi anasema simu za kisasa zimechukua nafasi kubwa kuliko hata matumizi ya luninga kwa sasa hasa ikizingatiwa bei za simu za inteneti imekuwa rahisi kuliko zamani.
“Mabadiliko ya teknolojia kwa simu ambazo zinakupa kila kitu zimechagiza kushuka na kupoteza umaarufu wa ving’amuzi. Siku hizi kila kitu unapata katika simu kitu ambacho starehe zote unapata humo hivyo wahusika wanatakiwa kuwa wabunifu katika hili ili kuwa washindani,”anasema Profesa Moshi.
Hata hivyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Pili Mtambalike anasema mfumo wa ulipiaji wa kila mwezi ndio chanzo kikubwa kwa wananchi kukosa taarifa hivyo kuna haja kwa mamlaka husika kukaa upya kuchunguza tatizo.
Mtambalike anasema uchumi wa nchi haumpatii tu wa kawaida fursa ya kupata habari kwani wanaishi chini ya Dola moja za Marekani ni ngumu mtu kulipia king’amuzi kwa ajili ya kupata taarifa.
“Watu hawawezi kuhangaikia kutafuta fedha za chakula halafu bado wanalipia kupata taarifa iwapo muda wa malipo umefikia kikomo ni suala la kukaa kwa wataalamu wa mamlaka husika ili kujadili mfumo mpya ambao tumekubali kuingia kwa miaka ya nyuma,” anasema Mtambalike.
Anasema kulingana na takwimu hizo ni wazi kuwa watu wengi hawapati taarifa kwani hata yeye anamiliki ving’amuzi vitatu ambavyo kwa mahitaji mbalimbali ilimlazimu kuvinunua.
Ofisa habari wa Kampuni ya StarTimes Media, Juma Suluhu anasema kampuni yao imetoa aina mbili ya ving’amuzi wateja wao ambavyo wanaweza kuangalia chaneli zote bila ya malipo.
Anasema baada ya kulipia malipo ya awali king’amuzi kingine wanalipia fedha kidogo kwa ajili ya matengenezo.
“Tuna ving’amuzi viwili kimoja ni bure kabisa, kingine unalipia kidogo ili kuweza kupata channeli nyingi zaidi,”anasema Suluhu.
Suluhu anasema katika kipindi cha kuhamia katika mfumo wa kidigitali walitengeneza ving’amuzi kwa bei ya chini ambavyo viligharimu dola 50 hadi 55 za Marekani mbali na bei halisi ya Dola za Marekani 60 kwa seti moja ya kingamuzi.
“Bei hizo zinajumuisha na kufungiwa king’amuzi na vifaa vyote ikiwemo rimoti, huku mtumiaji akipata chaneli 30 zikiwemo za nje na kulipia gharama ya mwezi kwa matengenezo ya dola 3 za kimarekani,” anasema.
Anasema katika mpango wa upya, zaidi ya vijiji 10,000 vitapata televisheni za dijitali ikiwa ni muendelezo kwa watu kuweza kupata taarifa kwa njia ya kidigitali na tayari vijiji 800 Tanzania wamepatiwa televisheni hizo.
TCRA hawakuweza kujibu maswali yetu kwa wakati kuelezea kiundani hali hiyo licha ya kuwatumia maswali zaidi ya mwezi mmoja na kufuatilia mara kwa mara kwa simu na kutembelea ofisini kwao.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani kabla ya kujiuzulu aliliambia Mwananchi kuwa TCRA ilitoa leseni kwa kampuni tatu (multiplex operators) zilizotakiwa kurusha matangazo ya idhaa tano za kitaifa bila ya malipo ya mwezi.
Ngonyani alisema leseni zilizotolewa kwa ajili kurusha matangazo zilihususha kampuni zinazouza ving’amuzi vya Digitek, Ting, Continental na Startimes.
“Wanaotumia satellite kurusha matangazo kama Azam, Dstv, na Zuku wao kwa kila mwisho wa mwezi ni lazima ulipie ili kupata chaneli zote zikiwemo za ndani,”alisema Ngonyani.
Alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu watu milioni 1.5 wametumia ving’amuzi vyao kupata taarifa hawa ni wale ambao wanatumia Ting, Startimes, Continental na Digitek.
Ngonyani alibainisha kuwa takwimu hizo ni sehemu ya watu 2.65 milioni wa Tanzania Bara ambao wanatumia ving’amuzi mbalimbali kujipatia taarifa huku akiwataka wananchi kutambua aina mbili za ving’amuzi ambavyo wanatumia.
“Mimi ni mmoja wa watu 1.5 milioni wanaotumia ving’amuzi vinavyotakiwa kutoa chaneli tano za ndani bure na tangu nimenunua sijapata tatizo hilo la chaneli za ndani kutokuonekana,” anasema.

No comments:

Post a Comment