Jarida la Time limewataja wanawake waliozungumza hadharani na kufichua kuhusu visa vya unyanyasaji wa kimapenzi kuwa "Mtu Mashuhuri wa Mwaka".
Limewataja kwa pamoja na "Waliovunja Kimya".
Kundi hilo lilihusishwa pia kwa karibu na kitambulisha mada #MeToo ambacho kilichipuka kuzungumzia tuhuma zilizofichuliwa dhidi ya mwandaaji wa filamu wa Hollywood Harvey Weinstein. Wanawake walitumia kitambulisha mada hicho kuzungumzia yale waliyopitia binafsi.
Lakini Time wamesema kitambulisha mada hicho kilikuwa "sehemu ya taswira, lakini si taswira kamili".
"Hili ndilo wimbi la mageuzi ya kijamii lililovuma kwa kasi zaidi ambalo tumeshuhudia katika miongo kadha," alisema mhariri mkuu Edward Felsenthal.
Ameambia runinga ya NBC kwamba wimbi hilo "lilianza kwa vitendo binafsi vya ujasiri vya mamia ya wanawake - na wanaume kadha, pia - waliojitokeza kuzungumzia waliyopitia."
Jarida hilo limechapisha picha za baadhi ya wanawake, wa kutoka asili mbalimbali.
Wasanii wawili wamejumuishwa - Ashley Judd, miongoni mwa waliozungumza wa kwanza dhidi ya Weinstein, na mwimbaji wa pop Taylor Swift, aliyeshinda kesi ya unyanyasaji dhidi ya DJ wa zamani aliyemshika makalio.
Kuna pia Isabel Pascual, 42, ambaye huchuma matunda Mexico (si jina lake halisi), Adama Iwu, 40, ambaye ni mtetezi wa haki katika kampuni na mashirika Sacramento na Susan Fowler, 26, mhandisi wa zamani Uber ambaye alimwangusha aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa Uber.
Rais wa Marekani Donald Trump ametajwa kuwa wa pili. Alipewa hadhi hiyo mwaka jana baada yake kushinda urais.
Utamaduni wa kumtaja mtu mashuhuri wa mwaka ulianza 1927.
Wengi wamekuwa watu binafsi lakini wakati mwingine makundi hutambuliwa.
Mwaka 2014 walitambua walichangia kupigana na Ebola.
Mwaka 2011 waandamanaji walioshiriki maandamano yaliyosababisha mageuzi mataifa ya Kiarabu.
No comments:
Post a Comment