Wednesday, November 15

Zuma awasihi wanajeshi Zimbabwe kutulia


Johannesburg, Afrika Kusini. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amelitaka Jeshi la Ulinzi Zimbabwe kuimarisha utulivu na kujizuia kufanya mambo yaliyo kinyume cha protokali ya umoja huo.
“Rais Jacob Zuma, kwa niaba ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), ametoa wito wa utulivu na kujizuia na ameelezea matumaini yake kuwa kinachofanyika Zimbabwe hakitasababisha mabadiliko ya serikali kwani itakuwa kinyume cha msimamo wa Sadc na Umoja wa Afrika,” imesema taarifa yake.
Rais ameitaka serikali ya Zimbabwe na Jeshi la Ulinzi la Zimbabwe (ZDF) kutatua mgogoro wa kisiasa kidugu na pia amelitaka jeshi kuhakikisha kwamba amani na usalama wa nchi havitetereki.
Amesema Sadc itaendelea kufuatilia kwa karibu sana hali na iko tayari kusaidia inapobidi kutatua mgogoro wa kisiasa kwa kuzingatia protokali na taratibu zilizowekwa na Sadc.
Zuma ametoa kauli hiyo baada ya askari na vifaru kuonekana jana wakiranda katikati ya jiji la Harare na ilipofika usiku zikatolewa taarifa na picha zilizoonyesha wamezingira majengo kadhaa ya serikali yakiwemo ya Shirika la Utangazaji Zimbabwe (ZBC).
Mapema alfajiri leo msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Sibusico Moyo alitoa taarifa kupitia ZBC akisema jeshi limechukua udhibiti likilenga “wahalifu” wanaomzunguka Rais Mugabe ambao walikuwa “wakifanya uhalifu uliosababisha mateso ya wananchi kijamii na kiuchumi ili kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.”
Katika taarifa yake hiyo, Moyo alisema Mugabe na familia yake wako “salama na wenye afya njema na kwamba ulinzi wao ni wa uhakika.”
Akisisitiza kwamba hayo hayakuwa mapinduzi, Moyo alisema “mara watakapokamilisha kazi hali itarejea kuwa ya kawaida”.
“Tunawahimiza mtulie na dhibitini mienendo isiyo ya lazima. Hata hivyo, tunawahimiza wafanyakazi na wanaojihusisha na biashara muhimu katikati ya jiji kuendelea na shughuli kama kawaida,” alisema Zuma.

No comments:

Post a Comment