Thursday, November 2

WANYANYUA VYUMA, WALIMU HATARINI

WATU 6,000 hadi 8,000 kila mwezi wanatibiwa maumivu ya mgongo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, Othuman Kiloloma alisema hayo jana katika mahojiano maalumu na MTANZANIA.
Dk. Kiloloma alitaja baadhi ya makundi ya watu walio hatarini kupata matatizo hayo kuwa ni pamoja na wabeba mizigo, ‘wanyanyua’ vyuma, walimu na wafanyakazi migodini.
“Mwalimu anakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupata maumivu ya mgongo iwapo kwa mfano wakati wa usahihishaji madaftari akikaa mkao ambao si rafiki kwa uti wa mgongo ni lazima atapata tatizo hilo.
“Unakuta mwalimu ana rundo la madaftari na wengi husahihisha wakiwa wameinama ni makosa makubwa,” alisema Dk. Kiloloma.
Akizungumzia kundi la wanyanyua vyuma, alisema wanapaswa kuwa na wataalamu wanaoitwa ‘trainers’ wanaojua jinsi ya kunyanyua
Vyuma vizito.
“Ni hatari, ingawa zipo pia sababu zitokanazo na matatizo ya kimaumbile yaani unakuta mifupa ya mgonjwa husika inakuwa haijakaa sawasawa wakati wa uumbaji, hasa kundi la watoto,” alisema.

Daktari huyo alisema wapo wanaopata maumivu ya mgongo kwa sababu ya uvimbe au saratani.

“Watu ambao wana matatizo ya damu (Gout Rheumatoid Arthritis) hizo ‘inffections’ za kwenye damu zinaweza kumsababishia mtu kupata matatizo ya mgongo,” alisema.

Alisema mbali na walimu, wanyanyua vyuma na mizigo pia huwa wanapokea wagonjwa ambao wamewahi kufanya kazi migodini.

“Utu uzima nao (watu wenye umri mkubwa) mara nyingi hupata matatizo ya mgongo.

“Ikiwa mtu anahitaji kunyanyua kitu kizito kilichopo chini, kwa mfano kreti la soda anapaswa kuchuchuma ndipo anyanyue lakini wengi huwa wanainama ndipo wanyanyue, ni makosa makubwa.
“Uzito wa mwili uliokithiri nao huweza kusabisha athari kwenye mgongo wa muhusika na hivyo kupata maumivu.
“Mgongo ni sehemu ya mwili ambayo huwa inabeba uzito wa mwili hivyo unapokuwa na uzito mkubwa tambua kwamba unajiweka kwenye hatari ya kupata maumivu ya mgongo,” alifafanua.
Wakati huo huo, MOI imefanikisha upasuaji wa watoto 20 kati ya 309 wenye matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema hayo jana katika mahojiano yake na MTANZANIA.
“Upasuaji ulifanyika kwa mafanikio makubwa na watoto wanaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment