Sunday, November 5

Wanaharakati wa kulinda mazingira waandamana Bonn

 Maelfu ya waandamaanji walikusanyika mjini Bonn Jumamosi kabla ya kuanza kwa mkutano wa kimataifa unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi mjini humo.

Klimakonferenz Bonn Demonstrationen gegen Kohle (Getty Images/S. Gallup)
Mkutano huo wa mazingira unaanza Jumatatu Novemba 6, na utadumu kwa wiki mbili zijazo hadi Novemba 17. Kiasi ya watu 25,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa kimataifa.
Suala la kuachana na uzalishaji wa makaa ya mawe Ujerumani ni moja wapo ya vipengele muhimu vinavyojadiliwa katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano kati ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na vyama vengine vya kisiasa , Chama cha walinda mazingira cha  Kijani na chama kinachoelemea upande wa biashara cha Free Democrats.
Waaandaji wa maandamano hayo wapatao 20,000 wameitolea wito serikali ya Ujerumani kutekeleza makubaliano ya mwaka 2015 yaliyofikiwa mjini Paris yenye lengo la kuhakikisha katika karne hii, uchumi wa dunia hautegemei mafuta na inachukua hatua kupunguza ongezeko la viwango vya joto duniani.
Ujerumani huenda isifikie malengo
Data za hivi karibuni zinaonesha kuwa Ujerumani itashindwa kufikia lengo lake la kupunguza kwa asilimia 40 kiwango cha gesi chafu ya Carbon Monoxide ifikapo mwaka 2020. Miongoni mwa waliondamana ni wanachama wa mrengo wa kushoto, vyama vya kisiasa vinavyolinda mazingira, vyama vya wafanyakazi na makundi yanayoipinga utandawazi.
Klimakonferenz Bonn Demonstrationen gegen Kohle (Getty Images/AFP/S. Gallup)
Utekelezaji wa mkataba huo utajadiliwa katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa unaofanyika mjini Bonn, utakaowaleta pamoja wajumbe wa nchi 196 wanachama wa umoja huo. Makubaliano ya Paris yaliyofikiwa 2016 yanalenga kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili.
Taarifa kutoka makundi 100 ya kiraia imesema maisha ya mamilioni ya watu duniani yako hatarini kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa kuna baadhi ya visiwa huenda vikapotea kabisa kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji ya bahari.
Mkataba wa Paris utafikiwa?
Mashirika hayo yanataka hatua za dharura kuchukuliwa kuepusha hatari hizo ikiwemo kuanza kupunguzwa kwa kiwango cha nishati itokanayo na mafuta na pamoja na makaa ya mawe. Makaa hayo ya mawe yanachangia kwa karibu thuluthi moja ya matumuzi ya nishati duniani na inachangia asilimia 40 ya umeme unaozalishwa, hiyo ikiwa mara mbili ya ile ya gesi asilia.
Ikilinganishwa na gesi na mafuta, makaa ya mawe yanachafua mazingira zaidi. Nchini Marekani utumiaji ya makaa hayo umepungua ambako sasa matumizi ya gesi ya asilia yanashika kasi, japo sio kwa kiwango cha kuridhisha.
Mkutano huo muhimu wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi unafanyika wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza nchi yake inajiondoa kutoka mkataba uliofikiwa mwaka jana mjini Paris, Ufaransa, wa makubaliano ya kihistoria ya tabia nchi na hivyo kuibua mashaka na wasiwasi kuwa huenda hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani, taifa lenye nguvu duniani ikahujumu kufikiwa kwa malengo ya makubaliano hayo.

No comments:

Post a Comment