Thursday, November 9

Walio kwenye ndoa za 'njoo tuishi' kuadhibiwa Burundi

Picha ya harusi mwaka 2015 mjini BujumburaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionBurundi ni moja ya nchi maskini zaidi duniani na baadhi ya raia wanasema hawawezi kumudu gharama ya sherehe za harusi
Watu wanaoishi katika mahusiano ya mume na mke bila kufunga ndoa nchini Burundi wameamrishwa kwamba wawe wameoana rasmi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu la sivyo wataaadhibiwa vikali.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya ndani na elimu Terence Ntahiraja amesema amri hiyo itasaidia kile alichokitaja kuwa ni ongezeko la watu nchini Burundi.
Amesema mahusiano yasiyo rasmi yamesababisha wasichana wengi wa shule kupata ujauzito na wanaume kupata fursa ya kuwa na mahusiano ya wanawake wengi kwa mkupuo.
Rais Pierre Nkurunziza, ambaye ni muumini wa kilokole , hivi karibuni alianzisha kampeni ya kitaifa ya maadili mema .
Burundi imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu mwaka 2015 Rais Nkurunziza alipotangaza kwamba angewania urais kwa muhula mwingine.
Waziri Ntarihaja ameambia AFP kwamba ndoa zilizorasmishwa kanisani au katika afisi ya serikali ndiyo suluhu pekee kwa tatizo la ongezeko kubwa la watu nchini humo na kwamba ni jukumu la kizalendo.
"Tunawataka raia wa Burundi wafahamu kwamba kila mtu anawajibikia maisha yake, na tunataka utulivu na utawala wa sheria humu nchini," alisema.
"Juhudi zote zinafanywa kwa kufuata mkakati wa kuwafunza raia wawe wazalendo," alisema, akirejelea mpango huo wa kueneza uzalendo uliozinduliwa na Rais Nkurunziza.
Haijabainika ni adhabu gani ambayo watapewa wale ambao hawatakuwa wamerasmisha ndoa zao kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mkulima mmoja ameambia AFP kwamba maafisa wa serikali tayari wamemtishia yeye na mpenzi wake kwamba watatozwa faini na kwamba mtoto yeyote atakayezaliwa bila wawili hao kufunga ndoa rasmi hawataruhusiwa kufaidi kutoka kwa mpango wa elimu bila malipo au huduma ya matibabu.
Mkulima huyo aliyejitambulisha kwa jina moja pekee kama Pierre, alisema ameshindwa kuoa rasmi kwa sababu hangeweza kulipa mahari aliyoitishwa na familia ya mpenzi wake.
Mamia ya watu walifariki tangu Bw Nkurunziza alipoanza azma yake ya kutaka kutawala kwa muhula wa tatu mwaka 2015.
Lakini miezi ya karibuni, hali ya utulivu imerejea.

No comments:

Post a Comment