Sunday, November 5

Wajawazito wasafiri umbali mrefu kufuata upasuaji


Madaba. Wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoa wa Ruvuma wamesema wajawazito wamekuwa wakisafiri umbali wa kilometa 127 kutoka eneo hilo kwenda Songea Mjini kufuata huduma ya upasuaji.
Kutokana na changamoto hiyo, wameiomba Serikali kuwasaidia kujenga chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Madaba ili kuepuke kero ya kufuata huduma hiyo Songea Mjini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanawake wanaoishi Madaba walisema ujenzi wa chumba hicho ulioanza muda mrefu lakini haujakamilika.
Mmoja wa wanawake hao, Esta Mlelwa mkazi wa Kijiji cha Mtepa alisema wajawazito wamekuwa wakikabiliwa na kero hiyo hali inayowalazimu kutumia pesa nyingi kusafiri kwenda kujifungulia mjini.
Alisema iwapo Serikali itaharakisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, itasaidia kuokoa maisha ya wajawazito kwa kuwa baadhi wamefariki dunia kwa kukosa huduma hiyo kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Mkazi wa Madaba, Agnes Myoka alimshukuru mbunge jimbo la Madaba, Joseph Mhagama kwa jitihada zake za kusaidia wajawazito kupata huduma bora za afya kwa kupeleka vitanda vya kujifungulia katika kituo hicho, magodoro, viti vya kubebea wagonjwa na gari la wagonjwa ili kupunguza changamoto zinazoikabili halmashauri hiyo.
Katibu wa afya wa kituo hicho, Yasinta Peter alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, chumba cha kupumzika wajawazito na upungufu wa wahudumu wa afya.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Shafii Mpenda alimshukuru mbunge wa Madaba kwa kutoa ushirikiano kusaidia kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alisema amechaguliwa na wananchi ili awasaidie kutatua kero zao ikiwa ni pamoja na kuwapelekea huduma za kijamii karibu.
Alisema licha ya kuwa na mfuko wa jimbo, lakini ameamua kutumia nguvu zake kwa lengo la kuleta maendeleo jimboni humo.

No comments:

Post a Comment