Wednesday, November 22

Wadau wataka mamlaka ya elimu, Mkapa azungumzia mfumo




       Rais mstaafu, Benjamin  Mkapa     
       Rais mstaafu, Benjamin  Mkapa      
Dodoma. Wakati wadau wa elimu wakipendekeza kuundwa kwa mamlaka ya kusimamia sekta ya elimu ili iendane na mkakati wa uchumi wa viwanda, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema nchi haijaweka msukumo katika kutafakari mfumo wa elimu.
Akizungumza katika kongamano la wanataaluma Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) jana, Mkapa alisema jamii ni lazima ikiri kazi kubwa inayofanywa na wakufunzi ambao wanaifanya katika mazingira magumu na changamoto nyingi.
“Hatuwezi kuridhika mno na kufikiri kuwa ni sawa, sote tunatambua jinsi mataifa yaliyoendelea yalivyofanya kuweza kufika walipo hivi sasa,” alisema.
Alitoa mfano wa mataifa kama Singapore, Korea Kusini na Vietnam ambayo yalitumia nguvu ya ziada katika kutoa elimu bora na kufanya mageuzi.
“Walifanya mapinduzi ya elimu. Walitumia rasilimali, wakafanikiwa. Bila shaka na sisi tunaweza tukafanya hivyo pia,” alisema.
Mkapa aliishauri Serikali kuviongezea fedha vyuo vikuu nchini ili vijikite katika utafiti wa kina kwenye ajenda ya maendeleo.
Alisema kufundisha na kujifunza pekee hakutoshi, bali vinatakiwa kutoa huduma ya utafiti ambayo itasaidia kulielekeza Taifa katika ajenda za maendeleo.
“Elimu itaendelea kuwa msingi na kiini katika Taifa kwenye ajenda ya maendeleo ya Taifa masikini. Ni kamba ambayo inawafunga watu pamoja,” alisema.
Wadau wa elimu UDSM
Katika kongamano jingine lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, John Kalage alisema mamlaka itakayosimamia elimu itawezesha kusaidia mabadiliko yanayofanywa na watunga sera.
Kongamano hilo lililoanza juzi na kumalizika jana ambalo lilikuwa linajadili umuhimu wa sera ya elimu ya ujamaa na kujitegemea katika kuelekea uchumi wa viwanda liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na shirika la HakiElimu.
Katika kongamano hilo, wadau wa elimu walipendekeza kuundwa kwa mamlaka ya kusimamia sekta ya elimu ili kuwezesha elimu inayotolewa iendane na uchumi wa viwanda.
Kalage alisema mamlaka itakayoundwa itasimamia elimu, itawezesha kusaidia mabadiliko yanayofanywa na watungasera kufanyiwa upembuzi kabla ya kuingizwa katika mfumo rasmi wa utekelezaji.
“Kuna baadhi ya mambo tunajadili leo, lakini si mapya. Kuna wakati waziri anakuja na kubadili mfumo bila kufanya tafakuri na uchambuzi wa kina kwani unaathiri mamilioni ya Watanzania kwa hiyo tukiwa na mamlaka ya kusimamia elimu, itatuwezesha kutoa elimu iliyo bora,” alisema Kalage.
“Tutakapokuwa na chombo hicho, kitaweza kusaidia kufanya upembuzi kwa kina na kitaweza kubaini tumefikaje hapa tulipo na tunatokaje,” alisema.
Mwenyekiti wa kongamano hilo, Jaji Joseph Warioba alisema mapendekezo yaliyotolewa, ikiwamo kuupitia mfumo wa elimu yatakuwa na tija kwa kuwa yatawezesha kubaini changamoto zilizopo na jinsi ya kuzitatua.
“Tunapaswa kutoa elimu iliyo bora na tunatakiwa kuwa na mwelekeo wa aina ya elimu tunayoitoa. Ni imani yangu, Serikali ambayo tumekuwa nayo toka jana (juzi) hadi leo itatusaidia kuyatumia mapendekezo na kuyaingiza katika sera na kanuni na kuona itaboreshaje elimu,” alisema Jaji Warioba ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu.
Jaji Warioba aliungwa mkono na mchangiaji wa mada, Dk Joviter Katabaro aliyesema kama nchi inataka kutoa elimu, basi ianzishe vyuo vya ufundi katika kila wilaya ambavyo vitawafundisha vijana kwa vitendo na shule ya mfano ya sayansi kwa kila wilaya kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda.
“Tanzania ya viwanda inahitaji watu wenye ujuzi na mbinu mbalimbali kuanzia ngazi ya chini, na vyuo hivi vya ufundi ni muhimu sana. Wazazi au walezi wakuze vipaji vya watoto wao,” alisema Dk Katabaro.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Jangwani, Ashura Mohamed alisema: “Vipaji vya wanafunzi vinapaswa kuendelezwa. Wapo wanaotaka kuwa waimbaji, wapo wanataka kuwa wachezaji. Si wote wanaokwenda shule ambao wanataka kuwa kama wanavyotaka wazazi au walezi wao. Kwa hiyo mzazi aendeleze kipaji cha mtoto wake.”
Kwa upande wake, naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya alikubaliana na ushauri wa wadau.
“Michango mingi iliyotolewa ina lengo la kujenga, kwa hiyo Serikali inayapokea na imani yangu tutafikia Tanzania ya viwanda,” alisema naibu waziri huyo.   

No comments:

Post a Comment