Saturday, November 4

Wabunge wa Chadema, CCM kunguruma Iringa


Iringa. Wakati Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akiongoza uzinduzi wa kampeni za Chadema za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa, Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde anatarajia kuzindua za CCM.
CCM inayozindua kampeni kesho Jumapili Novemba 5,2017 imemsimamisha Baraka Kimata aliyehamia chama hicho baada ya kujiuzulu udiwani wa kata hiyo na kujiondoa Chadema.
Sugu ananguruma leo Jumamosi Novemba 4,2017 akimnadi mgombea wa Chadema, Bahati Chengula.
Katibu wa Uenezi wa CCM Manispaa ya Iringa, Edol Bashiri amesema mbali na Lusinde, wabunge wengine watakaoshiriki uzinduzi huo ni Ritta Kabati na Zainab Mwamwindi ambao ni wabunge wa Viti Maalumu.
“Tumejipanga na maandalizi yote yameshakamilika, tunachosubiri ni uzinduzi wa kampeni kesho. Tumeshaanza kazi Kitwiru na kinachosubiriwa ni ushindi tu,” amesema.
Amesema kampeni itazinduliwa katika Mtaa wa Nyamuhanga A, Magengeni kuanzia saa saba mchana hadi saa 12:00 jioni.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema wanatarajia kuzindua kampeni leo na kwamba, mbali na Sugu, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche atakuwepo.
Amesema uzinduzi utafanyika katika Mtaa wa Kitwiru C.

No comments:

Post a Comment