Tuesday, November 14

Wabunge 40 wapanga kumng’oa Waziri Mkuu Uingereza


London, Uingereza. Wabunge wapatao 40 kutoka chama tawala cha Conservative inadaiwa wako tayari kutia saini barua ya kutokuwa na imani na kiongozi wao Waziri Mkuu Theresa May.
Gazeti la Independent limesema endapo wabunge wanane wataongezeka hivyo wakawa 48, idadi hiyo itakuwa inatosha kushinikiza kuanzishwa mchakato kamili wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye na hatimaye kuondolewa.
Gazeti la Metro limeripoti kwamba idadi hiyo iliongezeka katika wiki za hivi karibuni kutoka 35 baada ya May kutoa hotuba isiyoridhisha na chama kukabiliwa na ongezeko la kashfa tangu ulipoitishwa uchaguzi mkuu wa mapema Juni 8. Waziri Mkuu ameshuhudia mawaziri wawili, Michael Fallon na Priti Patel wakijiuzulu kipindi cha wiki moja.
Mbali ya kashfa ya ngono, mawaziri kujiuzulu na kosa lililofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje Boris Johnson lililochangia mwanamke mwenye uraia wa Uingereza, Nazanin Zaghari-Ratcliffe kukabiliwa na kifungo kirefu zaidi nchini Iran, mvutano kuhusu Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit ni miongoni mwa mambo yaliyoongeza hofu ndani ya chama katika kiwango ambacho May anashindwa kukidhibiti.
Watu wengi sasa wanaamini Waziri Mkuu ni hasara katika mchakato wa Brexit na wengine wanafikiri Conservatives wanahitaji kukaa kipindi kirefu kwenye upinzani ili wajiunge upya.
Waziri mmoja aliliambia gazeti la Independent: “Inatisha kuzungumzia jambo hili lakini nionavyo tunakaribia sana kwenye nukta ambayo tunapaswa kukaa muda wa kutosha kwenye upinzani ili kujirekebisha.”
Mwingine alisema: “Uvumilivu umepungua sana na katika namna fulani umekatika.”
Taarifa nyingine iliyochapishwa na gazeti la Sunday Mail imeelezea barua ya siri kutoka kwa Johnson na Waziri wa Mazingira, Michael Gove inayomtaka May kushinikiza mipango migumu ya Brexit.
''Ikiwa tunataka kukabiliana na wale wanaotaka kuuharibu mchakato huo, kuna njia za kusisitiza kuhusu namna ya kulitatua hilo,'' imesema barua hiyo na wamewambia May ''afafanue mawazo'' ya mawaziri walioko katika baraza lake la mawaziri ambao wanaunga mkono mipango mepesi katika mchakato wa Brexit.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Johnson na Gove wametaka mipangilio ya kipindi cha mpito kwa ajili ya nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ikamilike Juni 20, mwaka 2021.
Mambo haya yamekuja baada ya washauri wa EU kutishia kuzuia mazungumzo ya biashara hadi Machi mwakani labda Uingereza ikubali viwango ilivyopangiwa katika mpango wa Brexit. Mshauri mkuu katika mazungumzo ya Brexit, Michel Bariner ameiongezea presha serikali baada ya kuipa muda wa wiki mbili tu.

No comments:

Post a Comment