Hayo yamedhihirika katika ziara ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho ambayo imeingia wiki ya pili katika mikoa mbalimbali ambako uchaguzi wa marudio unafanyika.
Katika ziara hizo, viongozi hao na wengine wa vyama vingine vya siasa huzungumza na wananchi wa kata hizo pamoja na kuwanadi wagombea udiwani huku wananchi wakionekana kutamani kusikia kinachoendelea kwenye ulingo wa siasa za mageuzi nchini.
Hilo halina ubishi katika msafara wa kampeni za Chadema kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano na kusababisha misafara mirefu ya pikipiki, baiskeli na wengine kujipanga kando ya njia wakipungia mkono kuonyesha ishara ya vidole viwili.
Hayo yameonekana katika maeneo mengi hata vijijini ndani, katika maeneo ya Mtwara Mjini, Masasi, Rungwe, Mbeya, Tunduma, Sumbawanga, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro.
Katika baadhi ya maeneo, polisi wameamua kutumia mabomu ya machozi katika baadhi ya maeneo kama Mwanza na Moshi kuwatawanya mashabiki waliojitokeza kuwalaki viongozi, Edward Lowassa na Mbowe.
Kutokana na hali iliyojitokeza mkoani Mtwara, Mkazi wa Kata ya Reli, Emmanuel Kagenzi anasema, “Ni kama ndoto, tuliambiwa mkutano utakuwa saa tisa alasiri, lakini nimefika hapa tangu saa sita mchana, lengo ni kuhakikisha napata majibu ya maswali niliyokuwa nayo.
Anasema haamini kama nchi imefikia ilipo kiasi cha wananchi kushindwa kuzungumza na viongozi wao na kusikia misimamo na mwelekeo wa vyama vyao kutokana na zuio la mikutano ya kisiasa alilosema linawakosesha haki yao ya msingi.
Katika uwanja wa mkutano uliofanyika Kata ya Chanikanguo, wilayani Masasi ambako Mbowe alimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, James Kaombe umati wa watu ulionekana kuzidi ule wa Mtwara.
“Nimewahi na familia yangu, nilitaka kusikia mambo mengi na undani na ukweli kuhusu tukio la (kupigwa risasi) Tundu Lissu.
“Nimesikia kwenye vyombo vya habari, lakini mwenyekiti wetu ambaye tunamshukuru kwa kutuokolea jembe letu ana maelezo mazuri, ametueleza kuwa Lissu hayupo kwenye hatari ya kifo na anaendelea vema,” alisema Azidu Juma.
Juma anasisitiza kuwa wapo pamoja na viongozi wao licha ya kuwakosa katika majukwaa ya siasa kwa zaidi ya miaka miwili.
Kadri ziara ilivyoendelea ndivyo mapokezi ya Mbowe yalivyokuwa yakiongezeka. Katika Kata ya Ibhigi wilayani Rungwe mkoani Mbeya watu waliongezeka zaidi na katika baadhi ya maeneo walitanda barabarabi wakitaka mwenyekiti huyo azungumze nao.
“Haya ni madhara ya kutaka kuwaweka watu ndani ya chupa wasizungumze, hata mtoto ukimfungia muda mrefu anaweza kupoteza uelewa na kujifunza anavyoviona tu hata kama ni tabia za wanyama,” anasema Mbowe.
Hali hiyo iliendelea katika wilaya ya Momba Kata ya Ndalambo, mkoani Songwe ambapo wananchi walimpokea Mbowe kilomita 20 kabla ya kufika eneo la tukio.
Muda mwingi wakati anahutubia, Mbowe alilazimika kuzuia mihemko ya furaha ya wananchi ili waweze kusikilizana.
Kwa upande wa Kusini na Nyanda za juu Kusini, funga kazi ilikuwa Rukwa katika Kata ya Sumbawanga Asilia ambako Jeshi la Polisi lililazimika kuharakisha kumuondoa kiongozi huyo wa Chadema.
Katika uwanja wa Momoka ambako alihutubia kumnadi mgombea udiwani, kulijaa watu hadi ungeweza kudhani ni kampeni za kuwania urais.
Gari la Polisi lenye askari wenye silaha lilitangulia mbele, katikati la Mbowe na lingine nyuma na kwa umbali na kumsindikiza kwa kilomita tano ambako walishuka na kumtaka Mbowe na msafara wake kuondoka eneo hilo haraka kuelekea Iringa.
Lissu aibua simanzi
Mapema katika mkoa huo, kila wakati Mbowe alipokuwa akimtaja Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana shangwe iligeuka simanzi.
Kila anapopita ilionekana watu walikuwa wanataka kufahamu nini kilitokea kwa Lissu, kila Mbowe alipotaka kuzungumzia hakutumia nguvu kuwatuliza wananchi, walinyamaza wenyewe huku baadhi yao wakisikika wakieleza masikitiko yao.
“Mbowe ameokoa kiumbe tulicholetewa na Mungu kama zawadi, Lissu ni wa kipekee ni zawadi kutoka mbinguni,” alisema Zephania Kalinga mkazi wa kata ya Sumbawanga Asilia mkoani Rukwa.
Mbowe alitumia mikutano hiyo kuelezea kilichotokea na hali ya Lissu ambaye bado anaendelea kupatiwa matibabu nchini Kenya.
Utekelezaji ahadi
Wananchi katika maeneo mengi walionekana kutaka kufahamu hatma ya ahadi walizoahidiwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku Mbowe akiwataka kuacha ushabiki wa kisiasa kwenye mikutano, badala yake waitumie kuwabana watawala wanapokwenda kuwaomba kura.
“Kuna suala la milioni 50 kila kijiji, kuna suala la wazee, watoto kutibiwa bure, dawa kupatikana kila kona, hayo ni miongoni mwa mambo mnayopaswa kuhoji badala ya kushangilia na kupuliza mavuzezela kwenye mikutano ya watawala,” anasema Mbowe
Akizungumzia suala la ahadi Mkazi wa Mtwara, Johari Kidugo (46), anasema chama tawala kinapaswa kujitafakari kabla ya kurudi na kuomba kura hata ya uchaguzi mdogo wa madiwani.
Anasema hafahamu watakuja na sera na ahadi gani ilihali zile walizotoa hazijatimia. “Sikatai yapo mazuri wanafanya, lakini yanamezwa na hali ngumu ya wananchi, kama hakuna unafuu katika maisha ya mwananchi wa kawaida” alisema Kidugo.
Akizungumzia mwamko wa wananchi kwenye kampeni hizo, Mbowe anasema unatokana na kilichotokea baada ya uchaguzi mkuu 2015 baada ya taifa kukumbwa na ganzi na wananchi wakibaki na maswali mengi juu ya matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema kabla hawajakaa vizuri majukwaa mawili muhimu ya kuwapa taarifa wananchi, matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na mikutano ya hadhara, yalizuiwa.
Aliongeza, wapinzani walichoambulia ni kamatakamata, kufungwa, kubezwa na kutumika nguvu nyingi isiyohitajika dhidi yao.
Alisema hamu kubwa ya wananchi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo imechangiwa na kukaa miaka miwili bila mikutano ya hadhara.
“Hili unaweza kuliona katika mikutano hii, si mashabiki tu wa Chadema wanaojaa kwenye mikutano, bali wa vyama vyote, huku wote wakiwa wahanga wa kunyimwa haki yao muhimu kikatiba,” anasema Mbowe.
No comments:
Post a Comment