Wanawake wa Freemason wamekuwa wakikongamana kwa zaidi ya miaka 100 sasa - wakifanya matambiko na sherehe sawa na wenzao wa kiume.
Lakini si watu wengi wanaofahamu kuwepo kwa kundi hili. Sasa tunaweza kukufahamisha zaidi kuhusu shughuli za Freemason hawa wa kike baada ya kipindi cha redio cha Victoria Derbyshire cha BBC kuruhusiwa kuzungumza nao.
"Freemason ni nani?" anauliza mmoja wa viongozi wao ambao huitwa master (gunge) katika Kongamano Tukufu la Jumuiya ya Freemason wa Kale.
"Ni mfumo wa kipekee wa maadili ambao umezingirwa na istiari na ishara zenye maana," anajibu Dialazaza Nkela.
Nkela anashiriki katika sherehe ya kipekee ya kumfikisha ngazi ambayo hufahamika kama "shahada ya pili".
Ni sherehe ya kusherehekea kupanda hadhi kwake katika kundi lake.
Kufikia kwake "shahada ya kwanza" kuliadhimishwa kwa kuingizwa kwake katika kundi hilo, shughuli ambayo ilihusisha yeye kuweka wazi "mkono wake wa kulia, ziwa lake la kulia na goti la kulia" kitanzi kikiwa kimewekwa kwenye shingo lake.
Kila sehemu ya tambiko hilo, hudaiwa kuwa na maana yake - ingawa hatukufahamishwa zaidi.
"Shahada ya tatu" hudaiwa kuwa "pale unapokumbana na kifo ili kuzaliwa upya" na huwakilishwa na "mwisho wa uhai mmoja na kuanza kwa maisha mengine".
Maana ya hili pia, wanaweka siri.
Lakini ufichuzi huu wenyewe ni kidokezo kuhusu shughuli na imani za kundi hili lenye usiri mkuu.
Watu wengi hata huwa hawafahamu kwamba kuna mafreemason wa kike.
Freemason wa kiume - ambao walianza rasmi mikutano yao zaidi ya miaka 300 - wamekuwa wakiangaziwa zaidi.
Kwa sasa huongozwa na mwanamfalme mtawala wa Kent.
Lakini ukijumlisha makundi mawili yaliyopo ya freemason wa kike - Honourable Fraternity of Ancient Freemasons na Order of Women Freemasons, ambayo yaligawanyika mapema karne ya 20 - kuna karibu mafreemason wa kike 5,000.
Wanachama wa Order of Women Freemasons hukutana mara kwa mara katika mahekalu au nyumba kote nchini Uingereza.
Wakati wa sherehe zao, wanawake huvalia gauni ndefu za rangi nyeupe pamoja na mapambo shingoni kuashiria cheo cha kila mwanachama.
Ibada zao huanza kwa msafara kwenye njia kuu ya kuelekea kwenye madhabahu ndani ya hekalu.
Wanachama wa kundi hilo huinama wanapofika pale mbele, ambapo huwa ameketi mkuu wao ambaye hufahamika kama grand master (gunge mkuu).
Grand master (Gunge mkuu) wa sasa ni Zuzanka Penn ambaye huketi katika kiti kikuu ambacho hufanana na kiti cha enzi.
Huwa kuna maombi wakati wa ibada zao, na wakati mwingine unaweza kuhisi kana kwamba hilo ni kundi la kidini, ingawa Bi Penn anasisitiza wkamba hilo si kundi la kidini.
"Ili uwe wa Freemason, lazima uwe umeamini katika kiumbe (au roho) mkuu," anasema, lakini unaweza kuwa katika "imani (dini) yoyote ile".
"Huwa tuna watu ambao wana imani sana kidini, na wengine ambao hawafuati sana dini - lakini ni watu wa asili mbalimbali, au imani mbalimbali," anasema.
Wengi wa wanawake wamasoni huwa wana miaka 50 na kwenda juu - jambo ambalo wanataka sana kubadilisha.
Kwa sasa, wanawatafuta wanawake vijana, wakiwemo wale waliojiunga na vyuo karibuni, wawe wanachama.
Mtaalamu wa macho Roshni Patel anafanyiwa sherehe ya kumfanya kuwa wa ngazi ya Mastre katika kundi hilo.
Alijiunga na Freemason miaka saba iliyopita.
Hatukuruhusiwa kuhudhuria sherehe hiyo, lakini tunafahamu kwamba alipewa "heshima" ya kuketi kwenye kiti kile kinachofanana na kiti cha enzi.
"Shughuli yote ya kuwekwa kwenye kiti hicho, ilikuwa ya kuteka hisia sana," anasema, akiondoka.
"Hasa kwa wanachama wote wa nyumba yetu, ambao wananidhamini sana."
Alipoulizwa kuhusu kuwa Freemason wa ngazi ya master (gunge), aliongeza: "Bado nina mshangao," huku akijaribu kukubali uhalisia wa ufanisi wake.
Lakini kikwazo kikuu zaidi pengine kwa wale wanaotaka kujiunga na kundi hilo huwa ni sifa zake za usiri mkuu pamoja na kuhusishwa kwake na ufisadi.
Kadhalika, tuhuma kwamba wanachama wa kundi hilo hufaana na kusaidiana ili kufanikiwa katika taaluma zao mbalimbali pamoja na biashara.
Hili si jambo ambalo Bi Penn analitambua.
"Nimekuwa wa Freemason kwa zaidi ya miaka 40 na sijawahi kuahidiwa chochote na mtu au kumfaa mtu mwingine yeyote (kwa sababu ni wa Freemason).
"Huwa unasikia hadithi hizi, lakini sijawahi kusikia kisa chochote kama hicho katika Freemason kamwe."
Mwaka 1997, kulikuwa na wito kutoka kwa waziri wa mambo ya ndani wa wakati huo Jack Straw kwa maafisa wa serikali na majaji kufichua kwa hiari iwapo ni wanachama wa Freemason.
Mpango huo ulifutiliwa mbali baada ya Freemason kutishia kuishtaki serikali ya Uingereza.
Christine Chapman, gunge mkuu (grand master) wa Honourable Fraternity of Ancient Freemasons, anasema ingawa wana "maafisa kadha wa polisi (ambao ni wanachama)...sijaona yeyote akisaidiwa [kwa sababu ya kuwa mwanachama]".
Lakini kwa muda mrefu kumekuwa na tuhuma kwamba kundi hilo huhusika katika ulaji rushwa katika idara ya polisi na idara ya mahakama.
Kanuni za kimasoni husema wanachama wanafaa kusaidiana na kufaana na kuweka siri za kisheria za wanachama wenzao. Hii imewafanya wengi kuwa na wasiwasi wa kutumiwa wka kundi hilo kuendeleza ulaji rushwa.
Takwimu muhimu kuhusu Freemason
- Kuna takriban wamasoni 4,700 wa kike Uingereza, ukilinganisha na takriban wamasoni 200,000 wa kiume
- Wafreemason hukutana katika hekalu ambalo pia huwa wanaliita "lodge" (au nyumba). Inafahamika kwamba huko ndiko waasi wa kale walikuwa wanakutana wakifanya kazi ya ujenzi wa kanisa
- Huwa wanavalia aproni maalum za kimasoni, utamaduni unaotokana na imani ya jadi kwamba wamasoni walitokana na waashi, ambao walikuwa wanavalia aproni maalum kujilinda dhidi ya mawe wakifanya kazi ya ujenzi
- Ngazi ya "shahada ya tatu" huwa ni ngazi ya mwisho katika kuwa mmasoni kamili. Sherehe ya kuingiza mtu katika ngazi hii huhusisha kuhojiwa vikali, ambapo wazo la kumpa mtu "shahada ya tatu" huwa na asili yake.
- Mafreemason maarufu ni pamoja na Sir Winston Churchill, Sir Arthur Conan Doyle, Rudyard Kipling, Robert Burns, Oscar Wilde na Peter Sellers
Bi Chapman anasisitiza kwamba usiri wa Freemason hutokana na haja ya kuunda mvuto fulani na pia upekee fulani na si "kuficha uovu fulani".
"Hatuna mipango ya kujaribu kutwaa udhibiti wa ulimwengu, licha ya dhana hizi ambazo huenezwa na watu waongo mtandaoni, na hatujaribu kupindua serikali au mambo kama hayo.
"Tunahitaji kuhifadhi kiasi fulani cha usiri kwa sababi hilo ndilo hufanya kundi letu kuwa maalum."
Moja ya mambo maarufu kuhusu umasoni huwa ni salamu zao - na kwa hilo hakuna tofauti kwa wanawake pia.
"Ndio, bila shaka [tuna salamu zetu za kipekee]," anasema Bi Penn, bila kueleza salamu hizo huwa vipi.
"Ni siri yetu. Ni lazima ujiunge nasi kisha nitakwambia huwa zinahusu nini," anasema, huku akitabasamu.
No comments:
Post a Comment