Katika siku za karibuni kumeanza kuongezeka chuki na uadui baina ya wanasiasa wa upinzani na chama tawala.
Chuki hizi zinajengwa kutokana na kauli na matendo ya wanasiasa wetu jambo ambalo si jema kwa mustakabali wa Taifa.
Tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, wanasiasa wa vyama vyote, wamekuwa ni marafiki na walibishana kwa hoja nyakati za kampeni na baadaye walikaa pamoja.
Tulizoea kuwaona wanasiasa wakishirikiana kwenye matatizo kama ugonjwa, misiba na majanga mengine.
Hata kwenye vikao vya bunge, huwa tunawaona wakibishana kwa hoja ndani ya bunge na wakitoka nje utawakuta wakiwa pamoja.
Wakiwa Dodoma wamekuwa wakinywa pamoja na hata kwenda mnadani kula nyama pamoja, kwa dalili tulizoziona kwenye uchaguzi uliopita hali imeanza kubadilika.
Haikuwa ajabu kuona wanasiasa wakipigana hadi damu kumwagika, baadhi wakitekwa na wengine wakijeruhiwa kwa vipigo. Tambo ni nyingi huku kauli za kusaka maridhiano ili kurejesha misingi ya siasa za kistaarabu zikionekana kuwa mbali. Kwa bahati mbaya, viongozi wastaafu na viongozi wa dini ambao ni nguzo kuu katika kurejesha umoja na mshikamano katika taifa nao wamekaa kimya. Ukimya wa viongozi hawa unaweza kutafsiriwa kwa namna mbalimbali, inawezekana wana hofu ya kusimama hadharani na kusema hapana au wanapenda hali hii.
Lakini pia ukimya wao inawezekana wamekata tamaa na kuamua kuacha mambo yaende kama yalivyo lakini nina hakika ipo siku wataulizwa.
Imeanza kuzoeleka sasa, kuona viongozi wa kisiasa wakisimama majukwaani na kutoa kauli za uongo ulio dhahiri na hakuna ambaye anasimama kuwarekebisha.
Wanaojua ukweli na wenye mamlaka ya kusema hapana, ndani ya vyama vyao, wamekuwa kimya na wakiacha bora liende ili tu kusaka ushindi au kuungwa mkono.
Bahati mbaya hali hii inawagusa wanasiasa vyama vyote, hakuna jema ambalo linafanywa na chama kimoja na kupongezwa na chama kingine.
Malumbano yanaongezeka na walio na nguvu wameongeza matumizi ya nguvu hizo ili kuwadhibiti wenzao.
Hakika sasa tunajiondoa taratibu kwenye siasa za Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alipenda siasa za maridhiano na kuruhusu watu kushindana kwa hoja. Katika uchaguzi mkuu mwaka 1995 mara baada aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani na kugombea urais, alikuwa na mvuto wa ajabu.
Watu walimbeba mitaani, walifunga maduka kumfuata lakini wakawa wanabughudhiwa na polisi, lakini Mwalimu akiwa katika kampeni za kumsaidia mgombea urais wa CCM wakati huo, Benjamin Mkapa, aliwataka wanaombeba Mrema waachwe waendelee kumbeba hata wakipokezana kama maiti, kwani watu wanaobebwa juu wanajulikana hali zao.
Maneno hayo, yalipunguza matukio ya kumbeba Mrema bila kutumia nguvu na hakika hizi ndio siasa ambazo tumezizoea, kuruhusu nguvu ya hoja kushinda. Tanzania kwa miaka mingi inasifika kwa ustaarabu wa watu wake, watu wa mataifa mengi wamekuwa wakija kujifunza ustaarabu wa Watanzania. Viongozi na wanasiasa wa Tanzania kwa miaka mingi wamekuwa ni mfano wa kuigwa duniani, matendo na kauli zao, vimekuwa ni dira katika kutatua migogoro hasa katika nchi za Afrika.
Ipo siku vyama vya siasa vitaondoka lakini Tanzania itaendelea kuwapo.
No comments:
Post a Comment