Historia inasema ndege za abiria zinazopaa angani, meli kubwa za mizigo zinazoelea juu ya bahari bila kuzama licha ya kuwa na uzito kuzidi sarafu ya Sh100, magari, treni, mashine za kitabibu kama vile X Ray, CT Scan na MRI, majengo marefu kama Mnara wa Babeli, kompyuta, smartphone, mikorogo inayotumiwa na wanawake kubadilisha rangi ya ngozi, umeme, mabomu ya nyukilia na kila kitu kilichokuja baada ya Mungu kukamilisha kazi ya kuumba dunia, vilibuniwa na binadamu.
Sayansi nayo inatuambia kwamba, kula, kulala, kutembea, kukohoa, kufikiria na kila kitu kinachofanywa na binadamu huanzia kwenye akili iliyofichwa ndani ya ubongo—kwa hiyo, hata vyote vilivyobuniwa na wanadamu vilianzia huko. Halafu sasa, sayansi inafunga kwa kutupa tetesi kwamba, eti, kwa yote yaliyofanyika duniani, yalitumia takriban asilimia 10 tu ya akili ya mvumbuzi, yaani hadi hivi sasa, hakuna binadamu aliyewahi kutumia zaidi ya asilimia hizo za akili. Hii ni sawa na kusema kama itatokea mmoja kati yetu akatumia asilimia mia moja ya akili yake, huenda nae akatengeneza ‘kijisayari’ chake nje ya dunia na kuumba ‘binadamu’ wake huko.
Lakini sasa kupitia hii sayansi ya matumizi ya akili kuna swali linaibuka. Kama sote tunatumia si zaidi ya asilimia kumi, mbona maisha yetu yanatofautiana? Kuna wengine wanaishi kama wanatumia asilimia 50 ya akili zao na wengine ni kama hawana kabisa ubongo.
Lakini tafiti zisizo rasmi zinadai kinachotokea ni kwamba, mgawanyo wa matumizi ya akili zetu ndiyo unaoamua namna tutakavyoishi. Na kinachotufanya wengi tuishi kana kwamba hatuna hata hizo asilimia 10 zinazodaiwa huwa tunatumia ni jinsi ambavyo kiasi kikubwa tunakipelekea kwenye mambo yasiyo ya msingi.
Kwa mfano, kuna watu wana nyumba ndogo za kutosha kwa zaidi ya miaka kumi na wake zao hawajui. Mtu anazaa hadi watoto huko na anawahudumia na mke yupo tu, haelewi A wala Ba kwa sababu mume amejitahidi kuficha. Hii haiwezekani kirahisirahisi tu, inahitaji utumie zaidi ya asilimia saba ya asilimia kumi ya akili tunazotumia binadamu wa kawaida.
Ili kumudu mwanamke zaidi ya mmoja na isitokee wakajuana inahitaji kwanza uwe na kumbukumbu za kutosha kukumbuka kila uongo uliomwambia mke wako ili usichanganye na uongo utakaomwambia kimada, pia inahitaji akili za kukariri majina na uwezo wa kukumbuka ili hata siku moja, isitokee uko na mkeo Mama Neema, ukamuita kwa jina la Kimada wako, kitawaka.
Ukubali ukatae, nguvu unayotumia kumiliki mwanamke zaidi ya mmoja na hawajuani, ungeitumia kwenye mambo ya msingi, mbona na wewe ungekuwa umeshavumbua hata katreni kako kanakopaa angani – na ingependeza zaidi.
No comments:
Post a Comment