Rais Donald Trump wa Marekani amejitolea kuwa mpatanishi wa mzozo wa Bahari ya Kusini ya China inayowaniwa na mataifa sita ya kusini mwa Asia, huku China ikisema itashirikiana na wenziwe kuutatua mzozo huo.
Akizungumza katika mkutano wake na Rais Tran Dai Quang mjini Hanoi hivi leo (Novemba 12), Rais Trump alisema kama akiombwa, basi yuko tayari wakati wowote "kuwa mpatanishi" wa mzozo huo.
Vietnam imekuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya madai ya China kwamba ndiyo pekee yenye umiliki wa Bahari ya Kusini ya China, na hasa hatua ya taifa hilo kubwa kwenye eneo hilo kujenga visiwa vya kubuni na kuweka vituo vya kijeshi kwenye bahari hiyo, ambayo hutumika kusafirisha bidhaa za dola trilioni 3 kwa mwaka.
Hata hivyo, Trump alikiri kwamba msimamo wa China kwenye mzozo huo umekuwa tatizo kubwa, lakini anaweza kutumia ushawishi wake na wa nchi yake kufikia suluhisho. "Mimi ni mpatanishi na msuluhishaji mzuri," alijisifia.
Vietnam pia imeshaichukuwa ardhi inayozunguka miamba na visiwa vya Bahari ya Kusini, ingawa si kwa kiwango ambacho China imefanya. Sambamba na Vietnam na China, mataifa ya Brunei, Malaysia, Ufilipino na Taiwan nayo pia yana madai kama hayo kwenye bahari hiyo.
China yasema itashughulika yenyewe
Rais Donald Trump wa Marekani akiwa na mwenyeji wake, Rais Xi Jinping, wakati wa siku za kwanza za ziara yake nchini China.
Kwa upande wake, Rais Xi Jinping wa China amesema nchi yake itashirikiana na mataifa ya kusini mwa Asia kulinda amani kwenye bahari hiyo. Akizungumza na mwenzake wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, kandoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) nchini Vietnman, Rais Xi alisema China inahitaji kuona amani, utangamano na maendeleo kwenye eneo hilo la Bahari ya Kusini.
Rais Duterte, ambaye nchi yake iliwahi kupeleka kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa dhidi ya China juu ya mzozo huo, amesema watalishughulikia suala hilo baina yao.
Bahari ya Kusini ya China ilijadiliwa mjini Beijing katika siku ya kwanza ya ziara ya Trump ya siku 12 barani Asia na waziri wake wa mambo ya nje, Rex Tillerson, alisema Marekani na China ziliambizana ukweli wa wazi.
Marekani imeikasirisha China kwa kuendeleza doria ya manuwari na ndege karibu na visiwa vinavyomilikiwa na China.
Mnamo mwezi Agosti, mawaziri wa mambo ya nje wa kusini mashariki mwa Asia na China walianzisha utaratibu wa mazungumzo juu ya Bahari ya Kusini ya China, hatua iliyopongezwa kama ya maendeleo, lakini inayoonekana na wengine kama mbinu ya China kuvuta muda wa kuimarisha nguvu zake baharini.
No comments:
Post a Comment