Sunday, November 12

TRA yataka taarifa za watu wanaotiliwa shaka


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wananchi wasikubali kupatiwa huduma na mtu wanayemtilia shaka.
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi ya TRA makao makuu imetoa taarifa hiyo kwa umma baada ya Novemba 3,2017 kumkamata mtu aliyejifanya kuwa mtumishi wa mamlaka hiyo.
TRA imesema Dunia Tema, mkazi wa Buguruni, alikamatwa akituhumiwa kujifanya mtumishi wa mamlaka hiyo na kutoa huduma kwa mteja ndani ya ofisi ya TRA Kariakoo – Gerezani jijini Dar es Salaam.
Mamlaka hiyo imesema baada ya mtu huyo kukamatwa alifikishwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi akituhumiwa kujifanya mtumishi wa umma.
TRA imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara moja katika vituo vya polisi na ofisi za TRA endapo watakuwa na shaka na mtu yeyote anayewahudumia.
Pia, mamlaka hiyo imewasisitiza wananchi wasikubali kupewa huduma zozote na mtu wanayemtilia shaka.
“TRA inapenda kuwakumbusha kwamba, watumishi wake wote wanapaswa kuvaa au kuwa na kitambulisho chenye majina na cheo wanapokuwa wanatimiza majukumu yao ya kila siku mahali popote,” imesema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment