Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza kutekeleza shughuli za uwajibikaji kwa jamii katika mwaka wa fedha 2017/2018 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshwaji wa Sekta mbalimbali kama Elimu, Afya, Maji na Utawala Bora.
Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu katika tukio la kukabidhi hundi za fedha kwa ajili ya kusaidia uimarishwaji wa Chama cha Maafisa Uhusiano Tanzania pamoja na kukabidhi fedha za kuwezesha ununuzi wa mafuta na dawa kwa Chama cha Wanawake Albino cha Ndugumbi lilofanyika tarehe 03 Novemba, 2017 Makao Makuu ya TPDC.
“Leo tunayo furaha ya kuanza rasmi shughuli zetu za uwajibikaji kwa jamii kwa kuhakikisha afya bora kwa ndugu zetu kutoka kikundi cha Wanawake Albino cha Ndugumbi kwa kuwapatia fedha za kuweza kufanya manunuzi ya dawa na mafuta ya kupaka ili kuimarisha afya ya ngozi zao na kujikinga dhidi ya maradhi ya Kansa na hivyo kurudisha tabasmu kwao na kuona kuwa Shirika lao la Mafuta la taifa linawajali na liko pamoja nao katika mapambano dhidi ya maradhi ya Kansa.” Msellemu alieza katika tukio hilo.
Meneja Mawasiliano wa TPDC akikabidhi hundi kwa Uongozi wa Chama cha Maafisa Uhusiano Tanzania.
Baada ya kupokea msaada wa fedha kutoka TPDC, Mwamvua Kambi ambaye ni Katibu wa Ndugumbi ametoa shukrani kwa TPDC kwa kuwajali na kuwasikiliza kilio chao maana kilio chao kikubwa ni Kansa ya Ngozi ambayo kwa dawa na mafuta watakazonunua zitasaidia kupunguza mionzi ya Jua ambayo ni hatarishi kwa afya za ngozi zao na kwa msaada walioupata ni mkubwa na unawatosha pamoja na wenzao katika kikundi.”
Aidha Meneja Mawasiliano alieongezea kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuboresha masuala ya Utawala Bora nchini, Shirika linaamini kuwa kwa kukisaida Chama cha Maafisa Habari wa Tanzania kitakua kimeimarisha eneo la Utawala Bora ambapo kupitia Kongamano la Maafisa habari ambalo litalenga kwenye kuimarisha mchango wao katika kuijenga Tanzania ya Viwanda wataendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuelimisha Umma wa Watanzania juu ya uwajibikaji wa kizalendo katika kuiletea Nchi Yetu Maendeleo ya kweli katika Sekta ya Viwanda.
David Mwaipaja ambaye ni Mratibu wa chama ametoa shukrani kwa mchango wa TPDC, “Tunashukuru saana kwa utayari mliounyesha wa kuhakikisha Chama cha Maafisa Uhusiano kinafikia Malengo yake na kiukweli matokeo makubwa kwa mlichokifanya leo hayataonekana leo hii lakini nafasi kubwa ya kushukuru itapatikana siku ya Mkutano Utakaolenga kuangalia Nafasi ya Maafisa Uhusiano katika Kuelekea Tanzania ya Viwanda ambapo mtapata nafasi ya kueleza umuhimu wenu au mchango wenu katika kuijenga Tanzania ya Viwanda”.
Meneja Mawasiliano wa TPDC akikabidhi hundi kwa Chama Ndugumbi Albino kwa ajili ya kuwezesha manunuzi wa mafuta ya ngozi.
Msellemu anansisitiza kuwa “kwa Mwaka huu wa fedha TPDC inatarajia kutekeleza ujenzi wa kituo cha Afya Tunduru, ujenzi wa vyoo kwa wananfunzi wenye ulemavu Shule ya Msingi Shangani na vyoo kwa Shule ya Msingi Kilwa Kivinje, ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Mingoji pamoja na kufadhili zoezi la upimaji wa afya kupitia Taasisi ya Moyo katika kuendesha zoezi la upimaji afya litakalofanyika Wilayani Luangwa Mkoani Lindi.”
Msellemu amefafanua kuwa hii si mara ya kwanza kwa TPDC kutekeleza jukumu lake la msingi katika uwajibikaji kwa jamii inayoizunguka ila ni mwanzo tu wa shughuli hizo kwa mwaka huu wa fedha.
“TPDC tumekuwa na utaratibu wa kutekeleza majukumu yetu kwa jamii toka huko nyuma ambapo tuliweza kuchangia madawati na viti kwa shule za Msingi na Sekondari kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam, ujenzi wa madarasa, mabweni, vyoo, ofisi za serikali za mitaa na n.k”.
TPDC kama Shirika la Mafuta la Taifa linao wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria za Nchi na kama Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 inavyoelekeza namna ya utekelezaji wa wajibu wa Sekta ya Mafuta na Gesi kwa jamii, Shirika litaendelea kutekeleza wajibu huo kwa lengo la kuhakikisha manufaa ya Gesi Asilia nchini yanapatikana kwa wananchi si kwa kutokana na mapato ya gesi asilia pekee kwa Serikali lakini pia kwa kuboresha Sekta za Elimu, Afya, Maji, Utawala Bora, Miundombinu na kadhalika.
Viongozi wa Chama cha Maafisa Uhusiano Tanzania na Chama cha Ndugumbi pamoja na Meneja na Maafisa wa TPDC mara baada ya makabidhiano ya Hundi katika Ofisi za TPDC Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment