Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson yuko Myanmar atakutana na Aung San Suu Kii na pia mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing. Tilleson atarajiwa kusisitiza kurudi Myanmar wakimbizi wa Rohigya.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani yuko nchini Myanmar kukutana na mkuu huyo wa jeshi la Myanmar jenerali Min Aung Hlaing. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson atakutana pia na kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi katika ziara yake hii ya kwanza nchini humo. Viongozi hao baadae wanatarajiwa kuwahutubia waandishi wa habari. Waziri Tillerson anatarajiwa kutoa mwito wa kumaliza matumizi ya nguvu katika jimbo la Rakhine. Majeshi ya Myanmar yanalaumiwa kwa kuitendea maovu jamii ya Waislamu walio wachache ya Rohingya.
Jeshi la Myanmar limekanusha vikali madai ya kukiukwa haki za binadamu za jamii ya Waislamu wa Warohingya wakati wa operesheni zilizofanywa baada ya Warohingya wenye msimamo mkali kufanya mashambulio mnamo mwezi wa Agosti. Warohingya zaidi ya laki 6 wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh tangu kuzuka kwa mashambulio dhidi yao.
Umoja wa Mataifa umeyaita kuwa ni mauaji ya kimbari. Afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amewaambia waandishi wa habari kwamba Tillerson anasisitiza kurudi salama nchini Myanmar kwa wakimbizi wa Rohingya. Hata hivyo haijulikani kama Tillerson atatoa vitisho vya kuwekwa vikwazo vipya dhidi ya jeshi la Myanmar.
Hivi karibuni bunge pamoja na baraza la Seneti nchini Marekani lilipitisha sheria ya kuizuia nchi hiyo kutoa msaada wa kijeshi kwa Myanmar. Sheria hiyo pia ililenga kuwawekea vikwazo vya kifedha na kuwanyima viza maafisa wa kijeshi wa Myanmar. Kaimu mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Phil Robertson amesema ni vizuri kuwachukulia hatua hizo maafisa wa jeshi la Myanmar.
Taarifa iliyotolewa mapema leo inasema maelfu ya Warohingya bado wanaendelea kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh. San Suu Kyi mwanaharakati wa muda mrefu wa demokrasia aliingia madarakani baada ya uchaguzi wa kwanza wa wazi kufanyika mwezi Novemba mwaka 2015 nchini Myanmar, lakini pia kiongozi huyo anakabiliwa na lawama za kimataifa kwa kushindwa kuutatua mzozo wa wakimbizi unaoikabili jamii ya Waislamu walio wachache wa Rohingya. Kunyamaza kwake kumemuharibia sifa ya kuwa kiongozi bora katika nyanja za kimataifa.
No comments:
Post a Comment