Miundombinu ya uchumi inajumuisha miradi ya usafirishaji na uchukuzi kama vile ujenzi wa reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, ununuzi wa meli, na ndege. Uwekezaji katika sekta ya umeme, afya, maji na elimu pia ni miundombinu miundombinu muhimu kutokana na mchango wake kwenye uchumi wa taifa.
Kuimarisha miundombinu ya uchumi ni pamoja na kuzuia baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ili kuimarisha na kuendeleza soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani pamoja kukuza sekta nyingine zinazohusiana na viwanda.
Soko la viwanda vya ndani likilindwa, litavijengea uwezo wa kuimarisha ubora na kuweza kushindana kwenye soko la kimataifa ambako kuna bidhaa za mataifa kutoka mataifa mbalimbali.
Nchi yeyote inayohitaji kukuza, kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya uchumi ni lazima ielekeze fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara za aina tofauti kuliko matumizi ya kawaida.
Kubana matumizi na kuhakikisha kila senti inayopatikana ama kwa njia ya misaada, mikopo au makusanyo ya ndani inaelekezwa kwenye shughuli iliyopangwa kwa kuzingatia thamani ya fedha ni jambo linalopaswa kuzingatiwa.
Tanzania sasa hivi imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya uchumi, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imejikita katika uendelezaji na uimarishaji wa miundombinu ya uchumi kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha ‘standard gauge’.
Mradi huu unatajwa kugharimu kiasi cha Sh16 trilioni mpaka utakapokamilika. Mradi mwingine ambao ni sehemu ya miundombinu ya uchumi ni ununuzi wa ndege ambazo zitaongeza idadi ya watalii pamoja na fedha zitakazokusanywa kutoka eneo hilo.
Tayari ndege mbili zimeshanunuliwa na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine nne zinatajwa kugharimu Sh227.6 bilioni yameshafanyika.
Licha ya kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea nchini kutokana na kurahisishwa kwa usafiri huo wa anga, ndege hizo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi marafiki wa kiuchumi.
Zikiwapo za kutosha zitakazokuwa zinaenda kwenye mataifa yamayofanya biashara zaidi na Tanzania, yatawapunguzia wajasiriamali gharama za kuunganisha ndege huku zikitoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani kuzitumia jambo litakaloongeza mchango wa sekta ya usafirishaji kwenye pato la Taifa.
Serikali pia inaendelea kupanua, kuboresha na kujenga viwanja vipya vya ndege sehemu mbalimbali nchini jambo litakalotoa nafasi kwa usafiri huo kuwahudumia wasafiri wanaofanya safari za ndani hata kimataifa.
Serikali pia inaendelea na mchakato wa kujenga bawawa la umeme la Stigler’s Gorge wakati usambazaji wa nishati hiyo vijijini ukiendelea. Dhamira iliyopo ni kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma hiyo ili kuwa chachu ya maendeleo vijijini. Kiasi cha Sh389.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) kwa kipindi Julai, 2016 mpaka Machi.
Barabara kadhaa zimeendelea kujengwa nchini kwa kiwango cha lami huku baadhi zikijengwa kwa changarawe kuhakikisha huduma ya usafiri na usafirishaji inakuzwa na kuimarishwa.
Ili kuendeleza usimamizi wa barabara na miundombinu yake na kuongeza mchango wake kwenye uchumi, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura).
Usafirishaji wa bidhaa hasa kutoka na kwenda vijijini ambako bidhaa nyingi huzalishwa ni changamoto iliyokuwapo kwa muda mrefu. Kadri inavyoshughulikiwa ndivyo maisha ya wananchi husika yanavyoendelea kuimarika.
Serikali inadhibiti upotevu wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengineyo ikiwemo Tanga na Mtwara. Pamoja na mambo mengine, inahakikisha bandari zinatumika kama lango kuu la kukuza uchumi.
Sekta ya elimu haijasahaulika, Serikali imeendelea kutoa elimu bure kwa Watanzania wanyonge na masikini kuanzia awali hadi sekondari mpango unaoigharimu wastani wa Sh18.77 bilioni kwa mwezi ambazo nisawa na Sh225.24 bilioni kwa mwaka.
Miradi mingi ya maendeleo inasimamiwa na kuendelezwa na Serikali. Kukuza, kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya uchumi ni sawa na kulima au kutafuta mali juani, tukitarajia kuvuna kisha kulia kivulini wakati ukifika.
Utekelezaji wa miradi hii huchukua muda mrefu mpaka kukamilika kwake. Baadaye huanza kufanyakazi na taratibu wananchi huanza kuona faida zake.
Baadhi huchukua muda mwingi kabla matunda yake hayajaonekana kwa wananchi. Tuendelee kuvumilia kwani mambo mazuri yanakuja.
No comments:
Post a Comment