Friday, November 10

Sitaki wadhifa wa Waziri mkuu, asema Raila Odinga

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, akisalimiana na aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Kenya Johnnie Carson mjini Washington DC. Novemba 10, 2017.
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, alisema Alhamisi kwamba haungi mkono azimio la baraza la makanisa ya Kenya(NCCK) la kutaka kubadilishwa kwa katiba na kubuniwa kwa nafasi ya Waziri mkuu, manaibu wawili na kiongozi wa upinzani bungeni.
Odinga aliyasema hayo wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mjini Washington DC.
Kabla ya mahojiano hayo, kiongozi huyo wa chama cha ODM alitoa hotuba kwenye ukumbi wa taasisi ya mambo ya kigeni, (Center for Strategic and Internatrional studies) katika hafla iliyohudhuriwa na wadau kadhaa.
"Mimi sitafuti kazi na huo ni mtazamo duni mno kwa suala hilo," alisema Odinga.
Mwanasiasa huyo alisisitiza kwamba muungano wa upinzani wa National Super Alliance, NASA, hautambui urais wa Uhuru Kenyatta na kutaka mikakati ya kufanya uchaguzi mpya uatakaokuwa "wa haki na kweli" iwekwe.
"Muhula wake uliisha rasmi tarehe Mosi mwezi Novemba," alisema.
Odinga alitaka kuwe na serikali ya mpito kwa kipindi ambacho mchakato wa kuhakikisha uchaguzi huo hautakuwa na dosari.
Kuhusu hoja zilizowasilishwa mahakamani kupinga uchaguzi wa tarehe 26 mwezi Oktoba, Odinga alisema uamuzi wa mahakama hautakuwa suluhisho kwa mzozo unaoikabili Kenya.
Aidha Odinga aklizikosoa nchi za Magharibi kwa kile alichokiita kutojali maadili ya kidemokrasia katika bara la Afrika. Alisema Marekani ni sharti ionyeshe azima ya kushinikiza nchi ambazo hazifuati mwongozo wa kidemokrasia.
Hafla hiyo iliongozwa na aliyekuwa balozi wa Mrekani nchini Kenya, Mark Bellamy.

No comments:

Post a Comment