Monday, November 6

SIRI BOMBERDIER NJE

SERIKALI imesema ifikapo Julai  mwakani, ndege zote zilizoagizwa zitakua zimeingia nchini tayari kuanza kazi.
Msemaji Mkuu wa Serikali,  Dk. Hassan Abbasi, amesema kwa sasa Serikali imejipanga   kuleta   ndege hizo na zitawasili Juni 2018.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana kuhusu mafanikio ya miaka miwili ya Rais Dk. John Magufuli madarakani tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka 2015.
Dk. Abbasi ametoa kauli hiyo huku hadi sasa ikiwa haijaelezwa  hatima ya kesi  ya ndege   ya Bombardier Q400 Dash 8, ambayo inadaiwa kuzuiwa  Canada kutokana na serikali kushindwa kutekeleza amri ya mahakama ya kimataifa ya kulipa fidia.
Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSD) iliyotolewa mwaka 2010 iliitaka Serikali kuilipa kampuni ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering Ltd dola  za Marekani milioni 25   na riba ya asilimia nane (Sh bilioni 87).
Kuhusu kesi zinazoikabili  Serikali, Dk. Abbasi, alisema kuna kesi mbili bila kutaja za aina gani;   moja ambayo Serikali imeshtakiwa na nyingine imeshtaki na   ipo katika hatua nzuri.
“Ndege kubwa kuliko zote itaingia Julai 2018 ambayo ndiyo ndoto ya serikali na kuhusu kesi siwezi kufahamu zote kwa sababu  kuna nyingine ni za  binafsi ingawa Tanzania imeshitaki na wao wameshitaki na na ipo katika hatua nzuri,” alisema.
Dk. Abbasi alisisitiza kuwa  ndege zote zilizoagizwa zikiwamo  Boeing 787, Bombardier CS300, Boeing 787 – 1 abiria 262 Bombardier 400 – 3 abiria 76, Bombardier CS300 – 2 abiria 132, zote zitaingia mwezi Juni.
Alisema dhamira ya serikali ni kulifufua Shirika la Ndege  na imefanya hivyo.
“Tunafufua Shirika la Ndege, tumeanza na juhudi hizo …  hadi kufikia mwakani ndege zote tulizoagiza zitakuja na hiyo uliyoitaja ipo kwenye  majaribio kwa maana ya vipimo na kufanyiwa ukaguzi, itakapokamilika itakuja nchini,’’ alisema.
WAFANYAKAZI HEWA
Msemaji huyo wa serikali pia alielezea mafaniko mengine kuwa ni pamoja na kudhibiti ufujaji wa fedha za umma hasa kwenye suala la wafanyakazi hewa ambako iliwaondoa  katika mfumo wa malipo wafanyakazi hewa takriban 20,000 na kuokoa  Sh bilioni 238.
Alisema wafanyakazi wenye vyeti feki takribani 12,000 wameondolewa katika mfumo wa serikali na kuokoa    Sh bilioni 142.9.
Hata hivyo akijibu swali la kuhusu uamuzi wa kusimamisha  ajira za watumishi wa kada ya afya waliopangiwa vituo vya kazi hivi karibuni katika halmashauri mbalimbali, alisema hatua hiyo inatokana na kufanya uhakiki na marekebisho na baada ya kukamilika zitatangazwa tena hivi karibuni.
Alisema marekebisho hayo ni pamoja na ukaguzi wa taaluma ili yasiweze kurudiwa makosa ya kuwa na wafanyakazi hewa na vyeti feki na baada ya hapo yatatangazwa tena.
VITA YA UFISADI
Alizungumzia mafanikio ya vita ya ufisaidi akisema ni pamoja na kuanzishwa kwa mahakama ya ufisadi na  kufanya usimamizi wa fedha za umma kuhakikisha zinazopatikana kutokana na jasho la walipakodi zinatumiwa ipasavyo ili kuleta faida kwa wananchi.
Alisema mahakama ya ufisadi imeanza kazi  kwa kasi kwa kuanzia mahakama za chini  zikiwamo kesi za  uhujumu uchumi katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mikoa mengine mbalimbali na hadi sasa kuna kesi 104.
Dk. Abbasi alisema kesi zenye maombi ya dhamana yaliyokamilishwa na kupelekwa mahakama ya uhujumu uchumi kwa uamuzi ni 77 na   tatu zimeanza kusikilizwa katika mahakama hizo.
MAZUNGUMZO MAKINIKIA
Mafanikio mengine  ni   mazungumzo ya historia na kampuni ya  Barrick    kwa kuwa katika mabadiliko yaliyofanyika, taifa  kwa sasa litapata hisa asilimia 16 na mgawanyo wa asilimia 50/50 wa faida katika migodi ya madini.
“Mazungumzo katika maeneo mengine kama Tanzanite na almasi yanakuja lakini tayari uzalishaji umeongezeka kutoka karati kati ya 15,000-18,000 hadi karati kati ya 28,000 na 32,000,’’ alisema Dk. Abbas.
SAFARI ZA NJE 
Msemaji huyo wa serikali, alisema serikali imefanikiwa kufuta safari za nje ya nchi sisizo za msingi    na matumizi yasiyokuwa ya msingi kwa viongozi na maofisa  wa umma yameshuka.
Alisema kwa mwaka 2014 -2015 takribani Sh bilioni 216 zilitumika  kwa mambo kama hayo   lakini kwa mwaka 2015 -2017 Sh bilioni 25 tu   zimetumika hadi sasa.
Aliyataja mafanikio mengine   aliyoita ya uamuzi mgumu  ambayo ni pamoja na kitendo cha serikali kuhamia Dodoma, ndoto aliyoiita ni ya miaka 44 iliyopita ambayo utekelezaji umefanyika sasa.
Mafanikio mengine  ni katika makusanyo ya kodi ambayo kwa mwaka  yameongezeka mwezi.
Alisema  hadi kufikia Juni mwaka huu zilikuwa zimekusanywa  Sh trilioni 15 zilikusanywa wakati mwaka 2015 zilikusanywa Sh trilioni 9.9.
Dk. Abbasi alisema kutokana na makusanyo hayo,   bajeti imeongezeka katika sekta zote hasa miradi ya maendeleo na  katika miaka miwili limekuwapo ongezeko la asilimia 40.
Alisema ongezeko hilo  ni kwenye sekta ya afya kwenye dawa na vifaa tiba ambako mwaka huu bajeti imekuwa Sh bilioni 261 wakati mwaka 2015 ilikuwa Sh bilioni 30.
“Mwaka 2016 serikali ilitenga  Sh bilioni 251 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba na yote ilitolewa katika vituo 268 vya afya wakati Hospitali ya Taifa Muhimbili imepata  CT-Scan mpya na hivi sasa inasaidia wagonjwa 50 kutoka 20 kwa siku.
“Bila kusahau elimu bure   serikali ikiwa inatoa Sh bilioni 20 kwa mwezi kugharamia ada, posho za wakuu wa shule, uendeshaji wa shule na chakula   na  Sh  bilioni 3 kwa ajili ya kugharamia mitihani ya  darasa la nne, saba, Form II na Form IV,   jumla zikiwa Sh bilioni 23,’’ alisema Dk. Abbasi.
Akizungumzia mafanikio katika elimu ya juu, alisema Serikali  inagharamia wanafunzi wenye uhitaji wa elimu ya juu kwa ada, matumizi na vifaa kwa   Sh bilioni 427 kutoka Sh bilioni 48.6 za mwaka 2015/16.
Alisema  kwa mwaka huu pekee wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa wameongezeka kutoka 28,785 hadi 30,000.
MIRADI YA MAJI
Kuhusu  miradi ya maji, alisema zimekwisha kutumika Sh bilioni 550   kwa ajili ya kutoa maji Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Tabora na jirani.
“Na pia   mradi wa maji Arusha umetumia Sh  bilioni 476  na katika miji 17 na Zanzibar miradi ya maji imegharimu Sh trilioni 1.2,” alisema.
BARABARA
Alisema Serikali imejenga takribani kilometa 1,500 za barabara na kutumia Sh trilioni 1.2 ambazo zote ni fedha za ndani, sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa itakayotumia trilioni 1.9.
UMEME
Dk. Abbasi alisema kuwa pia Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi ya historia ya umeme ambayo ni Kinyerezi I Extension ambayo mtambo wake unazalisha Megawati 185 za umeme ambazo zitaingizwa katika gridi ya taifa  ifikapo Novemba 2018.
UWEKEZAJI
Msemaji huyo wa serikali  alisifu maendeleo ya uwekezaji  nchini hasa katika kutekeleza sera ya ‘Tanzania ya Viwanda’ kama vile  kuanzishwa Kiwanda cha Chaki Maswa, Kiwanda cha Sayona Mwanza na vingine vingi.

No comments:

Post a Comment