Monday, November 13

Serikali yatishia kulivunja Baraza la Madiwani Kigoma Ujiji


Dodoma. Serikali imeionya Manispaa ya Mji wa Kigoma Ujiji kuacha kuendelea kuwasiliana na Mpango wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) na kama ikiendelea itachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuvunja Baraza la Madiwani.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kujiondoa katika mpango huo mapema mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema bungeni leo Jumatatu wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye chama chake kinaongoza manispaa hiyo.
Zitto katika swali lake la nyongeza amesema kuwa nchi za Hungary na Urusi ambazo Serikali inasema nazo  zimejitoa katika mpango wa OGP ni miongoni mwa nchi zinazoendeshwa kidikteta kwa kutofuata utawala bora.
"Nchi za Hungary na Urusi zinaendeshwa bila kufuata demokrasia zinaendeshwa kidikteta ni aibu sana kwa Serikali kusema inaiga nchi ambazo zinaenda kinyume na demokrasia," amesema.
Amesema majukwaa hayo ya kimataifa yanatengeneza mahusiano na kwamba Canada ni mwenyekiti wa mpango huo.
Hata hivyo, amesema juzi ameona Rais John Magufuli amemwandikia Waziri Mkuu wa Canada kuhusu suala la Bombardier.
"Serikali haioni kwamba ingeendelea kuwa mwanachama wa OGP na mwenyekiti ni Canada hili ombi lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi," amehoji Zitto.
Zitto amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa miji 15 duniani ambayo ipo katika mpango huo na kwamba Serikali inatoa kauli gani juu ya ushiriki wa mji huo  katika OGP ambayo imekuwa ikifaidika na mpango huo na miji mingine inayotaka kuingia katika mpango huo.
Akijibu hayo Mkuchika amesema Tanzania imejitia katika mpango kwa hiari yake  yenyewe na kwamba hawajaiga nchi yoyote.
"Sisi ni Taifa huru linalojitawala linalofanya matumizi yake yenyewe, bila kushurutishwa na Taifa lolote liwe dogo ama kubwa duniani," amesema.
Amesema Canada na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na pia Tanzania ina ubalozi wake na hivyo kuwa mwanachama wa OGP na kutokuwa mawasiliano na nchi hiyo haiwezi kuwa tatizo.
Amesema andiko la mpango huo linasema nchi ikijiondoa uanachama na washirika wake wote shughuli na uanachama unakoma.
Hata hivyo, amesema kuwa Serikali ina taarifa kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji bado inaendelea na mpango huo na OGP walimwandikia waziri wa mambo ya nje kuwa bado wana nia ya kuendelea na halmashauri hiyo.
"Sasa nataka kupitia Bunge lako tukufu kuionya Manispaa ya Ujiji kutoendelea. Nchi inayozingatia utawala bora haiwezi Serikali kuu ikafanya maamuzi lakini baraza la madiwani likasema haliwezi kutekeleza. Nataka nionye Halmashauri ya Kigoma Ujiji iache mara moja. Yale ni maamuzi ya Serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa Serikali itachukua  hatua kali za kisheria na nyinyi mnajua kwenye baraza la madiwani hatua kali za kisheria ni kulivunja baraza na kuunda Tume ya Manispaa," amesema.
Mkuchika ameomba madiwani na Zitto kutoifikisha Serikali huko.
Katika swali lake la msingi Zitto amehoji kwanini Serikali imeamua kujiondoa kwenye mpango huo.
Akijibu Mkuchika amesema Serikali imejiunga na mipango ya kikanda na kimataifa mbalimbali hivyo ni maoni yake kuwa shughuli zinazotekelezwa kupitia mipango hiyo mingine kupitia vyombo mbalimbali inatosha kwa nchi kujijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
Mkuchika amesema kujitoa katika mpango huo hakuna madhara yoyote.

No comments:

Post a Comment