Saturday, November 11

Senegal wafuzu kwa Kombe la Dunia Urusi kwa kulaza Afrika Kusini

Sadio ManeHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionSadio Mane alitekeleza mchango muhimu mechi hiyo
Senegal maarufu kama Simba wa Teranga wamefuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili baada ya kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Afrika Kusini katika uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane Ijumaa.
Watarejea Urusi kucheza miaka 16 baada yao kushangaza watu wakicheza katika Kombe la Dunia mara ya kwanza, michuano iliyoandaliwa Korea Kusini na Japan.
Sadio Mane, alirerejea mapema kutoka kuuguza jeraha, alichangia sana ushindi huo wa Simba wa Teranga.
Alitoa pasi safi kwa mshambuliaji wa West Ham Diafra Sakho aliyeweza kumbwaga kipa wa Bafana Bafana Itumeleng Khune, na kuwaweka Senegal kifua mbele katika mechi hiyo dakika ya 12.
Winga huyo wa Liverpool kisha alisaidia kushinda mechi hiyo kwa kuchangia bao la pili dakika mbili kabla ya muda wa mapumziko.
Kombora lake la karibu na goli lilikombolewa na Khune lakini mpira ulipodunda ukatumbukizwa wavuni na beki wa Afrika Kusini Thamsanqa Mkhize aliyekuwa anaanguka chini.
Bafana Bafana walijaribu kadiri ya uwezo wao kusawazisha kabla ya kufungwa bao hilo, Lebogang Manyama akigonga mwamba wa goli naye Percy Tau akishindwa kufunga mpira uliodunda na kuanguka miguuni mwake baada ya kipa wa Senegal Khadim Ndiaye kuzima kombora la Themba Zwane.
Wenyeji walijaribu kutatiza walinzi wa Senegal, safu ambayo ilikuwa inamkosa Kara Mbodji ambaye anatumikia marufuku, lakini walishindwa kuzalisha matunda.
Senegal walitumia nafasi zao chache kufunga na kushinda mechi.
Hatua ya Senegal kufuzu imemfanya kocha wa Senegal Aliou Cisse kujiunga na marehemu aliyekuwa nahodha wa Nigeria Stephen Keshi as kama watu ambao wamewahi kucheza na pia kuongoza timu ya Afrika kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Timu zote mbili zitakutana tena Dakar Jumanne katika mechi ambayo itakuwa tu ya kutimiza wajibu kwani Senegal wamejiunga na Nigeria na Misri katika orodha ya nchi ambazo zimefuzu Kombe la Dunia.

No comments:

Post a Comment