Majaji wa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita mjini The Hague, Uholanzi, wamemhukumu kifungo cha maisha kamanda wa zamani wa Bosnia na Serbia Ratko Mladic katika kesi ya mauaji ya halaiki iliyokuwa inamkabili.
Hii ni hatua iliyofunga ukurasa wa yale mauaji ya miaka ya tisini ya eneo la Balkan. Kesi ya Mladic ndiyo ya mwisho kutoka iliyokuwa Yugoslavia na uamuzi huo umekuwa ukisubiriwa na maelfu ya wahanga katika eneo hilo ambalo limegawika pakubwa.
Mladic ambaye alikuwa anakabiliwa na mashtaka 11 alishutumiwa kwa kuongoza kikosi kilichohusika na uhalifu ikiwemo mauaji mabaya zaidi ya vita hivyo, ambayo yalijumuisha uvamizi wa miaka mitatu wa Mji Mkuu wa Bosnia, Sarajevo, pamoja na mauaji ya halaiki ya mwaka 1995 ambapo wanaume na wavulana 8,000 wa Kiislamu waliuwawa katika eneo la Srebrenica. Hayo yalikuwa mauaji mabaya zaidi kuwahi kufanyika Ulaya tangu vita vya pili vya dunia.
Jopo la majaji watatu katika mahakama hiyo wamempa kifungo hicho Mladic mwenye umri wa miaka 75 baada ya kumpata na hatia.
Waendesha Mashtaka walitaka ahukumiwe kifungo cha maisha
Waendesha mashtaka walitaka ahukumiwe kifungo cha maisha ingawa mawakili wa Mladic walitaka aachiliwe huru na aondolewe mashtaka yote. Waendesha mashtaka walimtuhumu Mladic na mwandani wake wa kisiasa Radovan Karadzic kwa kutaka kufanya mauaji ya kimbari ambapo walinuia kuwaangamiza Wabosnia Waislamu na Wabosnia Wacroatia kutoka maeneo yaliyokuwa yanadaiwa kumilikiwa na Wabosnia Waserbia pia.
Munira Subasic, ni rais wa chama kinachojiita "Kina mama wa Srebrenica," ambao ni wahanga wa yaliyotokea katika miaka hiyo, "Bosnia na Herzegovina inahitaji uwiano, bila shaka inahitaji hili, lakini kivipi? Kupitia uamuzi wa sawa na wa haki, kupitia kuwahukumu wahalifu wa kivita kwasababu ya ukweli. Bila ya ukweli hakuna uaminifu na bila uaminifu, hakuna uwiano," alisema Subasic. "Haki, uaminifu na uwiano ni vitu vitakavyokuwepo iwapo wale wote waliofanya uhalifu na mauaji ya halaiki watahukumiwa na majina yao yajulikane kama ya wahalifu wa kivita, kama vile tu majina ya watoto wetu yanavyojulikana kama ya wahanga," aliongeza rais huyo.
Radovan Karadzic alipewa kifungo cha miaka 40
Katika kesi iliyosikilizwa kwa kipindi cha miaka mitano, karibu mashahidi 600 walijitokeza kutoa ushahidi wao na kuliwasilishwa zaidi ya nyaraka 10,000 za ushahidi.
Mzozo wa iliyokuwa Yugoslavia uliebuka baada ya kuvunjika kwa lililokuwa shirikisho la makabila tofauti katika miaka ya tisini, ambapo uhalifu mbaya zaidi ulitokea huko Bosnia. Zaidi ya watu 100,000 waliuwawa na mamilioni walipoteza maisha yao kabla mkataba wa amani haujatiwa saini mwaka 1995.
Rais wa zamani wa Bosnia Radovan Karadzic alipewa kifungo cha miaka 40 mwaka jana kwa kupanga mauaji ya Bosnia ingawa amekata rufaa kuhusiana na uamuzi huo.
Mladic alikuwa mafichoni baada ya vita hivyo na alisalia mafichoni hadi kukamatwa kwake nchini Serbia mwezi Mei mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment