Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kumiliki magari 19, mali inayodaiwa hailingani na kipato chake halali.
Jennifer ameshtakiwa chini ya kifungu cha 27, (1) (a) na (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Maelezo hayo yalipaswa kusomwa leo Jumanne Novemba 7,2017 lakini Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter amesema bado hawajamaliza kuyaandaa.
Ameiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine. Upande wa utetezi uliowakilishwa na wakili Elisaria Mosha haukuwa na pingamizi.
Hakimu Huruma Shaidi ameahirisha kesi hadi Desemba 6,2017, mshtakiwa atakaposomewa maelezo hayo.
Jennifer anadaiwa kati ya Machi 21,2016 na Juni 30,2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA kwa cheo cha Ofisa Forodha Msaidizi alikutwa akimiliki magari 19.
Magari hayo ni Toyota RAV4 mbili, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish mbili, Toyota Mark II, Toyota Mark X, Toyota Regiusage, Toyota Estimated, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry.
Katika hati ya mashtaka imeelezwa magari hayo yana thamani ya Sh197.601 milioni mali ambayo inadaiwa hailingani na kipato chake halali.
Anadaiwa kati ya Machi 21,2012 na Machi 30,2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA mwenye cheo cha Ofisa Forodha Msaidizi alikutwa akiishi maisha ya kifahari ya thamani ya Sh333.255 milioni fedha ambayo inadaiwa hailingani na kipato chake halali.
Mshtakiwa aliyekana mashtaka hayo baada ya kusomewa yupo nje kwa dhamana
No comments:
Post a Comment