Monday, November 13

Nyalandu asikitishwa na Waziri Kigwangala



Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu  amesema inasikitisha kuona Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla  akitumia muda  ndani ya Bunge kumchafua, kudhihaki na kusema uzushi na  uongo dhidi yake.
Nyalandu amejibu mapigo hayo leo Jumatatu ikiwa imepita saa kadhaa kwa Dk Kigwangalla kumtuhumu mbunge huyo wa zamani kwamba alitumia madaraka yake vibaya wakati akiwa Wazari wa Maliasili na Utalii katika Serikali iliyopita.
Amesema, "hizi ni njama za makusudi zilizopangwa  kunichafua mara baada ya mimi kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hatua hii imepangwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi yeyote wa CCM atakayethubutu ama kudiriki tena kuhama CCM,” amesema Nyalandu.
Nyalandu amedai kuwa Dk Kigwangalla anatumika vibaya kwa kauli za uongo dhidi yake mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Katika kujibu mapigo hayo Nyalandu ametoa hoja sita kuonyesha Dk Kigwangalla ana chuki dhidi yake na amelidanga Bunge kwa tuhuma dhidi yake.
Amesema Dk Kigwangalla amekejeli kuwa Nyalandu alitumia fedha za Serikali kusafiri  nchini Marekani na msanii wa bongo movie Aunt Ezekiel.
“Habari ilikuwa ya kuzushwa  na ilichunguzwa na vyombo vya dola mwaka  2014 na kuthibitika ilitungwa na katika mkutano huo wa Washington DC nilialikwa na  Balozi wa Tanzania, Marekani na nikapewa ruhusa ya maandishi na Serikali kuhutubia mkutano huo kwa siku moja. Wasanii wote walioalikwa, akiwamo Aunt Ezekiel hawakuwa na mwaliko wa wizara ama Serikali, bali waandaji wa kongamano. Na Serikali haikulipa gharama zozote kwao."
Amesema Dk Kigwangalla amelidanganya Bunge kuwa Nyalandu ametumia  helikopta kugombea urais
“Habari hii ni ya uzushi na  waziri atakuwa aidha hana busara ambayo angepaswa kujiridhisha na taarifa kabla ya kuisoma bungeni ama waliomtuma wamemwambia asome  hivyo hivyo. Ukweli ni kuwa  Nyalandu alipokuwa CCM niligombea katika kinyang’anyiro cha urais  na kuomba kuteuliwa ndani ya CCM na alitumia aidha usafiri wa magari au ndege za kawaida kwa kulipa nauli (fixed wings pale ilipobidi), hadi mchakato ulipoisha kama uilivyoisha."
“Miaka yote nikiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, nimekuwa nikifanya kampeni za kumalizia kwa njia ya helikopta. Inawezekana Waziri Kigwangalla hajawahi kupanda helikopta katika maisha yake, nimjulishe tu kuwa kwangu huo ni usafiri wa kawaida sana na umesaidia ilipobidi kusaidia kufika baadhi ya maeneo jimboni kwangu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2000, 2005, 2010, na 2015.
Amesema Dk Kigwangalla amezusha kuwa  Nyalandu alitumia vibaya madaraka yake. Amezungumzia suala la Waziri Nyalandu kutotia sahihi tozo mpya zilizopendekezwa na Tanapa
“Jambo ambalo Dk Kigwangalla angepaswa kulijua kabla ya kutoa kauli isiyo sahihi bungeni ni kuwa sakata la tozo za  Tanapa lilijadiliwa bungeni  na Spika Anne Makinda, likiwa limeletwa na Kamati ya Lembeli na kwa kupitia wizara na nililitolea ufafanuzi na likamalizika na GN ilitolewa.”
Akizungumzia vitalu Nyalandu amesema, "inasikitisha sana na inatia aibu kwamba Dk Kigwangalla atalihadaa Bunge kuwa Nyalandu amehusika na kuuza au kugawa  vitalu  na mbaya zaidi kwa njia ya rushwa."
Amesema Sheria ya Wanyamapori inatamka wazi kuwa vitalu vitagawiwa kwa wawindaji kila baada ya miaka mitano  na mara ya mwisho vitalu vilitolewa Januari, 2017 ambapo Nyalandu hakuwa waziri.
"Pia kabla ya hapo vitalu viligawiwa mwaka  2013. Nyalandu hakuwa Waziri."
“Hii ni aibu sana natumaini kwa Dk  Kigwangalla na wanaomtuma wangetamani sana miaka ibadilike ili isomeke Waziri Nyalandu,” amesema.
Nyalandu amesema Dk  Kigwangalla amedai kuwa yeye (Nyalandu) alikuwa anafanyia kazi katika chumba maalumu katika hoteli ya Serena.
“Naomba athibitishe ni chumba namba ngapi na wahusika wa hoteli pia wathibitishe kama waziri, nilifanya kazi katika ofisi yangu iliyopo Wizara ya Maliasili na Utalii. Kigwangalla pia akumbuke mimi nilikuwa mteule wa Rais ambaye alikuwa na vyombo vya kumsaidia kusimamia mawaziri."
Mwisho Nyalandu amesema  mbwembwe hizi na kusingiziwa kunakofanywa kwa makusudi baada ya  yeye kuhama CCM  ni aibu kwa Taifa  na ni matumizi mabaya ya madaraka.

No comments:

Post a Comment