Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema hayo bungeni leo Ijumaa Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo.
Halima katika swali lake amesema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.
"Serikali inasemaje kuhusu kuleta sheria itakayofuta tabia ya wenye nyumba kulazimisha kulipwa kodi ya mwaka?" amehoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Mabula amesema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.
Mabula amesema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.
Katika swali la msingi, Halima amesema kumekuwa na upandaji holela wa gharama za pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
"Je Serikali haioni kuna haja ya kudhibiti upandaji holela ambao unaathiri wananchi wengi kutokana na kipato chao?" amehoji.
Akijibu, Mabula amesema utaratibu wa urekebishaji wa viwango vya kodi za shirika hilo husimamiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia kodi ya pango na kuidhinisha viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wapangaji wa nyumba za shirika.
"Kwa mara ya mwisho bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa iliidhinisha viwango vipya vya kutoza kodi kwenye nyumba za shirika mwaka 2011 ambavyo ndivyo vinavyotumika mpaka sasa," amesema.
No comments:
Post a Comment